SERIKALI ITAENDELEA KUJENGA HOSPITALI, KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA

                                              NA ZUHURA JUMA, PEMBA

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kujenga hospitali na vituo vya afya vyenye vifaa vya kisasa ili kuwapatia huduma bora za afya wananchi wake.

 Akizungumza wakati akifungua hospitali ya Wilaya iliyopo Kinyasini Wilaya ya Wete, Dk. Mwinyi alisema tayari zimeshajengwa hospitali  za Wilaya kwa unguja na Pemba huku Serikali ikiendelea kujenga hospitali za mikoa, rufaa na mwanzo (dispensaries na vituo vya afya) ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila ya usumbufu.

 Alisema kuwa, ujenzi wa hospitali hizo na vituo vya afya vitawapunguzia wananchi kwenda masafa marefu kuifuata huduma hiyo, sambamba ya kupata huduma bora kutokana na vifaa vya kisasa vilivyowekwa.

 "Tutahakikisha tunasogeza huduma bora za afya kwa wananchi, ili wawe na afya njema na sehemu ambazo bado hatujajenga basi wananchi wawe na imani kwani Serikali itawajengea ambapo kuna mradi wa shilingi bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali na vituo vya afya," alieleza Dk. Mwinyi.

 Aidha Dk. Mwinyi aliitaka Wizara waongeze wafanyakazi pale ambapo kunahitajika, kuwalipa watoa huduma na kuhakikisha maslahi yao yatapatikana kwa wakati ili wafanye kazi ya kutoa huduma kwa bidii.

 "Majengo bila huduma sio kitu, hivyo endeleeni kutoa huduma bora kwani vifaa vya kisasa vipo kwa hiyo hakuna sababu ya kutokutoa huduma bora kwa sababu maslahi yenu tunayazingatia ," alieleza Rais huyo.

 Dk. Mwinyi aliwataka madaktari kufanya kazi kwa bidii na kujifunza mbinu mpya kutoka kwa wataalamu wanaofika katika hospitali hizo, ili wawe na uwezo mzuri wa kutoa huduma.

 Pia aliwataka kuwa na moyo wa kujitolea katika kufanya kazi zao huku wakiacha ukali na lugha chafu wakati wa kuwahudumia wagonjwa kwani lugha chafu ni sababu ya kumuongezea mgonjwa maradhi.

 "Majengo haya muyasimamie na kutunza vifaa vilivyomo ili vitumike kwa muda mrefu na wananchi wapate kunufaika," alisema.


Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazuri alisema kuwa, zaidi ya shilingi bilioni 7 zilitumika kwa ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na vifaa, ambapo ina uwezo wa kulazwa wagonjwa 100 kwa wakati mmoja.

 "Miaka mitatu ya Dk. Mwinyi amefanya makubwa kwenye sekta ya afya, hivyo ni vyema tukazithamini juhudi hizi kwa kuendelea kuchapa kazi ili lengo la kutoa huduma bora za afya zifikiwe ipasavyo," alieleza.


 Nae Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema, kwa sasa huduma za afya zimeimarika katika Mkoa wake na wananchi wanapata matibabu bora.

 "Tunamshukuru Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwaletea huduma bora za afya, anahitaji kupewa pongezi kutokana na mambo anayoyafanya," alifahamisha.


Mwananchi Aisha Ali Massoud na Hassan Salim Bakar waliishikuru Serikali kuwajengea hospitali hiyo kwani wamepunguza masafa sambamba na kuimarisha uchumi wa vijiji vyao.

Walisema kuwa, wanatarajia kupata huduma mbali mbali za vipimo bila ya usumbufu wowote na kueleza kuwa wataendeleza ushirikiano kama ambavyo walishirikiana na wajenzi wa hospitali hiyo.

 

              

 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.