Serikali kujenga uwanja wa ndege wa kisasa Pemba



NA FATMA HAMAD, PEMBA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane imedhamiria kufanya mageuzi  makubwa katika sekta ya Usafiri wa Anga Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma katika uwanja wa ndege wa Pemba pamoja na kuifungua Pemba Kimataifa.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hussein Ali Mwinyi katika uzinduzi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na Barabara ya Mkoani Chake Chake uliofanyika Viwanja vya uwanja wa Ndege Pemba.

 Alisema ujenzi wa miradi hio ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM  ya mwaka 2025 ambapo malengo ya serikali ni kuhakikisha kuwa Pemba inakuwa na Uwanja wa ndege wa Kimataifa ambao utaifungua Pemba kwa kukuza utalii, uwekezaji na biashara. 

 Alisema  kuwa  serikali imejipanga katika kuhakikisha barabara zote za Zanzibar zinajengwa kwa kiwango cha lami na kuwa katika hali nzuri kwa kuhakikisha zinafanyiwa matengenezo pale inapohitajika.

Aidha,  alisema miradi hio itakapokamilika itapelekea kuimarika kwa huduma za usafiri wa anga na kuifungua Pemba kiuchumi kwa kuongezeka shughuli za kibiashara, kuimarika kwa sekta ya utalii itskayochangia kuongezeka kwa pato la Taifa na kupunguza umasikini kwa wananchi.

 Sambamba na hayo ametoa wito kwa Mkandarasi wa ujenzi wa uwanja huo kampuni ya PROPAV INFRASTRUCTURES na mshauri elekezi  Alhandasah Consultant kuifanya kazi hio kwa umakini na kua kwenye viwango vya Kimataifa na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

 Alifahamisha kuwa maendeleo yoyote yanahitaji kuwepo kwa Amani, Umoja na mshikamano hivyo amewaasa wazanzibari kuendelea kuidumisha amani iliyopo nchini pamoja na kuwataka kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa  ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya nchi.

 Kwa upande wake waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi  Khalid Salum Muhammed alisema Rais Dkt. Hussein Mwinyi amedhamiria kuifungua Pemba kiuchumi kwa kujengwa miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na Barabara ya Mkoani Chake Chake.

 Alisema Wizara ya Ujenzi inaendelea na ukarabati wa Bandari ya Mkoani ambayo itakuwa na uwezo wa kupakia meli kubwa kutoka nje ya nchi jambo litakalochochea ukuwaji wa uchumi kisiwani Pemba.

 Akisoma taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,Mawasiano na Uchukuzi Dkt. Habiba Hassan Omar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi kubwa katika kuimarisha huduma za Usafiri wa Anga na Barabara kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi na kuwaondolea usumbufu wananchi na wageni wanaofika  Zanzibar.

 Alisema Utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba umeanza rasmi Novemba 2024 na unatarajiwa kuchukua muda wa miezi 36 kumalizika kwake. 

 Mkandarasi wa ujenzi wa Uwanja  huo ni  Kampuni ya PROPAV INFRASTRUCTURES kutoka nchini Hispania na Msimamizi wa ujenzi ni Kampuni ya DAR AL HANDASAH CONSULTANTS kutoka Lebanon unatarajiwa  kugharimu jumla ya EURO Milioni 170. 

 Ujenzi wa Uwanja huo utahusisha Jengo jipya la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria wasiopungua laki tatu nanthelathini kwa mwaka ikiwemo abiria wa ndani (Domestic) na abiria wa kimataifa (International) pamoja na ujenzi wa Njia ya kuruka na kutua Ndege (Runway) yenye urefu wa mita 2,510 na upana wa mita 45 utakaokuwa na uwezo wa kutua ndege zote za aina ya Code 4C.

 Kwa upande wa Utekelezaji wa Mradi wa barabara ya Mkoani – Chake chake  yenye urefu wa (43.5km) inayojengwa na Kampuni ya PROPAV INFRASTRUCTURES ya Hispania ikisimamiwa na  Kampuni ya DAR AL HANDASAH CONSULTANTS ambayo inatarajiwa kuchukua muda wa miezi 36 hadi kumalizika kwake.

 Ujenzi wa barabara ya Mkoani Chake Chake utagharimu zaidi ya  EURO milioni 93 itakayohusisha njia za watembea kwa miguu,  taa za barabarani (streetlights) pamoja na alama zote muhimu za usalama wa barabarani.

 Alisema  pinidi ikikamilika barabara hiyo itawarahisishia wananchi kuzifikia huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa urahisi pamoja na kuunganisha mji wa Mkoani ambapo kuna Bandari ya Mizigo na abiria ya Mkoani na Mji wa Chakechake.

 Mkurugenzi wa Kampuni ya PROPAV INFRASTRUCTURES Bwana Cristiano Becker alisema wanatambua kuwa uwanja wa ndege ni mlango mkuu na daraja la kuiuganisha Pemba na dunia hivyo ameahidi kuujenga uwanja huo kwa viwango na ubora unaokubalika Kimataifa.

 Christiano alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeiamini Kampuni ya PROPAV INFRASTRUCTURES na kuipa mkataba wa kuujenga uwanja huo hivyo kampuni yake Itajenga Uwanja wa Ndege wenye hadhi na sifa zote za Kimataifa utakaoifungua Pemba kiuchumi na kiutalii.

 Akizungumzia ujenzi wa barabara ya Mkoani Chake Chake Christiano alisema  ahadi yake ni kujenga barabara hio kwa uaminifu mkubwa na yenye viwango vinavyoendana na mustakbali wa Pemba inayotakiwa itakayowavutia zaidi wawekezaji, kukuza uchumi na kuongezeka kwa ajira.

 Alisema ujenzi wa Mradi wa Uwanja wa ndege wa Pemba pamoja na barabara ya Mkoani Chake Chake utatoa ajira zaidi ya elfu moja kwa wakaazi wa Pemba, wananchi kupata fursa ya kufanya biashara ndogo ndogo pamoja na mafunzo na ujuzi kwa vijana watakaopata fursa ya kufanya kazi na kampuni ya PROPAV INFRASTRUCTURES.

 




 

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO