Unyanyapaa ulimsukuma Maryam kujifungulia nyumbani

 

Ilikuwa chanzo kumuambukiza mtoto wake VVU

Sasa anao watutu wakiwa salama, kama alivyo muume wake

NA FATMA HAMAD, PEMBA

MIMBA yangu ya kwanza nilijifungulia nyumbani kwani nilikua nanyayapaliwa, na ndio chanzo cha kumuambukiza mtoto wangu VIRUSI vya Ukimwi.

Hayo ni maneno ya Maryam Said mkaazi wa Chake chake mwenye umri wa miaka 38 ambae anaishi na virusi vya ukimwi kwa muda wa miaka 18 sasa.

Anasema alimuambukiza mtoto wake wa mwanzo mambukizi ya virusi vya UKIMWI

 Mimba yake ya kwanza, alijifungulia nyumbani, kwa hofu ya kwenda Hospital kwa kuogopa kunyanyapaliwa.

‘’Hadi leo najilaumu, na najutia nafsi yangu, kwa kitendo cha kutokimbilia hospitali kwa ajili ya kwenda kujifungua nikidhani kwamba nyumbani ni salama,’’anasimulia.

 Kwa sasa  ameshajifungua watoto  wengine watatu, ambao wako salama hawana   maambukizo  ya  VVU , baada ya kusikiliza na kutekeleza kwa vitendo ushauri wa watalamu wa afya.

 aligundulika na Virusi Vinavyosababisha  UKIMWI ( VVU)  mnamo tarehe 5/7/2005, wakati  alipokwenda Cliniki ya ujauzito, na hapo alianza kupewa ushauri na kuanzishwa kutumia dawa za kupunguza  makali ya VVU  ( ARV).

Anaeleza baada ya kupata majibu hayo alishikwa na simanzi na huzuni, na hakuweza kutumia dawa hizo, kwani akitaka nyumbani kwao wasijue mtihani huo uliomtokezea.

Na ndio mana ikapelekea mtoto wake huyo wa mwanzo kumuambukiza, kwani hakuwa akitumia  dawa za ARV.

‘’Sikufuata ushauri wowote wa daktari nilibakia tu nyumbani kwani nilikua na hofu, ili nisije nikagundulika kama nina VVU,’anasema.

Anasimulia kwamba  takriban  miaka  18  iliyopita , vitendo  vya kuwatenga  watu wanaoishi na VVU vilikuwa ni  vingi  sana.

“Watu wenye maambukizo ya VVU  hawakujitokeza hadharani  wala kufuata huduma za afya, kila mtu  aliogopa kusemwa, ‘’ anasimulia.

CHANGAMOTO AliZOZIPATA BAADA YA KUGUNDULIKA NA VIRUSI  VYA  UKIMWI.

Baada ya wazazi waeke walipogundua kama ana VVU  walimtenga na kumnyanyapaa.

‘Nilipata shida sana kwani nilinyanyapaliwa kutoka kwenye familia yangu hadi kwa majirani, sikuwa na mtu hata mmoja ambae alikua ananipa msaada wowote, ‘’ anaeleza.

Alikua anaishi kwa mateso na dhiki, ilipofika siku ya kujifungua, alijifungulia nyumbani kwao hakuenda Hospitali, kwani hakupata mtu wa kumshughulikia na kumpeleka, na pia alikua ana hofu ya kwenda kunyanyapaliwa.

 ‘’Nilijifungulia nyumbani kwani sikupata msaada wa mtu wa kunishughulikia na kunipeleka Hospitali, na hapo ndipo nilipomuambukiza mtoto wangu virusi, kwa vile hakupata huduma za kitalamu,’’anasimulia Maryam.

Anasema kitendo hicho cha kumsababishia mtoto wake kupata maambukizi  kinamtia huzuni na hatokisahau, na hatoacha kujilaumu maishani mwake.

Wakati akiwa na umri wa miezi miwili, mtoto  wake huyo aliumwa na homa  na kumpeleka  Hospitali, baada ya kupimwa nayeye akagundulika tayari ana VVU.

Hapo alipatwa na uchungu na akahisi kuwa hana tena faida yoyote ya kukaa tena katika dunia.

‘’Sikufichi nilipofika nyumbani nilichukua dawa ya Panya ili nijiuwe, nikataka kuanza kumpa mwanangu ila roho ya uzazi ikanijia, pamoja na rehma za Mungu, sikuweza ile chupa ika anguka chini na dawa ikamwagika.

Baada ya hapo alimchukua mtoto wake na kwenda kwa msamaria mwema kwenda kuomba msaada, ili amuhifadhi kutokana na shida alizonazo.

‘‘Yule mtu alichonisaidia alinichukua na kuniunga katika Jumuiya ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI  ( ZAPHA+) , ambapo hadi sasa nimekuwa Mwenyekiti wa jumuia hiyo  katika wilaya ya Chake chake na hapo ndipo nikaanza kupata elimu na hadi sasa nimekua mshauri mzuri’’.

Maryam  kwa sasa ameolewa na mume mwengine ambae hana maambukizi ya VIRUSI vya Ukimwi, ambapo amezaa watoto wengine watatu, na wote wako salama.

‘’Nashukuru sahivi nimeolewa na mume ambae hana mambukizi,  yuko salama,  kwa  vile  tunafuata ushauri wa daktari,’anasema.

Anasema jamii isiwanyanyapae watu wanaoishi na VVU, pia wasivunje ndoa au familia, endapo mmoja kati ya mwanandoa  atagundulika na virusi, kwani wanaweza kuishi bila kuambukizana.


     TATIZO  LA  UNYANYAPAA

Utafiti uliofanywa wa kuangalia matendo ya unyanyapaa katika  jamii ( Stigma index) uliofanywa na taasisi  ya  ZAPHA+ mwaka 2019, ulibaini kwamba vitendo vya unyanyapaa bado vipo.

Utafiti umeonyesha bado  vitendo  hivi vipo katika jamii,kwenye familia, sehemu ya kutolea  huduma kwa watu  wanaoishi na  VVU na mikusanyiko ya jamii.

Pengine kwa  Mariam kama visinge kuwepo vitendo  vya unyanyapaa kwa watu  wanaoishi na VVU  kwenye familia, angaliweza kuzuia  maambukizo  ya VVU  ya siende kwa mtoto wake.

‘’Kwa sasa  vitendo  hivi   vimepungua na watu  wanapatiwa huduma ,lakini miaka 18 iliyopita haikuwa rahisi kwangu kujitokeza  hadharani,’’anasema.

 HUDUMA YA KUZUIA MAAMBUKIZO YA VVU  KUTOKA KWA MAMA  KWENDA KWA WATOTO

Serikali imeanzisha huduma hii  kwa ajili ya mama  wenye maambukizi ya  VVU, wapate huduma na  waondoe  uwezekano  wa kumuambukiza  mtoto, wakati wa kujifungua  ama kunyonyesha.

Kutoka  na taarifa huduma hii kwa sasa ina  ufanisi  wa matokeo  ya  zaidi  ya asilimia  90  ya kuwalinda watoto  wasipate maambukizi.

Mratibu  wa Tume ya UKIMWI Pemba, Ali Mbarouk Omar, anasema kwa sasa huduma ya kuzuia  maambukizi  ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ina ufanisi mkubwa.

‘’Wastani wa mfano wa watoto 100, waliozaliwa na  mama  wenye maambukizo  ya  VVU basi 95 kati  yao kwa upande wa Zanzibar wanaweza kuzaliwa salama.

Haya ni mafanikio  makubwa ya kuzuia maambukizo  kutoka kwa  mama  kwenda   kwa mtoto, ‘’ anasema


FAMILIA YA MARYAM

Hamad Omar Ali (siojina lake halisi) ni kaka wa Maryam alikubali kwamba, kabla hawajapata elimu kuhusu masuala ya UKIMWI, walimtenga na kumsusa ndugu yao huyo.

‘’Ni kweli kwamba mwanzoni kabla hatujapata elimu tulimtenga, hatukilanae, hatukimshirikisha  kwa lolote la kifamila,anaeleza.

Anasema kwasasa  wamekua  nae bega kwa bega amekua msaada mkubwa katika familia yake na hata kwa jirani zao.

JIRANI YAKE

Maryam Salum mkaazi wa Mabaoni Chake chake, ambae pia nayeye anaeishi na VVU anasema kiukweli Maryam Said baada tu familia yake ilipogundua kwamba ana VVU ilimtelekeza.

‘’Maryam alikua akiishi kwa shida na  mateso, ambapo hata sisi jirani zake, tulikua tunamuonea huruma.

Anasema anadhani kwamba hali hiyo ilikua ikifanyika kwa kutokana na jamii kwamba, ilikua haijaelimishwa, juu ya masuala hayo, kwani ilikua hayajajulikana kama hivi sasa.

Anaeleza  yeye alipogundulika kwamba anaugonjwa wa Ukimwi ilikua tayari wameshakupata elimu hakukumbana na vikwazo kihivyo.

Jirani mwengine ni (Omar ambae sio jina lake halisi) anakiri kwamba maryam mwanzo alipogundulika na Viruzi vya UKIMWI, alikua akiishi kwenye mashaka, kwani familia yake na hata majirani wote walimsusia.

‘’Ijapokua alikua ni mtu hodarai kwa wenzake, lakini  hatukuliona hilo sote tulimtenga,  na hiyo ni kutokana na kwamba elimu juu ya masuala ya ukimwi ilikua bado hayajakuwepo,’’anaeleza.

MUME WAKE

Sabri Issa anasema ni kweli amemuoa mke wake huyo ambae anaishi na VIRUSI vya Ukimwi, ambapo tayari wameshapata watoto watatu na wakiwa salama.

Anasema wanaume wasiwakatae wanawake ambao wanaishi na VVU, kwani endapo watafuata ushauri wa wataalamu wa afya, wanaweza kuishi kwa furaha na amani na bila ya kuambukizana.

‘’Nimemuoa Maryam akiwa na maambukizi na tumeshazaa watoto watatu  na wala hatuna maambukizi tuko salama,’’anaeleza.

Anasema amekua akiangalia afya kila baada ya miezi mitatu, na kwa mara ya mwisho alikwenda  mwezi  wa  nne  mwaka huu.

Pia anaeleza kwamba amekua akitumia dawa kinga zinazoitwa PREEP, ambazo  hutumika kwa mtu ambae hana mambukizi, ambao wako katika hali rizki.

MTAALAMU WA AFYA

Dokta Rahila Salum Omar ambae ni msimamizi wa vituo vya kutoa huduma kwa watu wenye ‘VVU’ anasema,  kiutalamu ni kweli  mtu mwenye Virusi vya UKIMWI anaweza kuoa au kuolewa  na ambae hana virusi, na wakaishi salama wao na kizazi chao.

Anasema sio vizuri watu kuvunja familia zao  wala ndoa zao ikitokezea mmoja, wanaotaka kuoana,  kwa sababu mmoja wao amegundulika na mambukizi, na kuvunjika.

‘’Kiutaalamu ni kweli kwamba mtu mwenye VVU anaweza kuoa au kuolewa na alie kua hana na wala wasiambukizane na maisha kuendelea, kama alivyo Maryam’’,anaweka wazi.


Mkakati wa kimataifa wa shirika la Afya dunia (WHO) wa VVU, (2022 hadi mwaka 2030), imelenga kutokomeza ukimwi ifikapo 2030.

Zanzibar  inatekeleza  mkakati  huo kwa kuitika mwito  wa kimkakati  wa 95  tatu  ifikapo  2030. Mkakati huu  unalenga juhudi za mapambano  za kuifikia  dhamira hii ifikapo  2030.

 Asilimia  95 ya  wazanzibari ifikapo  2030  wanatambua afya zao ( wanaishi  ama hawaishi na maambukizo  ya VVU, asilimia 95  ya  wanaoishi na  VVU  wawe  wanatumia  dawa za kupunguza makali  ya  VVU  ifikapo 2030.

Na asilimia  95  ya  wanaotumia dawa  za  kupunguza makali ya  VVU  virusi  viwe vimefubazwa (  Havina madhara ya kuambukiza sana, kusababisha magonjwa nyemelezi ,ama kuongeza kinga ya mwili ).

Tanzania inadhamira ya dhati ya kukomesha janga la VVU iliyowekwa katika ngazi ya kimataifa ndani ya mfumo wa malengo endelevu ya maendeleo (SDGs).

Kwa mujibu wa Tathmini iliyofanyika Dicemba 1 2023, Takwimu nchini Kenya zinaonesha nchi hiyo inashika nafasi ya saba kwenye orodha ya mataifa yenye idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI duniani, huku Rwanda na Tanzania zikitaja kufanikia kudhibiti maambukizo.

MWISHO

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO