BISHAMBA ALI ALAWI: MWANAMKE MWENYE UTHUBUTU PEMBA
NA FATMA HAMAD, PEMBA
‘’Mwanamke akipewa nafasi ya kumiliki ardhi na akajishughulisha
na kilimo, basi haachi nyayo pekee ardhini, bali huacha alama ya mafanikio,’’
Hayo si maneno ya mtu mwengine bali ni mwanamke mpambanaji
mkaazi wa shehia Kambini Wilaya ya Wete Pemba, Bishamba Ali Alawi.
Katika mazingira ya kawaida ya vijijini, mwanamke huyo sasa
ni kielelezo tosha jinsi kilimo msitu (Agro forest) kinavyombadilisha maisha
yake.
Anasema, alipitia ugumu kwenye maisha yake kutokana na
kukosa kazi ya maana ya kujikwamua kiuchumi ingawa hakukata tama.
Lakini tangu mwaka 2023 aliposhiriki mafunzo ya kilimo msitu,
alianza kuona mabadiliko ya maisha kuwa mazuri kwa upande wake.
Kupitia mafunzo yaliotolewa na Chama cha Wandishi wa Habari
Wanawake Tanzania (TAMWA) kwaupande wa Zanzibar na Jumuia ya Uhifadhi wa Misitu
Pemba (CFP), Bishamba alijifunza kuchanganya aina ya miti mbali mbali kwenye
shamba lake.
Walifunzwa kwamba, uchanganyaji wa miti kwenye shamba moja unasaidia
kupata mazao kwa ajili ya chakula na biashara, huku wakidhibiti madhara
yanayoweza kutokea ikiwemo mmong’onyoko wa ardhi na mabadiliko ya tabianchi.
Katika shamba lake mama huyo amepanda migomba, miparachichi,
mboga, njugunyasa, choroko, miembe,mikungu na midimu.
Anasema, hali hiyo pia inapunguza gharama za mbolea na
kuongeza mavuna, ambayo inasaidia ustawi bora wa maisha ya mazao hayo.
Anasema, mwakajana alipovuna kwa mara ya kwanza mazao yake,
alifanikiwa kupata chakula na mazao mengine aliuza na kupata fedha ambazo
zimemuinua kiuchumi.
‘’Siku ile ya Jumapili nilipopata pesa yangu baada ya kuuza
mazao, nilijua huu ni mwanzo mpya wa maisha yangu,’’anasimulia kwa tabasamu Bishamba.
Anaeleza, kwa sasa ameboresha vya kutosha shamba lake na
limesheheni miti na mazao, hivyo hataabiki kwa chakula, mboga wala pesa za
matumizi.
Hadi sasa ameshavuna zaidi ya mara tatu na bado mazao
yamejaa shambani, anasubiri yapee aanze kuvuna.
‘’Tangu nianze kulima kilimo hichi sihangaiki wala
simsubirii mume wangu arudi na safari zake ndio nipate chakula, kwani ndizi,
mboga, mihogo napata shambani kwangu,’’anaeleza.
Anasema kilimo msitu kimekua mkombozi kwake kwani amekua akijipatia mahitaji yake yote anayoyahitaji,
pia amekuwa akiwasaidia wanawake wengine kufanya shughuli hizo, ili nawao
wajikomboe kiuchumi waondokane na umasikini na utegemezi.
‘’Nimeshafundisha wanawake takribani 12 juu ya kilimo hicho,
ambapo wengine wamekua viongozi wakulima matioti, wengine wamekua wakulima wakubwa na wameanza
kufaidika’’,anasema.
Anasema, alipoanza shughuli ya kilimo jamii ilimchukulia
kama hana kazi na amechanganyikiwa tu maisha, ingawa sasa wanayaona matunda
yake na wanatamani kuwa kama yeye.
‘’Mwanzo wananchi walinisimanga, kunikebehi na kuonekana
kama sina kazi, ila sasa hivi wananishangaa na kila mmoja amehamasika anataka
nimfundishe kwa faida ninayoipata,’’ anasimulia.
KUTOKA
SHAMBA HADI UONGOZI
Sasa Bishamba aligombea nafasi ya viti maalumu ingawa
hakubahatika kupata, lakini akiwa hai atahakikisha anaingia tena kwenye
kinyang’anyiro cha kugombea ifikapo mwaka 2030.
Anasema, mbali na kujipatia pesa na chakula, bali mafunzo
hayo yamemjengea uthubutu na ujasiri wa kusimama pahala popote kuzungumza bila
woga.
‘’Kabla sijaanza mradi huu wa kilimo msitu ilikuwa siwezi
hata kusimama mbele ya watu wawili tu, lakini sasa sina woga, nimekuwa kiongozi
kwa sababu nawafahamisha wanawake umuhimu,’’anasema.
‘’Nina miaka 54, sijawahi kujiingiza kwenye harakati za
uongozi, lakini mara hii baada ya kujengwa na kuandaliwa kupitia mafunzo hayo,
nimejaza fomu ya uwakilishi viti maalumu lakini sikufanikiwa,’’ anaeleza.
Hadithi ya Bishamba sio tu simulizi ya mavuno na mapato bali
ni alama ya uthubutu wa mwanamke wa kijijini, anaeamua kusimama imara katika
harakati zake za kiuchumi na kisiasa.
Uthubutu huo wa Bishamba unatoa mwanga kwa wanawake wengine
wa Pemba na Zanzibar nzima kwamba uongozi na maendeleo endelevu vinaweza
kuanzia shambani.
Jirani wa Bishamba, Sharif Hamad Sharif mkaazi wa Kambini
Kichokochwe anamuelezea mama huyo kuwa ni wa kawaida tu kijijini, ingawa kwa
sasa amekuwa mfano wa kuigwa.
‘’Tulikua tunamchukulia kama mama ambae hana uwezo wowote,
ingawa kwa sasa ni mwanamke wa mfano, kutokana na kujituma kwake na ameweza
kutuamsha na sisi,’’ anaeleza.
Khadija Ali Faki mkaazi wa Chwale ni mwanamke ambae
amejengewa uwezo na uthubutu na Bishamba, amejiingiza kwenye harakati za kilimo
msitu na sasa ameondokana na utegemezi katika maisha yake.
Yeye alikuwa ni mama wa nyumbani tu na hakua
akijishughulisha na kazi yoyote, hali ambayo ilikua ikimfanya kuishi mazingira
magumu.
‘’Nilikua nikimtegemea mume wangu kwa huduma zote, jambo
lilikua likiniwia vigumu mana maskini hawezi kuzimudu shida zote,’’ anaeleza.
Anasema, baada kupatiwa elimu na Bishamba, anaamini hali
itabadilika, kwani analima kilimo msitu atapata mazao kwa ajili ya chakula na
biashara, ili apate pesa za kujitatulia shida zake.
TAMWA
WANASEMAJE
Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar
kimekua mshirika mkuu katika kumuinua Bishamba na wanawake wengine kupitia
miradi mbali mbali.
Ambapo, katika tamko lao la Machi 2024, linasisitiza kwamba…
‘Sera za jinsia lazima ziwepo katika sekta zote, ili wanawake wasiachwe nyuma’
‘’Tunataka wanawake washiriki sio tu mashambani bali pia
kwenye meza za maamuzi na ndio maana tunawawezesha kwa namna zote ili lengo
letu likamilike,’’ anasema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka TAMWA
Zanzibar, Sofia Ngalapi.
Anasema, katika mradi wao wa
kilimo msitu (ZanzAdapti) ambao
wanautekeleza pamoja na CFP Pemba, CFI kutoka Canada, unawasaidia wanawake wa pwani
na visiwani, kuimarisha nafasi zao katika kilimo, mazingira na uongozi.
CFP
Mtetezi wa masuala ya wanawake kutoka Jumuia ya Uhifadhi wa
misitu kisiwani Pemba (CFP) Sada Juma Segeja, anasema wanafanya mambo mbali mbali
kuhakikisha wanawake wanapiga hatua.
Anasema, moja ya jambo ambalo wanalifanya katika shehia nne
wanazotekeleza mradi wa kilimo msitu, ni kuwapa mafunzo ya biashara, ili wawe
huru kiuchumi.
Alizitaja shehia hizo kuwa ni Mchangamdogo, Kambini
kichokochwe, Chwale na Kiuyu Minungwini.
Anasema, pia wanawapatia mbegu bora na miche ya kisasa, huku
wakiunda vikundi vya wanawake vya msaada wa pamoja na biashara.
TAKWIMU
Kwa mujibu wa utafiti wa CFP wa mwaka 2022 unaonesha kuwa,
zaidi ya wanawake 2,500 Pemba wameshiriki katika kilimo msitu.
Ikiwa ni asilimia 60 ya wanawake hao wameripoti kipato cha
kaya kuongezeka mara mbili ndani ya miaka mitatu, jambo ambalo ni furaha kwao.
Inaeleza kuwa, zaidi ya miti milioni mbili imepandwa kupitia
kwa vitalu vya kijamii.
KILIMO
MSITU NA MAPAMBANO DHIDI YA TABIANCHI
Kila shamba linapandwa miti 100-200, inayosaidia kufyonza
gesi ukaa na kulinda vyanzo vya maji.
Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) limeeleza,
kilimo msitu kina uwezo wa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 20,
katika vijiji vya Pemba ndani ya miaka kumi ijayo.
MAFANIKIO
YA KIMATAIFA
Katika nchi ya Kenya wanawake wa Machakos wamepunguza ukame
kwa kupanda miti kupitia kilimo msitu.
Ambapo kwa upande wa Uganda nako wanawake wa kijiji cha Mbale
wamepanda zaidi ya miti milioni moja, wakiboresha kipato na mazingira yao.
NINI
KIFANYIKE
Mafanikio ya Bishamba yanaonesha kuwa mwanamke akipewa
nafasi na msaada sahihi, anaweza kuvuka mipaka ya mazoea na kuwa sauti ya
mabadiliko.
Hivyo ipo haja kwa Taasisi na Mashirika mbali mbali kuwasaidia
wanawake, wawe na maendeleo bora ndani ya jamii.
MWISHO.
Comments
Post a Comment