MRADI WA SWIL ULIVYOLETA MABADILIKO KWA WANAWAKE WENYE ULEMAVU PEMBA

 


NA FAMA HAMAD, PEMBA

Mradi wa kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi , demokrasia na siasa (SWIL) umeandika historia mpya katika visiwa vya Zanzibar, umeleta nuru na matumaini kwa wanawake, hususan wale wenye ulemavu, waliokuwa kwa muda mrefu wakihisi kusahaulika katika safari ya maendeleo na uongozi.

Mradi huo ulizinduliwa rasmi mwaka 2020 na unatarajiwa kumalizika Disemba 2026 umeonekana na mafaniko makubwa katika hatuwa mbalimbali za utekelezaji wake. 

Utekelezaji huo wa (SWIL) ni ushirikiano kati ya TAMWA-ZanzibarZAFELAJUWAUZA, na PEGAO, umewafikia wanawake zaidi ya 4,000 katika wilaya za Pemba na Unguja, ukiwajengea uwezo, ujasiri, ari na ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Lengo kuu la mradi ni kuongeza ushiriki wa wanawake, ikiwa ni pamoja na wanawake wenye ulemavu, katika michakato ya uongozi, siasa na demokrasia Zanzibar (Unguja na Pemba) hivyo kuwawezesha kuwa “watendaji hai” badala ya kuwa katika pembezoni.

Utekelezaji wa mradi huo kwa sasa umeshawafikia  na kuwawezesha zaidi ya wanawake 6000 kwa zanzibar, Unguja na Pemba katika kudai haki zao ili nao waweze kuwawezesha wengine, ambapo tayari umeonyesha njia kwa Wanawake Wenye Ulemavu  katika kufikia hatuwa ya kudai haki zao za uongozi.

 Mradi huo wa SWIL  unafadhiliwa na ubalozi wa Norway unatekelezwa maeneo mbalimbali ambapo kwa upande wa  Pemba tayari   umeshawafikia wastani wa wanawake 4000.

 Katika hatuwa za kufanikisha lengo la mradi la kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi demokrasia na siasa kumeundwa kamati za Wilaya za kuhamasisha wanawake kudai haki zao za uongozi.

 Kamati hizo zinajulikana kwa jina la kiutaalamu 'citizen brigged' asilimia 60 ni wanawake na 40 ni wanaume ambao ndio walengwa wakuu wa kutowa ushirikiano kufikia malengo ya mradi huo.

Wanawake wenye ulemavu waliunganishwa zaidi na mradi kupitia Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), waliweza kupata mafunzo na kutambuliwa kama wanaharakati na haki zao.

Hivyo (JUWAUZA) Ofisi ya Pemba imetoa ushuhuda wa wanawake wenye ulemavu ambao kupitia mafunzo ya SWIL waliyoyapata  waliweza kuhamasika, na katika uchaguzi mkuu wa 2025 walijitokeza kwa wingi majimboni ambapo walikua ni 12, kwa Pemba pekee, ingawa hawakubahatika kuyakamata majimbo hayo.

JUMUIA YA WANAWAKE WENYE ULEMAVU INASEMANINI JUU YA HILO

Hidaya Mjaka Ali kutoka jumuia ya wanawake wenye Ulemavu kisiwani Pemba anasema Mradi wa SWIL umewanufaisha wanawake wenye Ulemavu, kwani katika Uchaguzi wa mwaka huu 2025 Wanawake  wenye ulemavu kisiwani Pemba wamehamasika na wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, ambapo haijawahi kutokea katika chaguzi zilizopita.

Anasema jambo ambalo limepelekea wanawake hao kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea ni kutokana na elimu walioipata kupitia mradi wa SWIL, iliyokua ikitolewa na Tamwa Zanzibar na Pegao.

‘’Haijawahi kutokea wanawake wenye ulemavu kujitokeza wengi kugombea nafasi za uongozi na kufikia idadi ya 12, hivyo napata kusema mradi wa Swil unatusaidia sisi wanawake wenye ulemavu,’’anasema.

Anasema katika miaka ya nyuma wanawake wenye ulemavu walikua wakiachwa nyuma katika fursa mbali mbali, ingawa mradi wa SWIL umewaona, umewasadia na wameweza kufahamu haki zao na nafasi zao.

Anasema licha ya kuwepo kwa changamoto ambazo zimekua zikijitokeza kwa wanawake wenye ulemavu, wamejenga uthubutu wa kuwania nafasi mbali mbali za uongozi.

USHUHUDA WA WANAWAKE WENYEWE WENYE ULEMAVU

  Halima Suleiman Ali mwenye ulemavu wa uoni hafifu mkaazi wa Mtambile Mkoani Pemba, anasema awali  alikosa utayari katika kushiriki  mchakato wa kutafuta nafasi ya uongozi hususani  majimboni.

Anasema kupitia mradi huo ameweza  kujiamini na kuongeza uthubutu wa kuwania nafasi ya Udiwani licha ya kushindwa  kutokana na sababu zilizopo katika michakato ndani ya  vyama.

 ‘’Kutokana na uwelewa na ujasiri nilioupata nimethubutu  kuchukua fomu ya kugombea Udiwani katika wadi yangu ya Mtambile,’’anasema.

Anasema katika maisha yake hakua na imani kama kuna siku atachukua fomu na kugombea, kwani hakua na elimu hiyo, ingawa kupitia SWIL anajivunia kwani ameondokana na woga na ndio maana 2025, akachukua fomu kwa ajili ya kuusaka Udiwani.

Amina  Abdala Said mwenye ulemavu wa viungo mkaazi wa  Changaaweni Mkoani Pemba, anasema mradi wa SWIL  umemjenga kwani amekua na uthubutu na  mwaka huu 2025, amekua Diwani wa viti maalumu kupitia Chama cha ACT WAZALENDO wadi ya Changaweni.

‘’Baada ya kupatiwa mafunzo licha ya kua sikujitupa jimboni ila nilingia kwenye kinyanganyiro cha viti maalumu kuwania udiwani na nashukuru nimefanikiwa kuikamata nafasi hiyo.

 Mwengine ni Katija Mbarouk Ali mwenye Ulemavu wa viungo mkaazi wa Kiuyu Minungwini wilaya ya Wete Pemba, anasema awali  hakua na uthubutu wa kushiriki katika mchakato wa kutafuta nafasi ya uongozi hususani katika majimbo, ingawa kupitia mradi huo ameweza kujitolea ,kujiamini na kuongeza uthubutu kuwania nafasi ingawa hakubahatika kuitia mkononi  nafasi.

JAMII

 Salim Khamis Juma  (43) mkaazi wa Wingwi Micheweni  anasema kabla ya kuja mradi wa SWIL wanawake hawakujuwa haki zao na ndio maana ikawa nafasi nyingi ilikua zinachukuliwa na wanaume na wao sikuzote kubakia mkiani.

 Anasema hatuwa inayochukuliwa na mradi kupita kila shehia  kuweza kutowa elimu hiyo ni ya mfano kwa vile wanawake wengi walikuwa wamelala katika suala la kudai haki zao hasa za uongozi na kuwaachia wanaume peke yao.

 “Mimi mwenyewe nilikuwa naona kama hakuna umuhimu wa wanawake kuwa viongozi, ila kumbe  tukiwapa wanawake kuongoza kuna mafanikio mengi yanaweza kupatikana kwa mfano Raisi wetu Mama Samia ambavyo anapambana tumepata neema kubwa kupitia kwake, kwa vile wao ni waaminifu kuliko ata sie wanaume

Yumna Khamis Ali  (32) wa Kinoe Konde anasema elimu inayotolewa na mradi wa Swill imeweza kuwafunuwa macho wanawake wengi na wanaelewa kuwa zipo fursa mbalimbali wanazikosa kutokana na nafasi nyingi kuchukuliwa na wanaume.

 “Huku vijijini zamani tulikua tuko nyuma  hasa katika masuala ya uongozi kwani tulikua tumezoea kwamba mwanamke ni mtu wa kukaa nyumbani tu na si wa kuwa kiongozi, ingawa kwa sasa mambo yamegeuka,’’anasema.

 WANAHARAKATI

 Mkurugenzi mtendaji wa mradi wa Swill kutoka PEGAO Hafidh Abdi Said anasema kwa Pemba mradi umevuuka lengo kwani wameshawaelimisha  zaidi ya watu na waliokusudiwa.

 Anasema uhamasishaji huo haukulenga tu kuwajengea uwezo wanawake hao kuwa viongozi serikalini wala vyama vya siasa pekee bali hata ndani ya sekta zilizomo kwenye jamii.

 "Wanawake wenye Ulemavu hawatakiwi tu kuingia ndani ya Serikali  bali hata ndani ya vyama, kamati za maendeleo , jumuiya , nafasi za usheha na maeneo mengine",alisema.

 Anafahamisha kuwa idadi ya wanawake wenye Ulemavu katika kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa mwaka 2025, imeongezeka, licha kwamba katika nafasi za maamuzi bado ni wachache.

 Mkurugenzi wa TAMWA  Zanzibar  Mzuri Issa Ali anasema mradi wa SWIL umefanikiwa kwa kiasi kwani katika jamii suala la itikadi  potofu za kua mwanamke hawezi kuongoza limepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla ya mradi huo.

‘’Kwa kweli SWIL imeikomboa jamii na hata wanawake, kwani umepunguza ile dhana potofu kwa jamii kwamba mwanamke hawezi kuongoza, kazi yake ni mama wa nyumbani tu,’’anasema.

 Bakar Mussa Juma, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wandishi wa Habarai kisiwani Pemba (PPC) anasema elimu iliyoitolewa   kupitia mradi huo  wamenufaika  katika kuisaidia jamii kuthamini mchango wa wanawake, na kuandika habari zenye kuitetea jamii ya wanawake, kuanzisha madawati ya kijinsia katika vyombo vyao.

Balozi wa Norway kutoka Tanzania Tone Tinnes anasema ili kufikia ndoto za wanawake wenye ulevu juu ya suala la usawa wa kijinsia, ni lazima kwa watekelezaji wa mradi huo wa SWIL, kuendeleza mapambano ya hali ya juu, bila kujali mitazamo ya watu wasio watakia mema wanawake hao.

Anasema mabadiliko hayapatikani kwa mara moja, na kuielimisha Jamii juu  ya masuala ya kijinsia sio jambo rahisi,  ni vyema kuongeza mapambano ya  hali ya juu ili kuhakikisha lengo la usawa linafikiwa.

 ‘’Mabadiliko hayawezi kupatikana tu kirahisi, inabidi tufanye kaze ya kuielimisha kidogo kidogo mpaka siku itafika na wanajamii wataelewa,’’anasema.

 VIONGOZI WA DINI

 Sheikh Said Ahmad Mohamed kutoka ofisi ya Mufti kisiwani Pemba anasema mwanamke hajakatazwa kuwa kiongozi na hasa akiwa atazingatia maadili ,mila na desturi za dini na jamii yake.

“Yapo mambo hupaswa wanawake wajiamulie wenyewe na sio busara kuona mifumo dume inatawala hadi kwa mambo ambayo ni ya pamoja au yanawahusu wanawake pekee,”alisema. 

Robati Migua Ndalami kiongizi wa dini Kwa upande wa Kikristo kutoka Chakechake anasema hata dini yao haijamktaza mwanamke kuongoza  kwani  kuna mabo ambayo yanawahu na yanatakiwa wayazungumze  wenyewe.

Takwimu

Katika Uchaguzi wa mwaka huu 2025, unaweka historia mpya, kwani ni mara ya kwanza wanawake kujitokeza kwa wingi

Ripoti za vyombo vya habari na mashirika ya jinsia zinaripoti ongezeko la wanawake wanaogombea mwaka 2025 ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.

 Zanzibar pia imeona wanawake wakichukua nafasi kubwa katika kuingia kwenye nafasi za juu za uongozi,ikiwa ni sehemu ya mwelekeo wa kitaifa wa kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa.

MIKATABA

Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), wa mwaka 2006  kinahimiza serikali, kuhakikisha ushiriki sawa wa watu wenye ulemavu katika siasa na maamuzi.

Hata Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na haki za kisiasa ya mwaka 1966 ibara ya 25, kila raia ana haki ya kupiga kura na kuchaguliwa, katika uchaguzi wa kisiasa.

Katiba ya Zanzibar ya 1984,kifungu chake cha 21(1) nacho kinatambua haki ya kila raia, kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi bila ubaguzi.

Kifungu kidogo cha (3) kinaeleza kwamba, kila mzanzibari anayohaki ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyoko chini ya mamlaka ya Zanzibar.

Sheria ya watu enye ulemavu namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 29 kinaeleza, umuhimu wa watu wenye ulemavu kufikia miundombinu pamoja na taarifa, mawasiliano na haki zote za kibinadamu.

Katika Nchi ya Nordic ilikua ya kwanza duniani kuanza upendeleo wa kijinsia wa asilimia 40,kwenye bodi za kampuni zilizoorodheshwa mwaka 2005, ikianzisha msukumo wa kimataifa wa kulazimisha kampuni kuwa na wanawake wengi kwenye bodi.

Makampuni makubwa ya binafsi ya Norway lazima yawe na bodi ambazo zinajumuisha angalau asilimia 40, ya wanawake au yatafungwa serikali ilipendekeza katika muswada katika msukumo zaidi wa kuvunja dari ya kioo inayozuia wanawake kufikia nafasi za juu.



Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO