UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.


NA FATMA HAMAD, PEMBA

……………..SIRI ya mtungi aijuaye kata………

Wahenga wametupa usia usemao ……Hasira hasara. Wakati mwengine hio hasira sio tu huathiri aliyefanya na aliyefanyiwa, bali watu wa karibu, mbali na hata jamii kwa ujumla.

Hili linaonekana sana pale ndoa inapovunjika baada ya wana ndoa kuamua lipasuke tugawane mbao, lakini misumari ya hizo mbao huwachoma na kuwaumiza wengi, wakiwemo wana familia na hasa watoto.

Mara nyingi pale wazazi wakiwa wametengana baada ya ndoa kuvunjika watoto hukosa huduma muhimu za maisha na kuathirika kimwili na kiakili na kiza hutanda katika safari yao ya maisha.

Mwana harakati maarufu wa kulinda na kutetea haki za watoto kisiwani Pemba, Tatu Abdala Mselem, amekuwa mara kwa mara akiiomba jamii kuvunjika kwa ndoa isiwe sababu ya kila mzazi kufumbia macho wajibu wake wa malezi ya watoto.

Hii ni kwa sababu mtoto  anapokosa huduma za lazima sio tu huwa mnyonge na kujiona kama yatima aliyekosa msaada, bali huwa hana furaha anapocheza, na akili yake huwa haifuatilii vizuri masomo.

 ‘’Kama ndoa imevunjika, kwa nini watoto waingizwe katika shida wakati wao sio walioingia kwenye mkataba wa ndoa, wala kupelekea wazazi watenngane?,’’anauliza.

Shehk Said Ahmad wa Chake chake aliwataka wanaume waseme na nafsi zao, watulize akili zao na inapobidi ndoa kuparaganyika basi waelewe bado wanayo dhima kubwa ya kuhakikisha watoto wanapata huduma zote muhimu na hawateseki.

’Ndoa ikifikia mwisho wake kwa kuvunjika  sio kuvunjika kwa wajibu wa kulea na kuhudumia watoto. Kwa mke huduma zinapaswa kuendelea mpaka inapomalizika eda, lakini kwa watoto lazima ziendelee kwa ukamilifu’’, aliongeza.

Rashid Said Nassor, Afisa Hifadhi ya Watoto katika Wilaya ya Chake chake anashangaa  iweje inapovunjika ndoa wathirika wakubwa wawe watoto wakati wao hawakuhusika na kutengana kwa hao wana ndoa?

WATOTO WANASEMAJEE.

Mwanafunzi mmoja wa darasa la kwanza wa Skuli ya Kangagani nilimkuta akiwa kwao nyumbani kwa takriban wiki mbili akiwa amepiga  kambi kwenye eneyo la uvunjaji  wa kokoto, badala ya kufanya kazi ambayo ndio ya mtoto. Nayo ni ya kusoma na kucheza.

Akinieleza kilichomsibu  alisema alilazimika kufanya kazi hio ya sulubu ili ajipatie mahitaji ya shuleni  na nyumbani kwao baada ya baba yao kutowajali kimaisha, kwa lugha ya siku hizi kuwatelekeza.

‘’Kwa sasa nabanja kokoto ili kujipatia vifaa vya skuli, kama viatu na sare, kwani mama yangu hapatiwi huduma na baba’’, alisema.

Mtoto huyu alisema ilikuwa ni mwaka  wa  saba  hajaitia machoni sura ya baba yake na amekuwa akisikia tu habari zake kutoka kwa mama yake, lakin hamjui huyo baba yake.

‘’Nasikia baba yangu anaishi Unguja, lakini sijawahi kumuona wala kupata  huduma yake yoyote.

Kwa hivyo ikifika karibu na kipindi cha Sikukuu huenda kubanja kokoto kwa ajili ya kujinunulia nguo,’’alileza.

Tabaan mtoto anayeishi katika mazingira kama haya huhisi unyonge na kuathirika kisaikolojia pale anapoona watoto wenzake wapo na baba zao au wanapewa pesa au kitu na huyo baba.

 Pamoja na changamoto hizo zenye maumivu makali huyu mtoto amesema lengo lake ni kusoma kwa bidii ili kuwa daktari wa binadamu na kuisaidia jamii yake.

Mtoto Juma mwenye umri wa miaka [15] mkaazi wa Mjini Wingwi (hilo sio  jina lake halisi) anaefanya kazi ya uvuvi wa samaki, amesema baba yao amewatelekeza takriban kwa miaka minane na   hawaulizi cha asubuhi wala cha jioni, cha kheri wala cha shari.

‘’Nimejingiza kwenye shughuli hizi za uvuvi ili nipate pesa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwetu na mimi binafsi,’’ameeleza.

Ali Khamis Kombo mwenye umri wa [15] mkazi wa kijiji cha Mijini Kiuyu aliacha kusoma na kufanya shughuli ndogo ndogo za kibiashara, kwa ajili ya kumsaidia mama yake.

 ‘’Nyumbani tuko watoto 9 na mama hana kazi yoyote. Hivyo nafanya kazi ili niendeshe familia yangu baada ya baba kutupa kisogo cha kutuhudumia,’’ameeleza.




WAZAZI WANASEMAJE.

Asha Ali, mkaazi wa Mjini Kiuyu, mwenye watoto tisa anasema  huduma zote anajitegemea, ingawa bado yuko kwenye ndoa ya mume alieongeza mke wa pili.

 ‘’Sio kama naona raha mwanangu kufanya biashara, lakini nitafanyaje. Sina budi ila kumtaka anisaidie kimaisha,’’anasema.

Bi kombo Khamis mkaazi wa mjini Wingwi anaeleza kuwa mume wake aliondoka kwenda uvuvini [dago ] Dar es Saalam karibu miaka minane iliopita na hurudi wkati wa  mwezi mtukufu wa Ramadhani tu.

 ‘’Ameniachia watoto  nane [8] na huenda pwani na  watoto wangu   kupanda mwani  ili tupate pesa za kujinunulia mahitaji mana baba yao amenitelekeza,’’anafahamisha.


Mratibu wa wanawake na watoto  wa Shehia ya Kangagani, Awena Salim Kombo, amesema wanawake wengi walioachiwa mzigo wa ulezi peke yao, huwauzisha biashara watoto wao ili wapate chakula.

‘’Ukimuuliza mama kwa nini hawa watoto hawaendi skuli na badala yake anawapa biahara kuuza  anakwambia afanye nini na hana uwezo wa kuwahudumia,’’anaeleza.

SHERIA  ZA AJIRA KWA WATOTO

 Sheria ya ajira na mahusiano kazini namba 8 ya mwaka 2006 inakataza mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 14 kuajiriwa na kukataza ajira kwa watoto wa chini ya miaka 18 katika maeneo ya migodi, viwanda, ubaharia katika meli au kazi nyingine yeyote inayotambulika kuwa hatarishi.

Hata hivyo, sheria inaruhusu ajira kwa watoto wa miaka 14 katika kazi nyepesi ambazo sio hatarishi kwa afya yake, lakini haiathiri mahudhurio ya watoto  masomoni.

WANAHARAKATI WANASEMAJE

Semeni Ali Khamis, mwanaharakati kutoka Jumuiya ya Wanawake  katika wilaya ya Micheweni ameleza kuwa watoto wengi wanaojiajiri ni wale ambao kuwa hawapati matunzo kutoka kwa wazazi wao.

 ‘’Katika kijiji changu cha Konde baadhi ya wanaume hujiingiza kwenye masuala ya ulevi tu, hawana habari ya kushughulikia familia zao,’’analeza.


Fathiya Mussa Said Mratibu wa Chama cha Wandishi wa habari wanawake Tanzania [TAMWA] ofisi ya Pemba amesema anapoachwa mwanamke anaachwa na watoto wote, hivyo shida na dhiki  zinawakumba zaidi watoto.

 ‘’Utawakuta watoto muda wa kuwepo masomoni wamebebeshwa mabakuli ya Mchicha, Kombe, na hata  Chaza na kutembeza mitaani, jambo ambalo linasababisha kufanyiwa udhalilishaji,’’ anasema.


OFISI YA MUFTI.

Afisa kutoka Ofisi ya Mufti iliopo Pemba, Abdalla Muhamed Abdala ,anasema utelekezaji wa wanawake unachangia kwa kiasi kikubwa watoto kujiingiza katika ajira.

Kwa bahati mbaya siku hizi kumekuwa na ongezeko la talaka ambapo kwa kipindi  cha Juni  hadi Agosti 2023,  kupitia ofisi ya Mufti wamelazimika kutoa talaka 18 na kupokea malalamiko 9 ya utelekezaji wa familia.

Alisisitiza ni vyema watoto wakapatiwa huduma muhimu na malezi ya familia ili wakuwe vizuri kwa faida ya taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania,  Patrobas Katambi, amesema  serikali haitavumilia kuona watoto wanakosa haki zao za msingi .

‘’Ni kosa kuajiri watoto kinyume na sheria inavyosema na adhabu inatolewa chini ya kifungu cha 102 (2) ambacho kinampa Hakimu wa wilaya na mkazi kutoa adhabu sawa na faini isiyozidi shilingi milioni 5 au kifungo cha mwaka mmoja au vyote,’’ anafafanua.

Kwa mujibu wa takwimu  kuna watoto milioni 152 wanatumikishwa duniani hivi sasa na kati yao 25,803 ( asilimia 5.6) wapo katika ajira  Zanzibar. Watoto hawa wa umri wa kati ya miaka mitano hadi 17 wameajiriwa au wamejiajiri. 

Hali hii imebainishwa katika taarifa ya Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ajira za watoto mjini Zanzibar. Siku hii huadhimishwa rasmi kila ifikapo Juni 12 ya kila mwaka.



TAKWIMU KUTOKA KITENGO CHA HIFADHI YA MTOTO.

Kwa mujibu wa takwimu za kitengo cha hifadhi ya mtoto Pemba katika wilaya ya Micheweni kwa mwaka 2022, malalamiko yalioripotiwa ya utelekezwaji wa wanawake ni 71, ambapo yamehusisha watoto 185, wanawake 92 na wanaume  93.

Kuanzia mwezi  Januari hadi Agosti mwaka huu malalamiko yaliyopokelwa ni 28,watoto walioripotiwa kutelekezwa ni 84 ( wanaume ni  49 na wanawake 35).

Shirika la Kazi Duniani [ILO] linakadiria kuwepo watoto  152 milioni  katika ajira duniani na kati yao  73  milioni wamo  katika kazi ambazo ni hatari.

Karibu asilimia 70 ya ajira  hizi za watoto ni katika  kilimo na sababu kubwa ni kutokana na umasikini na ugumu wa wazazi kupata ajira zenye hadhi.

Sheria ya Elimu Zanzibar ya  1982, kifungu cha 20, cha sharia hiyo kinamtaka kila mzazi kuhakikisha anampatia mtoto wake elimu ya lazima pale anapofikia umri wa miaka  saba..

 Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza wazi katika kifungu cha 15[1] kuwa kila mtu ana stahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafasi yake; maisha yake binafsi naya nyumbani kwake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake.

Pia kifungu cha 12[1] watu wote wapo sawa mbele ya sharia, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.

MKATABA WA AFRIKA.

Kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto [1999], kipengele cha 15, kinaeleza mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya kazi au ajira zitakazoathiri afya, elimu na maendeleo yake.

Serikali inatakiwa kuweka sheria za kima cha chini cha mshahara, muda wa  kufanya kazi, mazingira ya kazi na adhabu kwa wasio tekeleza haki hii.

Pia inawajibu wa kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za kazi au ajira mbaya kwa watoto.

MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto [1989] kipengele cha 32, kinaeleza mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya kazi au ajira zitakazoathiri afya au elimu yake.







 


Comments

Popular posts from this blog

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.