KILIMO MSITU TARAJIO LA KUJIKOMBOA NA UMSKINI

 


NA FATMA HAMAD, PEMBA

MKURUGENZI WA Jumuia ya uhifadhi Mazingira Pemba CFP Mbarouk Mussa Omar  amezitaka kamati zinazosimamia masuala ya uhifadhi wa mazingira kuhakikisha wanaendeleza shughuli hizo ikiwemo kilimo msitu, ili kuona wanajipatia kipato.

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na wanakamati hao ambao ni kutoka shehia za Chwale, Kambini kichokochwe, Kiuyu na Mchangamdogo katika mafunzo ya siku mbili ya kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza shughuli za uhifadhi mazingira,yaliofanyika Ofisi za CFP huko Minyenyeni mkoa wa Kaskazini Pemba.

 Alisema kilimo ndio tegemeo kubwa la Taifa, hivyo ni vyema wanakamati hao kuendelea kulima kilimo msitu, waweze kuzalisha mazao ambayo yatawasaidia kupata chakula pamoja na pesa ambazo  zitaendesha maisha yao.

‘’Ndugu zangu shughuli hizi za kulima kilimo msitu msifanye kwa sababu tu ya mradi, bali ifanyeni  kama ni kazi yenu ya kila siku, kwani mukifanya hivyo mtapata mazao mtakula nyumbani na mengine mtauza mtapata pesa mtasomeshea watoto wenu,’’aliwanasihi.

Aidha alisema endapo watajiendeleza na shughuli hizo wataondokana na utegemezi sambamba kujipatia kipato na sio kukaa na kusubiri ajira serikalini.

Kwa upande wake Afisa kilimo Msitu na usawa wa kijinsia Sada Juma Segeja alisema lengo la mafunzo hayo kwa kamati hizo ni kuwahamasisha suala zima la usawa wa kijinsia katika masuala uhifadhi wa mazingira.

Alisema wanaiwezesha kamati hiyo kutoa elimu kwa jamii kuona mwanamke anamiliki ardhi yake mwenyewe, aweze kulima kilimo msitu apate mazao ambayo yatamuezesha kuendesha maisha yake bila kumtegemea mtu.

‘’Kwa kweli lengo hasa la kuundwa kwa kamati hizi ni kwenda kuibadilisha jamii kuacha fikra potofu na kumpa fursa mwanamke aweze kumiliki adhi ili weze kutunza mazingira kama anavyofanya mwanamme,’’alisema.

Nao baadhi ya wanakamati hao walisema watahakikisha elimu hiyo wanaifikisha katika jamii zao na kuona wanawake wanapata fursa mbalimbali ikiwemo uongozi, kumiliki ardhi sambamba na kutunza mazingira.

MWISHO.



Comments

Popular posts from this blog

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

UROHO WA MALI KWA WANAUME UNAVYONYIMA WANAWAKE ARDHI

‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’