USHIRIKI MDOGO WA WATOTO WA KIKE WENYE ULEMAVU WA AKILI KWENYE MICHEZO

Wadau waanisha vikwazo, kimo cha mtazamo hasi, miundombinu isiyorafiki

Wenyewe wadai kutengwa, kuanzia ngazi ya familia, jamii

NA FATMA HAMAD, PEMBA

SERIKALI, ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa utaratibu mzuri wa kuwaendeleza watu wenye mahitaji maalum.

 Watu wenye ulemavu wamekuwa wakishiriki katika shughuli za michezo na kwa kiasi kikubwa wameweza kujipatia heshima wao na taifa, kwa kushinda katika mashindano mbali mbali.

 Licha ya juhudi za serikali katika kuhakikisha kundi hilo, linapata haki zao kama watu wengine hasa katika kushiriki katika mashindano yanayoandaliwa ndani na nje ya nchi, imekuwa tofauti kwa baadhi ya watu, kuwaficha watoto wa kike wenye ulemavu.

 Kwani wanayohaki ya kushirikishwa katika nyanja zote za kiuchumi, kama raia wote, bila ya kujali ulemavu wao, maana kinachoangaliwa sio ulemavu wao, ni haki zao na uwezo wao.

Haki ya kushiriki katika harakati za kimaendeleo, imeelezwa kwenye ibara ya 9 ya mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu ulioridhiwa na Tanzania mwaka 2009.

Na ndio maana, serikali, ikaweka muongozo ili maendeleo ya nchi yasiwaache nyuma kwa kuimarisha muundo wa tasisi za watu wenye ulemavu.

 WANAWAKE WENYE ULEMAVU

Asha Ali mwenye ulemavu  mkaazi wa Mkoani, anasema kikwazo kikubwa kinachopelekea mtoto  wa kike mwenye ulemavu wa akili kushindwa kushiriki michezo yao maalumu, ni wazazi kutokuwapa fursa.

‘’Wazazi hawana uwelewa juu ya suala la michezo, hivyo wanahisi wakitupa nafasi ya kutoka na kwenda kwenye michezo kitakacho kuja kukipata ni udhalilishaji,’’anasema.

Saada Hamada mwenye ulemavu mkaazi wa mamoja wilaya ya Micheweni anasema  wanawake wenye ulemavu wa akili, wamekua wakidharauiwa na kuonekana wao ni wa kufungiwa ndani.

‘’Bado jamii haijmpa nafasi mtoto wa kike na yeye kujichanganya na kucheza michezo kama wanavyofanya wanaume, wenye ulemavu,’’anafafanua.

Maulidi Khamis mwenye ulemavu wa viungo, anasema bado wanawake wenyewe, hawajahamasishwa vya kutosha kushiriki michezo.

Ingawa alishawahi kushiriki mashindano mara nne ya mpira wa miguu nje ya kisiwa cha Pemba, lakini  hakuna mwanamke yoyote alieingia kwenye mashindano hayo kupiti michezo mingine.

JAMII

 Juma Kombo Hija wa Micheweni, anaona bado jamii imekuwa ikiwachukulia mtoto wa kike wenye ulemavu wa akili, kwamba ni watu wa kusaidiwa, jambo ambalo sio sahihi.

‘’Unapo muelekeza kufanya kitu mtoto mwenye ulemavu wa akili, na yeye anafahamu na anaweza kufanya jambo, lakini hatuwapi fursa tunawafungia ndani tu tunaendelea kuwadumaza,’anaeleza.

Anakumbuka kuwa, zamani walikuwa nayo timu ya riadha ya wanawake wenye ulemavu, walishiriki mashindano lakini imekufa kutokana na kukosa kuungwa mkono.

Amina Omar Msellem wa Kichungwani Chake chake, anasema watoto wa kike wenye ulemavu wa akili, wanaendelea kuachwa nyuma, kwani wanaonekana wao hawana uwezo wa kufanya lolote lenye maslahi.

‘’Maranyingi tumekuwa tukiwachukulia watu wenye ulemavu wa akili, hawana marifa yoyote, hata tukiwalekeza hawawezi kufahamu, kutokana na mazingira yao,’’anasema.

Batuli Mussa Sharif kutoka Shehia ya Sizini alieleza kuwa watoto wakike wenye ulemavu wa akili, wamekuwa wakisahauliwa kupitia fursa tofauti, ikifikiriwa kuwa hana uwezo wa kuleta mabadiliko.

JUMUIA ZA WATU WENYE ULEMAVU

Afisa Utetezi baraza la Taifa la watu wenye ulemavu, wilaya ya Mkoani Warda Walii Mohamed, anasema bado kuna mtazamo potofu kwa jamii, na kuona ni kituko kuwashirikisha watu wenye ulemavu wa akili michezo.

‘‘Wazazi wamekua wakiwafungia ndani, wanaona hawana uwezo wa kushiriki kwenye michezo, tena hata ile maalum kwa ajili yao, jambo ambali sio sahihi,’’anasisitiza.

Moja ya mikakati yao, ni kuwashajiisha wanajamii kuwapa fursa, ili na wao washiriki michezo na kuingia katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Rashid Hamad Khamis Mwnyekiti wa jumuia ya watu wenye ulemavu  wa akili mkoa wa Kaskazini Pemba, anaona wazazi wenyewe wa watoto  wa kike wenye ulemavu wa akili, kama sehemu ya kikwazo kikubwa kuwashirikisha watoto wao katika michezo.

‘’Sisi viogozi tunahisi kama hatujawatendea haki wanawake wenye ulemavu wa akili, hivyo tumeamua kumpitia kila mzazi mwenye mtoto mwenye ulemavu, na kumshajiisha ili mashindano yanayokuja washiriki.

 Khatib Iddi Abdalla, ambae ni mwalimu wa michezo kisiwani Pemba, anasema jamii haina mwamko wa mtoto wa kike kushiriki kwenye michezo.

Ndio maana anasema ipo haja ya kutolewa elimu kwa jamii, ili fursa zilizomo kwenye michezo, zinapatikana kwa wanaume na wanawake.

WANAHARAKATI

Mratibu wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat- hiya Mussa Said, anaeleza kuwa mtoto wa kike mwenye ulemavu wa akili, hutafsiriwa kama mzigo, pale anaposhiriki michezo.

‘’Jamii wanaona mtoto mwenye ulemavu wa akili, kama vile hastahiki kushirikishwa michezo hasa kulingana na ulemavu wake,’’anafafanua.

 Saleh Hamad Juma kaimu Mkurugenzi wa jumuia ya Wasaidizi wa Sheria wilaya ya Micheweni anasema watoto wa kike wenye ulemavu wa akili hawashirikishwi kwa jambo lolote ikiwemo michezo. 

 

 ZFF

Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar ‘ZZF’  ofisi ya Pemba, Khamis Hmad Juma, anasema wameshaweka mkakati wa kuimarisha miundombinu kwa mtoto wenye ulemavu, ikiwemo kujengewa viwanja malumu.

Maana anakubali kuwa, sekta ya michezo ina fursa nyingi ikiwemo ajira, hivyo wakati umefika kwa jamii, kuwaruhusu watoto wanawake wenye ulemavu wa akili kushiriki michezo.

 

 WIZARA YA HABARI

Afisa Mdhamini wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mfamau anasema, watoto wa kike wenye ulemavu wa akili, hawashiriki michezo kutokana na kukosa viwanja vilivyo rafiki kwao.

Ingawa anakiri kuwa, wameshaweka mikakati ya kuwa na mazingira rafiki kuanzia kwenye viwanja, ili watu wenye ulemavu wa akili, na wao pate fursa ya kushiriki michezo. 

 Waziri wa wizara hiyo Tabia Maulid Mwita, anasema, tayari wziara imevisaidia vyama vitatu vya michezo ya watu wenye ulemavu, katika kuandaa na kushiriki mashindano, kadhaa yakiwemo ya taifa ya watu wenye ulemavu wa akili.

 Ambapo mashindano hayo yalifanyika mkoani Mwanza, na Zanzibar ilifanikiwa kupata medali 20, zikiwemo za dhahabu nane, fedha moja na shaba 11 kwa michezo tofauti.

Aidha wizara hiyo katika hutuba yake ya mwaka wa fedha 2023/2024, moja ya kipaumbele chake iliku ni kuimarisha miundombinu ya michezo kwa kufanya ukarabati mkubwa wa kiwanja cha michezo cha Amani na Gombani na kujenga viwanja vya michezo vya kisasa kwa kila wilaya.

Waziri Tabia anasema, kwa upande wa michezo ya watu wenye ulemavu wa mguu mmoja na mkono mmoja, Wizara imefanikiwa kulisaidia Shirikisho la mchezo huo, kushiriki mashindano ya Kitaifa yaliyofanyika Arusha.

Lakini hata Shirikisho la michezo ya Viziwi Zanzibar (SHIMIVIZA) limesaidiwa kuandaa bonanza, kwa ajili ya shamra shamra ya kuadhimisha siku ya viziwi duniani.

Sheria ya watu wenye ulemavu  namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 28 (9) kimesema watu wenye ulemavu wanayo haki ya kushiriki kwenye michezo na burudani.

TAMKO LA SERA YA MICHEZO YA MWAKA 2018

 Serikali itahakikisha Watu Wenye Ulemavu wanawekewa mazingira  Yanayofaa, kuwawezesha kupata fursa sawa na haki ya kushiriki mashindano  mbali mbali kwa uwezo wa hali zao.

 Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 21 (3) kila mzanzibari anayo haki ya kufanya kazi na anastahili fursa na haki sawa, kwa masharti ya usawa ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyoko chini ya mamlaka ya Zanzibar.

 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO