MAMA AJIFUNGUA NA KUMFUKIA MTOTO MCHANGA
NA FATMA HAMAD, PEMBA
Mama mmoja anayefahamika kwa jina la Mchanga Omar Said anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 mkaazi wa Kijiji cha Sizini Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba,anadaiwa kumfukia mtoto mchanga mara baada ya kujifungua.
Mama huyo akiwa kwa sasa ni mjane akiwa na watoto saba ambaye alitengana na Mwenza wake kwa zaidi ya miaka miwili ambapo kwa sasa anashiliwa na Jeshi la Polisi.
Akizungumza juu ya tukio hiilo Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Mgeni Khatib Yahya, alisema Jumamosi Mei 18 saa 5 asubuhi alipokea taarifa za mama huyo kuwa alijifungua na alichojifungua hakikuonekana, Wananchi walifuatilia suala hilo na kugundua kuwa mama huyo alijifungua na kisha kumfukia mtoto kibandani mwake.
Mkuu huyo wa wilaya alisema alimwita mama huyo na kuzungumza naye ambaye alimueleza kuwa sababu kubwa ya kumfukia mtoto wake mchanga ni umasikini unaomkabili kwani hana mtu wa kumtegemea ndio maana akaamua kuchukua uamuzi huo.
Mgeni alisema maamuzi aliyochukua mama huyo sio ya kiutu na ni kitendo cha jinai. Alichokifanya ni ukatili unaoangukia chini ya sheria ya mauaji, kwa hiyo Serikali itamchukualia hatua stahiki kwa kitendo hicho.
Hata hivyo alisema Mama huyo alihofia kupata aibu kwa jamaa na marafiki kwa kujifungua kichanga hicho Nje ya Ndoa na kukuamua kufanya umuamuzi huo.
‘’Juzi tarehe 18 mwezi huu nilipokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwa walimuona mama huyo akiwa na ujauzito lakini mwisho wa siku wanamkuta hana tena ujauzito na wala hana mtoto,” alisema.
Aidha alisema mama huyo hakupaswa kufanya kitendo hicho ilikuwa kama aliona hali sio mzuri angalikwenda kuripoti ofsini kwake kuangalia namna ya kumsaidia lakini hakufanya jambo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospital ya Micheweni Daudi Rashid Mkasha, alisema walipofika eneo la tukio walikona eneo lililochimbwa na kufukiwa, wakafukua na kukuta mwili wa mtoto ukiwa tayari umeshaharibika.
‘’Tulifika kwenye tukio hilo tukaona kwenye jiko lake kafukia kisha juu kaweka kuni tukafukua tukakuta mtoto kashaharibika tukaona mifupa hali hiyo imetuhuzunisha sana kuona kichanga kimepoteza maisha’’alisema.
Suleiman Shaame Hamad, ni Sheha wa Sizini alikiri kutokea kwa tukio hilo na kushangazwa kitendo cha mama huyo kuchukua hatua ya kukifukia kichanga kisichokuwa na hatia.
Inasemekana baada ya mama huyo kugundua kuwa wananchi wameshapata taarifa za tukio alilolitenda alitaka kujinyonga lakini Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumtia mbaroni.
Comments
Post a Comment