UNYANYAPAA ADUI ASIEONEKANA KWA WAGONJWA WA KIFUA KIKUU

 



NA FATMA HAMAD, PEMBA

 NI kawaida ya binadamu walio wengi wanapoumwa hunasibisha maradhi yao na imani za kishirikina.

 Na aina hii ya watu hawasikii, hawaoni wala hawashauriki kuhusu huduma za hospitali na hatimae kuangukia kwenye waganga wa kienyeji.

 Ingawa baadhi yao huelekeza imani zao kwengine baada ya kuona huduma za hospitali hazikuzaa matunda huku wakiwa wanaripoti kila wanapopangiwa.

 Ugonjwa wa kifua kikuu ni moja ya ugonjwa ambao watu wengi huelekeza imani zao kwengine kutokana na jinsi unavyokuja huku ukiwa dalili za mwanzo kutoonekana.

 ‘’Kila siku unapoenda hospitali ukisema unaumwa na kifua unapewa dawa tu bila kupimwa, hivyo hali ikiendelea kudhoofu mtu anajiona kama tayari ana magonjwa mengine ya kishirikina,’’ alisema mwananchi Faida Hassan mkaazi wa Finya Wilaya ya Wete, Anasema, wakati mwengine kutokufanyiwa vipimo ndipo kunakosababisha watu wengi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wengi.

 Hivyo ugonjwa huo unapokuathiri bila kupata dawa, mwili hudhoofu na kuonekana kama kituko kwa jamii na hatimae kudharauliwa na hata kuitwa kwa majina mabaya.

 Mwandishi wa makala haya katika utafiti wake alibaini kwamba maradhi ya mwili hutibiwa kwa dawa, lakini maradhi ya maneno, dharau huponya kwa heshima na mapenzi.

 Kifua kikuu (TB) bado ni moja ya magonjwa yanayoendelea kuikumba jamii ya Zanzibar ambao unaotibika, ingawa waliowengi wanadhani ni ugonjwa wa kurogwa na  kupona kwake ni shida hasa pale unapokosa kujulikanwa ugonjwa unaougua.

 Ndio maana mtu anapopatwa na tatizo hilo anajisikia dhalili sana huku jamii ikimuona  kama ni mzigo na  baadhi ya watu humtenga.

 Jambo ambalo hupelekea baadhi ya wagonjwa kujificha ni kutokupata matibabu kwa usahihi kwani hichukua muda kugundulika na hivyo ugonjwa unapomuweza hujisikia shida kufika tena hospitali kwa kuhofia kudharaulika na kusababisha ugonjwa huo kuendelea kusambaa.

 MASHUHUDA WA UGONJWA WA TB

 Amina Ali (sio jina lake halisi) anasema  alipogundulika kuwa anaugua  kifua kikuu, alijikuta akikwepwa na marafiki, ndugu na hata jirani zake ambao walikua wanaishi pamoja.

 ‘’Nilijihisi watu wananichukulia kama mzigo, wengine waligeuza nyuso zao njiani nilipokua ninapita,’’ anasimulia dada huyo.

 Anasema alikaa miezi kadhaa nyumbani kwake akiwa haendi pahala popote kutokana na aibu aliyokua nayo.

 Mgonjwa mwengine Ali Said ambae hakutaka jina lake litajwe mkaazi wa Micheweni, anasema alipogundulika ana ugonjwa wa TB na kuanza kutumia dawa alitengwa, hata ndani ya familia yake.

 "Nilitengewa vyombo vyangu kama sahani, bakuli na kikombe na havikuweza kuchanganyishwa na vyombo vyengine vya nyumbani," anaeleza Ali.

 Wahida Seif mkaazi wa Chake Chake ambaye pia (sio jina lake halisi) anasema, alipogundulika tu kuugua TB alihamishiwa chumba alichokuwa akikaa na kuwekwa chumba cha uwani kwa madai ya kwamba ndani wanalala watu wengi, hivyo atawaambukiza.

 Anasema, pamoja na maumivu ya ugonjwa huo pia hali ya upweke ilimzidishia maumivu na kusababisha kuugua mara mbili.


 JAMII

 Khadija Ali Hamad mkaazi wa Sizini  yeye anasema, wagonjwa wa TB bado wanaendelea kunyanyapaliwa, jambo linalopelekea watu kushindwa kufika hospitali kufanyiwa uchunguzi wakati wanapohisi dalili za ugonjwa huo.

 ‘’Na ndio maana ugonjwa wa TB ikawa  unasambaa kwani watu hawajitokezi Hospitali kufanyiwa uchunguzi wakapatiwa tiba mapema wakati wanapogundulika, kutokana na unyanyapaa wanaofanyiwa wanaougua ugonjwa huo,’anasema

 Said Ali Said mkaazi wa Tumbe anasema, endapo Jamii haitoelimishwa madhara ya unyanyapaa, huenda ugonjwa ukaongezeka  kwani wengi watakwepa kwenda hospitali na badala yake kukimbilia kwa waganga wa jadi  na kukosa  tiba sahihi ambayo inaweza  kusababisha kupoteza maisha kabisa.

 WATAALAMU WA AFYA

 Afisa Habari Tehama na Mawasiliano kutoka Kitengo shirikishi Ukimwi, Homa ya Ini, Kifua kikuu na Ukoma Kisiwani Pemba  Khalfan Khamis Khalfan anasema, bado tatizo la  unyapaa kwa wagonjwa wa kifua kikuu  linaelendelea siku hadi siku.

 Anasema, watu waliowengi wanashindwa kujitokeza hospitali kufanyiwa vipimo na kuanza matibabu mapema, kwa kuhofia  kunyanyapaliwa.

 "Ni juzi tu wiki zilizopita tuliripotiwa kesi ya mgonjwa kutengwa na jirani zake ambao wanaishi katika nyumba moja," anasema.

 Anafahamisha kuwa, mgonjwa wa TB anapoanza kutumia dawa kwa muda wa wiki mbili inakua hawezitena kuambukiza, hivyo jamii isiwatenge bali iwashirikishe katika  shughuli zote za kifamilia na kijamii.

 Dokta Rahma Omar Mtaalamu wa Afya Zanzibar anasema, ugonjwa wa kifua kikuu sio laana, bali ni ugonjwa kama ugonjwa mwengine na unatibika.

 ‘’Jamii inauona ugonjwa huu kama ni aibu na kuwafanya wanaougua kukimbia matibabu na kushindwa kufanikisha tiba zao, jambo linalopsababusha kuenea," anasema.

 Kwa mujibu wa wataalamu wanasema, kuchelewa kupimwa, kuacha dawa katikati na msongo wa mawazo ni baadhi ya madhara ya moja kwa moja ya unyanyapaa.



VIONGOZI WA DINI

 Sheikh Said Ahmad Mohamed ambae ni Mratibu wa Ofisi ya Mufti Pemba anasema, maradhi ni mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo  haipendezi kubaguana kwa sababu tu mtu amepatwa na ugonjwa fulani.

 Anasema, hata dini inaeleza kwamba anapoumwa mmoja wao wawe karibu nae zaidi na kumpa moyo wa imani, ili aweze kuwa karibu na mola wake na kupeleka maombi yake, huku akiondokana na dhana potofu za kishirikina.

 Nae Robati Migua Ndalami kiongizi wa dini ya Kikristo anasema, kwa mujibu wa mafundisho ya dini yao haipendezi kumtenga, kumnyayasa mtu kisa ameugua, hakuna anaependa maradhi isipokua ni mipango ya Mungu mwenyewe na kila binadamu ataumwa.  (Jina la 'Robert' liangalie vizuri spelling zake ulivyoliandika, au ndivyo alivyokutumia?)

 WANAHARAKATI

 Khadija Kombo Khamis ni Makamo Mwenyekiti wa Klabu ya Wandishi wa habari kisiwani Pemba (PPC) anasema, katika kupiga vita unyanyapaa kwa wagonjwa wa TB wanatoa elimu kwa jamii kuacha tabia ya kuwanyanyapaa wagonjwa wanaougua ugonjwa huo.

 ‘’Sisi kama wandishi wa habari  tunaelimisha jamii kupitia vipindi na makala mbali mbali ili kuachana na masuala hayo, kwani maradhi humfika kila mja,". anaeleza.

 Anasema, ili kupunguza tatizo hilo ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake kuendeleza juhudi za kutoa elimu kwa jamii, kufahamu madhara ya unyanyapaa kwa wagonjwa wanaougua TB, kuondosha maambukizi ili jamii ibaki salama.

 TAKWIMU

 Ripoti za Taifa za kifua kikuu zinaonyesha kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar, imepiga hatua katika kupunguza maambukizi, ambapo kiwango cha kuenea kimeshuka kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 183 mwaka 2023.

 Hata hivyo changamoto bado zipo kwani wagonjwa wengi hawafiki hospitali mapema, kutokana na hofu ya kutengwa ama kusemwa vibaya.

 SERA NA MIKAKATI

 Shirika la Afya Duniani (WHO) limezindua mkakati wa 'End TB Strategy' unaolenga kuondoa TB ifikapo mwaka 2030, chini ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 3.3), ambapo mikakati hiyo imepewa kipaumbele katika kupunguza unyanyapaa na kutoa elimu kwa jamii.

 Serikali kupitia Zanzibar Integrated HIV, TB and Leprosy Programme (ZIHTLP) imeanzisha kampeni za uhamasishaji na upimaji wa mapema, huku Wizara ya Afya Zanzibar iikiweka msisitizo kwenye elimu ya jamii, usiri wa huduma na ufuatiliaji wa karibu wa wagonjwa.

 NINI KIFANYIKE

 Ili kuona unyanyapaa kwa wagonjwa wa TB umeondoka ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake kuchukua hatua ya kuelimishana, kuachana na tabia ambazo zinachangia kwa asilimia kubwa kuenea kwa mambukizi yatokanayo na maradhi hayo," wanasema wanajamii.

 Hata hivyo endapo wagonjwa wataangaliwa kama mzigo katika jamii, ni kuzima matumaini yao na juhudi za afya ya umma.

 Kwa pamoja jamii na Serikali zinaweza kushinda TB si kwa dawa pekee, bali pia kwa kuondoa woga na unyanyapaa. 

 'Zanzibar bila Kifua Kikuu inaweezekana, kwa pamoja tunaweza'.

 

                            

 

 

 


Comments

Popular posts from this blog

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO

‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’