Polisi waahidi kuweka ulinzi kwa wagombea wanawake
Na Fatma Hamad, Pemba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba limesema, litahakikisha linaimarisha ulinzi kwa wagombea wanawake dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, ikiwemo kupigwa, kutukanwa na kunyanyaswa katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi Cyprian Mushi amesema, wapo baadhi ya wanawake ambao wana nia ya kuingia majimboni kugombea uongozi ingawa, wamekua na hofu ya kufanyiwa kwa vitendo vya udhalilishaji.
Amesema, suala la kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, hivyo ni wakati wa akinamama kuhakikisha wanaingia kwa wingi kwenye chaguzi, ili wawe wengi kwenye vyombo vya maamuzi.
‘’Suala la uongozi si kwa mwanamme pekee bali hata mwanamke, hivyo msiogope kuingia majimboni, kwa sababu ni haki yenu kikatiba, msiwaachie wanaume pekee,’’ameeleza.
Amesema kuwa, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 watahakikisha wanaimarisha ulinzi mkali hasa kwa wagombea wanawake, ili kuona wanamaliza uchaguzi katika hali ya amani na usalama bila ya kupatwa na madhara yoyote.
Aidha, amewasisitiza wanawake ambao wataingia kwenye mchakato wa uchaguzi, kuhakikisha waimarisha suala la amani na utulivu wakati wote wa kampeni, wakati wa uchaguzi na hata utakapomalizika.
Kwa upande wake Tumu Mwalimu aliegombea ubunge kupitia Chama cha Mainduzi (CCM) Jimbo la Wingwi amesema, wanawake wengi ambao wanania ya kuingia katika chaguzi hasa wa vijijini, wamekua wakirudi nyuma, kutokana na kuwa na hofu ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Amesema, ni ukweli uliowazi kwamba baadhi ya wagombea wanawake wamekuwa wakidhalilishwa kwa kutukanwa, kuitwa majina mabaya, kupigwa n ahata udhlilishaji wa kingono, jambo ambalo limesababisha wengi kukata tamaa.
Nae mgombea Maryam Saleh Juma aliegombea Ubunge jimbo la Ole mwaka 2020, kupitia chama cha Ukombozi wa Uma amesema, endapo wagombea wanawake watawekewa ulinzi madhubuti, kutasaidia kuwatoa hofu na kua na imani ya maisha yao wakati wote wa Uchaguzi.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Rashid Khalid Mkoa wa Micheweni kichama, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuandaa mkakati huo wa kuwahakikishia wagombea wanawake usalama wao kwani kutatoa fursa zaidi kwa wanawake wengi kuingia majimboni kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar, Dk. Mzuri Ali Issa amesema, hofu ya usalama ni jambo linalozuia wanawake wengi kushiriki siasa.
“Wanawake hukumbwa na vitisho vya moja kwa moja vinavyohatarisha maisha yao na ya familia zao, hili huwatisha hata wale walio tayari kugombea,” amesema.
Ameeleza, kutokana na wanawake na makundi maalumu kuwa na wasi wasi na vurugu za uchaguzi, Dk. Mzuri alipendekeza kifungu kipya kinachozungumzia ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi ambacho kinaitaka Tume ya Uchaguzi kuwa na Polisi mahususi kwa ajili ya uchaguzi na kuwapangia majukumu kwa namna ambavyo itafaa.
Mshauri Elekezi na Mchambuzi Masuala ya Utawala Bora na Mtetezi wa Demokrasia, Almas Suleiman amesema, ili nchi iwe na demokrasia lazima isimamie yale ambayo wananchi wake wanayataka kwa mustakbali mzuri.
Moja ya jukumu la Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024 ni kuandaa na kusimamia Kanuni za Maadili ya Uchaguzi.
Comments
Post a Comment