VIKUNDI VYA USHIRIKA VYAOMBA KUUNGWA MKONO

 




                        NA FATMA HAMAD PEMBA

Wanakikundi cha Mapambano Co-Oparative  kinachojishuhulisha na ufugaji wa Samaki, Kaa na Kamba kilichopo Sizini wilaya ya Michewemi mkoa wa Kaskazini Pemba wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, pamoja na asasi nyengine kuviangalia na kuviunga mkono vikundi vya ushirika, ili viweze kwenda samba mba na Sera ya Serikali   ya Uchumi wa Buluu.

Wakizungumza  na  mwandishi wa habari hizi  huko kwenye Kikundi  chao  Sizini Wilaya ya Micheweni walisema sera ya Serikali ya Uchumi wa Buluu ni kuhakikisha   wanaviinuwa  vikundi vya ushirika  ili viweze kutoa tija na kuondokana na umasikini.

Alisema  wamekuwa wakipata faida kubwa  kwani tayari wameshapata  pesa za kuendeshea  maisha  yao kupitia mavuno  waliovuna msimu uliopita.

‘’ Tumeamua kufuga, Kamba na Samaki  jambo ambalo litatuwezesha kujingizia kipato, hivyo twaiomba Serikali ituunge mkono kihali na mali ili kutimiza malengo ya Serikali juu ya uchumi wa buluu,’’ walieleza wanakikundi.

Mapema Naibu katibu wa kikundi hicho  Thamrat Suleiman Said aliwataka wanakikundi wenzake  wasikatishwe tamaa na maneno ya watu bali waendelee kupambana  wakiendeleze kikundi chao.

“ Sisi kama vijana wa kike ni lazima tujiamini, tupambane  ili tuweze kukiendeleza kikundi chetu jambo ambalo litatusaidia kupata kipato cha halali, “ alifahamisha.

Akitoa nasaha kwa wanakikundi hao Meneja wa mipango  ya Bahari na Pwani  kutoka  Shirika la International Union for Conservation of Nature  ( IUCN )  Elinasi Monga, alisema ni vyema kwa wanakikundi hao kuendeleza  mradi wao huo  wa ufugaji wa Samaki na Kamba  kwani sasa hivi Duniani kote wamelekeza nguvu zao kwenye bahari.

“ Mukiitumia bahari vizuri mtaweza kuondokana na Umasikini, mtakuza uchumi wa nchi pamoja na kuondokana na mabadiliko ya tabia ya nchi’’, alifahamisha  Meneja.

Alisema endapo watajipanga  na kuachana na migogoro wataweza kujipatia kipato ambacho kitaweza  kuendesha maisha yao sambamba na kujipatia ajira.

Nae Ofisa mdhamini wizara ya Uchumi wa Buluu Dk, Salim Moh’d Hamza aliwataka kuendeleza   ushirika wao  kwani kutawawezesha kupata fursa mbali mbali  za kimaendeleo zilizopo Nchini kupitia sekta ya Uvuvi.

“Serikali ya Zanzibar  inalengo la kuekeza zaidi kwenye sekta ya bahari, hivyo ni vyema mjitoe ili kuendana na soko la dunia,’’ alisema Ofisa mdhamini.

Alisema wizara itaendelea  kuwasaidia wanakikundi wanaojishuhulisha na masuala ya baharini ili waweze kuenda na Sera ya Serikali ya Uchumi wa buluu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho Khalfan Hamad Khalfan alisema kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2013, kilianza na wanachama 10 wanawake 5 na wanaume 5, na sasa kinawanachama 17 wanaume 8, wanawake 9 tayari walishawahi kuvuna mara tatu.

Hata hivyo alieleza  kwa msimu huu wameingiza vifaranga vya Kaa kilo 150, wenye thamani ya shilingi Laki tisa (900,000) Samaki vifaranga Elfu kumi na moja mia tano na nne (11,504) wenye thamani  shilingi milioni Nne Elfu ishirini na Sita na mia nne (4,026,400) na Kamba ndoo mia tisa wenye thamani ya  shilling Milioni Saba (7,000,000).



                                        

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.