MAGUMU ANAYOYAPITIA MWALIMU WA MADRSA MWENYE ULEMAVU WA VIUNGO PEMBA HAYA HAPA.


Saada Khamis: Mwalimu wa madrassa mwenye ulemeavu

Awapatia watoto elimu kwenye mazingira magumu

NA FATMA HAMAD, PEMBA

‘’KIPINDI cha mvua  wanafunzi hulazimika niwafungie  wasije madrasani mpaka  zitakapo malizika,’’ hayo ni maneno ya Sada  Khamis  Hamad  mwenye ulemavuwaviungo  ni  mwalimu wa madrssa.

Kwake anasema ulemavu alionao  haukua mzigo kuwa  asitimize ndota zake za kuwa mwalimu wa madrassa.

Hii ni baada ya kuukosa uwalimu wa skuli kutokana na changamoto za hapa na pale, ingawa hakukata tamaa.

‘’Nilikuwa natamani siku moja niwe darasani nafundisha   ila sikubahatika, kusoma skuli hata darasa moja, kwani ilikuwa iko maeneo ya mbali na siwezi kutembea,’’anakumbuka.

 Ukosefu wa kiti mwendo kwa wakati huo, na hasa kutokana na ukata wa fedha waliokuwa nao wazazi wake, ulimkosesha elimu ya skuli.

Yote hayo ni masikitiko ya Mwalimu wa Madrasa ya Qur-aan  Sada Khamis Hamad mwenye ulemavu wa viungo anaeishi katika kijiji cha Shumba Vyamboni Wilaya ya Micheweni Pemba.

Maalim Sada Khamis Hamad ambae ni mtoto wa sita  katika familia yao ana umri wa miaka 28,  anasema suala la kukata tamaa na yeye lilikuwa mbali mno.

Bada ya miaka kadhaa, alishindwa hakuweza tena kwenda madrasa kutokana na hali yake na kwa vile hana usaidizi wa kigari ambacho chengemuwezesha kumsaidia.

Baada  ya  kuona  anakosa  kusoma,  ndipo  akamua  anzishe  madrasa  yake  mwenyewe  baada ya kuhitimu kusoma Qur-aan  ili  aweze  kuiendeleza  elimu yake.

 ‘’Nilisema  ijapo kuwa  sikuweza  tena kwenda  kusoma, lakini   isiwe  sababu  ya  kukaa  tu nyumbani, ndipo  nikamua  nianzishe  madrasa  yangu, ili kuwafundisha watoto,’’anaeleza.

Huu ni mwaka wa nne tangu kuanzisha madrasa  hiyo, ambapo alianza  na  wanafunzi  wanne (4)  wawili wa kike na  wawili  wanaume  na  sasa  ana  wanafunzi 52.

ANA CHANGAMOTO GANI?

 Moja anayoiona na kumkosesha usingizi ni ukosefu wa  sehemu  salama  ya  kusomeshea wanafunzi kutokana na mazingira yake.

 Kwake mazingira hayo, hayako rafiki,  kwani  kwa sasa anatumia kibaraza cha  nyumba  yao kuwafundishia  wanafunzi  wake.

‘’Nasumbuka  sana  hususan kipindi  cha  mvua barazani panakuwa  hapasomeki  inabidi  wanafunzi  wasije  madarasa mpaka  mvua  zikate,’’ anasema.

Wanafunzi wamekuwa wakikimbia na kwenda madrssa nyengine kwa vile kuna  sehemu  salama  za kufundishia.

Akasema ni wakati kwa wale wanaouguswa na haki ya watoto juu ya elimu, kuona wanamtembelea na kumpiga tafu, ili kumjengea madrassa ya kisasa.

‘’Si vyema nguvu zote zikaelekezwa kwenye ujenzi wa miskiti pekee, bali msingi wa dini ya kiislamu, ni uwepo wa madrassa za kisasa na sio kusomea barazani,’’anafafanua.

WANAFUNZI WAKE

 Asha Khamis na Ali Juma wanafunzi wanaosoma  katika  madrsa hiyo, wanasema hawaridhishwi  na  kitendo cha kusoma  barazani.

‘’Kwakweli  hatupendi kusoma mazingira haya, kwani  pakiwa na jua hapakaliki, na kukiwa na mvua tunafungiwa kabisa,’’wanasema.

 Wanasema kama kweli kuna nia ya kweli kwa wadau wa haki za watu wenye ulemavu na watoto kusaka elimu, hakuna budi kujenga madrassa ya kisasa.


MAMA MZAZI

Hadia Salim Ameir, anasema  mungu  amemjaalia  kuzaa  watoto  wanne  wote  wenye  ulemavu  wa viungo  ambapo  mmoja  alifariki.

Anasema mwanzo akiwazaa wanakua ni wazima  wanatembea wenyewe, lakini  kila  wakiwa wakubwa  ndio wanapata ulemavu.

 ‘’Nilikua nawazaa ni wazima lakini mwisho wake wanakua walemavu, na sikuwapeleka Hospital nikajua ni sababu gani ilopelekea  hivyo’’,anasema mama huyo.

 

Aidha alieleza kuwa anaishi katika mazingira magumu  yeye na watoto wake  kwani  hata nyumba yao wanayoishi imeshakua mbovu na haina hata  huduma rafiki  za  vyoo  kwa  ajili  yao.

 “Baba yao ameshafariki  huduma  zote   wananitegemea   mimi na sina msaidizi, sina  hata  kazi ya uhakika ya kufanya  maisha  yangu  ni  magumu  nahitaji  msaada”, alieleza.

Kwa bahati mbaya wako viongozi wa majimbo kama vile Mbunge au Mwakilishi hajawahi kupita katika familia yetu ili kuangalia changamoto zilizopo kwenye familia hii.

Mratibu  wa Baraza  la  Taifa  la  Watu wenye  ulemavu  Pemba  Mashavu   Juma  Mabrouk, anasema  wamekua  wakiwasaidia  watu  wenye  ulemavu, ambao  wanajishuhulisha  na  harakati  mbali mbali.

 Anasema  wamekua  wakifurahika  wanapoona  watu  wenye ulemavu   wakijishuhulisha   na  shughuli  mbali  mbali, hivyo  amewataka  wahisani  na  wasamaria  wema  kuelekeza   macho yao kwao.

 Hata hivyo amewashauri wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika madrassa hiyo, kuonesha mfano kwa  kuanza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa madrassa ya kisasa.

” Sisi Baraza hatuna mfuko maalumu wa kumsaidia mtu mmoja moja kama huyo, kwani anayoyafanya ni mambo ya kijamii ispokuwa tunawaomba wanajamii kuchangia, ili aweze kujenga madrassa”, alishauri.

UONGOZI WA SHEHIA

Sheha wa shehiya  ya Shumba vyamboni Time  Said   Omar, ameleza kuwa  mwalimu  huyo anapata shida kwani  anasomeshea  wanafunzi wake  katika baraza  ya  nyumba  yao  na  wakati  mwengine  hukaa kwenye  Muembe.

Amesema  ameshachukua  jitihada  mbali  mbali  kuhakikisha  anapatiwa msaada  wa kujengewa madrassa  japo  chumba kimoja,  lakini  bado  hajafanikiwa.

‘’Nimeshawapeleka viongozi wengi ili waweze kumsaidia lakini bado hatujafanikiwa na   hivi saivi nimejipanga niende   kwenye jumuia ya Milele Foundation ili waweze kumsaidia’’, alieleza sheha .

Licha ya ulemavu wake lakini mungu amemjalia kipaji cha elimu  ameshafika  Dar-es-salamu  kushiriki mashindano ya qur ana, hivyo anahitaji  kuungwa mkono   kwa hali na mali  ili aweze kuendeleza  kipaji chake hicho.

 

UONGOZI WA WILAYA

Mkuu  wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, anasema anaelewa changamoto ya mwalimu, huyo ingawa wanaangalia namna ya kumsaidia.

‘’Hakuna fungu maalum kwa ajili ya kumsaidia  mtu  mmoja  mmoja  kwa  ajili  ya  kujengea  nyumba  ama  Madrassa,  lakini kama wakitokezea wahisani tutampekelekea,’’anasema.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MICHEWENI.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Micheweni Hamad Mbwana Shehe amesema kwa kipindi cha mwaka jana waliwapatia vifaa vikiwemo Grenda,Mashine, Plesi   kikundi cha watu wenye ulemavu wa viungo cha Hirimu fasi cha micheweni na kikundi cha watu wenye ulemavu wa uoni [Zanab] kutoka micheweni shilingi Milioni moja kwa ajili ya kwenda kwenye maonyesho.

Ameeleza kuwa kwa mwaka huu  halmashauri haitowi tena pesa kwa vikundi vya wajasiriamali,  kwani Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dk Hussein Mwinyi  wakati akizindua vitambulisho vya Wajasiriamali alielekeza ni vizuri kuwepo na mfuko mmoja  ili  kuwapatia fedha kwa kiwango kinachoridhisha  wanaostahiki kupewa.

 ‘’Nivizuri kuwepo na mfuko mmoja tu  na kusiwe na mifuko mingi mfano Halmashauri, Uwezeshaji Benki ,’’ ameeleza mkurugenzi halmashauri.

 Amesema kuwa  kwa mwaka huu tayari wameshawasilisha zaidi ya shilingi  Milioni ishirini katika mfuko huo  na huko ndiko watakakopatiwa watakaohitaji wakiwemo watu wenye ulemavu.

OFISI YA MUFTI

Msaidizi Katibu ofisi ya Mufti Sheikh Said Ahmad Mohamed, kwa vile ofisi hiyo ndio msimamizi mkuu wa madrasa zote za Qur-an, ameahidi kuonana naye.

‘’Nimevutiwa mno kuona kuna mwanamke tena mwenye ulemavu wa viungo ameanzisha mpango wa kuihuisha dini ya kiislamu, na sisi tutaangalia namna ya kumasaidia,’’anasema.

KATIBA YA ZANZIBAR YA MWAKA 1984

Kifungu cha 10 (g) kinafafanua ‘kwamba serikali itawekea mazingira rafiki kwa makundi ya wagonjwa, waliojiajiri, wazee, watoto na watu wenye ulemavu’.

Lakini hata kifungu cha 12 (1) kimefafanua kuwa, ‘watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria’.’

SHERIA YA WATU WENYE ULEMAVU NO 9/2006

Kifungu cha 9, kinaelezea haki ya kupata elimu kwa watu wote wenye ulemavu na mafunzo mengine kama ilivyo kwa raia wengine. 







8




 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.