JAMII YATAKIWA KUWACHA TABIA YA KUWAFICHA WADHALILISHAJI

 


                            NA FATMA HAMAD,PEMBA

Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya ameitaka Jamii kuwa mstari wa mbele kutoa mashirikiano kwa  vyombo vya Sheria wakati kunapotokea vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia Vijijini mwao.

Mkuu huyo ameyasema hayo wakati akifungua kongamano maalumu la kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na watoto, ambalo limeandaliwa na Jumuiya ya Sauti ya Vijana [Youth  Voice Oganization] lililofanyika Tumbe Mashariki wilaya ya Micheweni Pemba.

Amesema suala la udhalilishaji bado ni tatizo ambalo linaendelea kuiathiri Jamii, hivyo ni wakati kwa jamii kuacha muhali na kuvunja ukimwa kusimama kidete kutoa ushahidi ili kuona wahalifu wanaotenda makosa hayo wanatiwa hatiani jambo ambalo litaondosha vitendo hivyo viovu ndani ya jamii.

‘’Nashangaa sana eti unamuonea huruma mdhalilishaji kisa ni mtoto wa kaka yako, Dada yako, Mjomba wako, mbona yeye hakuona aibu kukudhalilishia mtoto wako,alisema.

Alisema katika wilaya ya Micheweni wamekua wakijitahidi kupambana na udhalilishaji ili kuona unaondoka, lakini bila ya kuwepo na  mashirikiano ya pamoja kati yao na jamii sio rahisi kufanikiwa, bali mutaendelea kuwatupia lawama Polisi na mahakama kila siku kwamba hawatendi haki.

Hata hivyo aliwataka wazazi na walezi kuwa karibu pamoja na kufuatilia nyendo za watoto wao ili, waweze kuwalinda na vitendo hivyo.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sauti ya Vijana Pemba Said Mussa Rashid alisema licha ya Elimu inayotolewa kisa siku kwa jamii juu ya madhara ya udhalilishaji, lakini bado jamii imegubikwa na jinamizi la Ruswa muhali, jambo ambalo linapelekea kesi nyingi za udhalilishaji kushindwa kupata hatia.

‘’Sababu kubwa inayokwamisha kesi za udhalilishaji zisiendelee ni rushwa muhali inayotawala katika jamiizetu, alieleza.

Aidha alieleza kuwa ni vyema jamii kubadilika na kila mmoja kuumwa na mtoto wa mwenzake  jambo ambalo  litasaidia kuwalinda na vitendo vya ubakaji.

 Nae Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Haji Abasi alisema wapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwafanya watoto wao kama ni vitega uchumi hali ambayo inapelekea udhalilishaji zaid kwa muathirika.

‘’Mtoto  ameshabakwa wazazi  mnadai pesa na kumnunulia kitu cha thamani, kufanya hivyo tunazidi kuwadhalilisha watoto wetu tuacheni hilo jamani, alisema.

Hivyo alitaka Jamii kuripoti katika vyombo vya Sheria vitendo vya udhalilishaji na sio kuzimalizia kifamilia.

 Katika madhimisho hayo kauli mbiyu ya mwaka huu inasema Wekeza kuzuia ukatili dhidi ya Wanawake na watoto.

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO