JINSI MICHEWENI ILIVYOWAOKOA WATOTO DHIDI YA AJIRA ZA UTOTONI
Miaka iliyopita, katika baadhi ya vijiji vya Micheweni, ilikuwa kawaida, kumuona mtoto mwenye umri mdogo akiwa shambani, bandarini au sokoni badala ya kuwa darasani.
Wengine walikuwa wakibeba mizigo, kuvua samaki, kuuza bidhaa au kufanya kazi za nyumbani kwa muda mrefu, huku ndoto zao za elimu zikififia taratibu.
Ingawa kupitia ushirikiano kati ya serikali ya wilaya, kamati za skuli, walimu, wazazi, viongozi wa dini pamoja na mashirika ya kutetea haki za watoto, Micheweni inaanza kushuhudia mwanga mpya katika mapambano dhidi ya ajira za watoto.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni Khatib Juma Mjaja, anasema kwa miaka ya sasa Micheweni, inaanza kuandika historia mpya, tofauti na zamani ambapo watoto wengi walionekana mashambani na bandarini, wengi wao wanaonekana wakiwa madarasani wakijenga ndoto zao.
Sheha wa Sizini Suleiman Shaame Hamad anasema mkakati umezaa matunda kwani kuanzia mwaka 2023 hadi 2025 Shehia yake pekee imefanikiwa kuwaokoa watoto 70 katika ajira.
Mkuu wa Divisheni Idara ya Elimu Mbadala na watu wazima Pemba Salim Kuza Sheikhan anasema kwa Pemba pekee waliokolewa watoto 19,421.
Anasema kwa
wilaya ya Mkoani ni 4111 wanawake 2044 wanaume 2067,ambapo wilaya ya Chakechake
3627 wanawake 1718, wanaume ni 1909.
Wete 4074
wanawake 1705 wanaume 2369, huku wilaya ya Micheweni 7,609 wanawake 2,967
wanaume 4,642, ikiwa ndio wilaya ilikua ikiongoza kwa ajira za utotoni.
MVUVI
Omar Khatib
Omar mvuvi kutoka bandari ya Shumbamjini Michewe anasema mkakati
umesaidia kwani kazi ya kubeba Samaki kwenye dau na kupeleka kwenye mnada kwa
sasa zinafanywa na watoto wa miaka 18,19.
‘’Zamani ilikua ukiwakuta zaidi ya watoto 12 wenye
miaka 13,14, wakibeba na kupara Samaki hapa bandarini,’’ingawa saiv hatuwaoni.
WALIMU WA SKULI
Mwalimu wa seksheni ya utawala Skuli ya msingi B Micheweni Abdi Othman Faki anasema walikua wakiandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza takribani kila darasa 70 hata ikifikia mwisho wa mwaka ama darasa la pili utakuta wanafika 40 ama 35 tu.
“Tulikuwa tunaandikisha wanafunzi wengi mwanzoni mwa muhula, lakini baada ya muda baadhi yao wanapotea kabisa, wengine wanakuwa wanapelekwa kufanya kazi.”
Anasema wamepunguza ajira za watoto, kwani wanapita kila sehemu na kuwarudisha skuli wale wote ambao wametoroka na kujishughulisha na shughuli ndogondogo kama kubanja kokoto na kuuza biashara.
Anasema mwaka 2023 wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba skulini hapo ni 161, waliokuwa hawakufanya kwa utoro ni watatu tu, na waliofaulu ni 21 kwani ndio mwaka walioanza mkakati huo.
Mwaka 2024 walikua ni 187, waliokua hawajafanya mtihani ni wanane tu, wanawake watatu, wanaume watano na waliofaulu ni 23.
Ikiwa kwa mwaka 2025, walikua ni 174 waliotoroka ni tisa (9), wanawake wawili (2), wanaume saba (7), waliofaulu ni 19.
Anasema kwa miaka ya nyuma ikichukua takribani wanafunzi kati ya 20 ama 25 hawakufanya mitihani hiyo na kujiingiza kwenye shughuli ndondogo.
Mwalimu mkuu Skuli ya msingi Sizini Suleiman Abdulla Khamis, anasema walikua na wanafunzi 70 waliorudishwa baada ya kutoroka na kujihusisha na ajira.
‘’Kwa kweli tulikua na darasa letu mbadala la walirudi Skuli, na sasa wanaendelea na masomo, wengine wamefaulu darasa la saba na wengine wameshafika darasa la 12,’’anafafanua.
Anasema wanafunzi walioko darasa la saba mwaka huu walianza darasa la kwanza wakiwa 163 na sasa wapo 180 wanawake 92 wanaume 88.
Anasema wanafunzi hao tokea walipoanza darasa la kwanza hakuna hata mmoja ambae ameacha masomo, isipokua wengine wamepata uhamisho wa kwenda skuli nyengine baada ya wazazi wao kuhama.
MKAKATI ULIVYOANZA KUBADILI MICHEWENI
Afisa Elimu wilaya ya Micheweni Asha Rashid Abdulla anasema Baada ya kuona ajira za watoto zimekithiri, serikali ya wilaya, kwa kushirikiana na kamati za skuli ilianza kuweka mkakati maalumu wa kuzuia ajira hizo.
Anasema miongoni mwa mikakati walioichukua ni Kufanya mikutano ya kijamii, kufuatilia watoto wanaokosa masomo, ziara za nyumba kwa nyumba, kushirikisha viongozi wa dini na masheha.
“Tuligundua kuwa bila kushirikisha jamii moja kwa moja, tatizo hili lisingemalizika,”anasema.
Anasema tokea walipoanzisha mkakati huo hali imebadilika Micheweni, ambapo mwaka 2025/2026 imeibuka na ushindi wa kwanza kwa Zanziba katika matokeo ya darasa la saba.
KAMATI ZA SKULI ZINAVYOGEUKA NGOME YA ULINZI
Khamis Khatib mwanakamati skuli ya Sizini anasema Kamati zinatembelea familia zenye watoto wanaofanya kazi na kupewa elimu kuhusu madhara ya ajira za watoto.
“Sasa mzazi akimzuia mtoto kwenda skuli jamii nzima inahoji, kwanini anafanyishwa kazi.”anaeleza.
SASA: WATOTO WANARUDI MADARASANI
Mabadiliko yanaonekana wazi katika baadhi ya skuli za Micheweni, ambapo watoto waliokuwa wameacha masomo, wameanza kurejea darasani.
Mwanafunzi Mohamed Othman Himid (16)wa darasa la saba (sio jina lake halisi) anaishi na shangazi yake anasema, baada ya babayake kufariki hakubahatika kuandikihwa skuli, bali alikua anafanya kazi za kulima na kubanja kokoto.
Anasema alikua anaumia kuona watoto wenzake wanakwenda skuli, kwani nae ndoto yake kubwa ilikua ni kuwa Mwalimu.
“Nilikuwa nafanya kazi badala ya kusoma, lakini sasa nimekuja skuli nasoma na wenzangu na natamani niwe mwalimu.”
Mwanafunzi mwengine Asha Ahmed Mohamed(17) (sio jina lake halisi) mkaazi wa Micheweni aliewahi kufanya kazi ya kupanda mwani anasema sasa anaamua kuja skuli na anatamani siku moja kuwa mwalimu.
‘’Wazazi wangu hawakunipeleka skuli kwa sababu hawana uwezo nikawa nafanya kazi ya kupanda mwani tu’’, anasema.
Anasema kwa vile alikua anahamu ya kusoma, mwaka 2023, ndipo alipochukua hatua ya kwenda skuli kujiandikisha na kuanza masomo.
Rahma Omar Juma (16) (sio jinahalisi) wa Micheweni anasema alikua anajishughulisha na kazi ya kupanda Mwani apate pesa aisaidie familia yake kimaisha.
‘’Wakati nikiendelea na shughuli zangu hizo alikuja mwalimu nyumbani akanishawishi nirudi skuli, nikakubaliana nae nimerudi, sasa napata elimu na wenzangu na ninamatumaini makubwa ya kufaulu mtihani wangu wa darasa la saba,’’anasema.
Omar Assa Ali mwenye umri wa miaka (15) (sio jina halisi) mkaazi wa Tumbe anaefanya kazi ya kupara samaki bandarini, anasea anafanyashughuli hizo wakati akisharudi masomoni.
‘’Siku za jumamosi na Jumapili ama skuli zikifungwa ndio huja bandarini kupara Samaki na tena muda ambao si wakwenda madrasa,’’anafahamisha.
Baadhi ya wazazi wamebadili mtazamo baada ya kuona umuhimu wa elimu kwa maisha ya mtoto.
Mzazi moja ambae hakutaka kujulikana jina lake, mtoto wake alimkatisha masomo na kumtaka aende pwani apate pesa amsaidie mahitaji nyumbani.
Anasema kwa sasa baada ya kupata uwelewa juu ya umuhimu wa elimu licha ya umaskini wake, anaona ni bora amuache aendelee na masomo na wenzake.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la kazi duniani (ILO) Tanzani, juhudi za pamoja kati ya serikali, jamii na mashirika ya watoto zimechangia kupungua kwa ajira za watoto nchini.
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi anasema kwa mujibu wa Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi, unaonesha kuwa utumikishaji wa Watoto umepungua kutoka asilimia 29 mwaka 2014 hadi asilimia 24.9 mwaka 2021.
Anasema serikali imeanzisha mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mpango Kazi wa Taifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA II, 2024/25–2028/29) na Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto.
Patrobas Katambi,akizungumza na waandishi wa habari Juni 12,2025 jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Watoto.
Zanzibar imefanikiwa kuwaokoa watoto 1,630 waliokuwa wakijihusisha na ajira za utotoni au waliokuwa katika hatari ya kuingia kwenye ajira hizo, ikiwemo kuvunja kokoto, kupara samaki na kujihusisha na shughuli za uvuvi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na
Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, anasema kati ya watoto hao, 1,629 wanatoka
Pemba huku mtoto mmoja akitokea Unguja.
Shariff ameyasema
hayo, Juni 11, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
Mwanakwerekwe, kuelekea Maadhimisho ya
Siku ya Kupinga Ajira za Watoto Duniani ambayo hufanyika Juni 12 kila mwaka.
Anasema kati ya
watoto hao, wavulana walikuwa 1,127 na wasichana 502.
CHANZO NIPASHE
Sheria ya Elimu Zanzibar ya mwaka
1982, kifungu cha 20 kinamtaka kila mzazi kuhakikisha anampatia mtoto wake
elimu ya lazima pale anapofikia umri wa miaka saba.
Katiba ya Zanzibar ya 1984 katika kifungu cha 12[1] kinasema, watu
wote wapo sawa mbele ya sharia, na wanayo haki, kupata haki sawa mbele ya
sheria.
Mkataba wa Afrika wa Haki
na Ustawi wa Mtoto [1999], kipengele cha 15, kinaeleza mtoto ana haki ya
kulindwa dhidi ya kazi au ajira zitakazoathiri elimu na maendeleo yake.
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto [1989] kipengele
cha 32, kinaeleza mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya kazi au ajira
zitakazoathiri elimu yake.
NCHINYENGINE ZIPOJE
Uganda: Imefanikiwa kupunguza kiwango cha uajiri wa watoto
kutoka asilimia 22.6 (mwaka 2012) hadi asilimia 19.1 kulingana na takwimu za ILO.
Malawi: Kiwango cha ajira za watoto kinakadiriwa kuwa kati ya asilimia 30 na 38 katika miaka ya hivi karibuni.
China: Imepiga hatua kubwa kihistoria katika kupunguza ajira za watoto na utumikishwaji, huku idadi ikionekana kuwa chini zaidi ya asilimia 3 kama ilivyo katika maeneo mengi ya Asia na Pasifiki.
MWISHO
Comments
Post a Comment