WANAWAKE WATAKIWA KUSHIRIKIANA ILI WAWEZE KUJILETEA MABADILIKO

Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,  Mama Zainab Kombo Shaib, ametoa wito kwa wanawake nchini kushikamana ili kuweza kujikomboa kutokana na ukubwa wa wimbi la changamoto zinazowakabili 

 Mama Zainab ametoa wito huo huko, Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba, wakati  akizungumza  na akinamama wa ACT-Wazalendo wa Mikoa miwili kichama, ya Wete na Micheweni kisiwani humo.

 Alisema ukombozi wa mwanamke ni sawa na ukombozi wa jamii yote na njia ya matumaini kuelekea maendeleo ya Taifa zima

 Alifahamisha kuwa matumaini na mafanikio ya ukombozi wa kweli wa mwanamke hayawezi kufikiwa pindipo akinamama wenyewe watashindwa kujitambua, kushikamana na kusaidiana.

 "Wanawake ni wengi, na  nguvu yetu ni kubwa sana, tukiungana,tukishirikiana pamoja tukaacha makundi na kuchukiana tutafika mbali na tutalisaidia taifa katika kufikia ukombozi" alieleza Mama Zainab.

 Mama Zainab aliwataka wanachama hao kuendeleza uwajibikaji katika shughuli za chama ili kuisimamisha dhamira ya Uzalendo.

 Aidha Mama Zainab alisema amejitolea kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kuwasaidia watoto yatima na wenye  ulemavu , kwani kufanya hivyo ni wajibu wa kila mwanajamii sambamba na kuwataka wazazi kutokuwaficha watoto wenye ulemavu kwani nao wanahaki ya kuishi nakupata huduma za kijamii kama wengine.

 Katika kikao hicho wanawake 50 wamechukua kadi kwa niaba ya wenzao 350 na kujiunga rasmi na chama hicho, sambamba na kurejesha kadi 20 za Chama cha CUF.

 Mama Zainab aliwasihi wanawake hao kuendelea kuiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa na kuwaahidi kwamba Makamu wa kwanza wa Rais, kwa kushirikiana na serikali wapo katika mipango madhubuti ya kuitafuta haki ya wahanga wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Bi. Awena Sinani Masoud, mke wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Marehemu Maalim Seif  Sharif Hamad, alisema binafsi anamuunga mkono Mhe.Othman Masoud, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, na kusema anamatumaini makubwa kwamba ataifikisha Zanzibar katika hadhi yake.

 "Uwezo mkubwa  alionao Mhe. Othman unanipa faraja sana kwamba anaweza kuendeleza hatua alipofika Maalim Seif" alieleza 

 Aidha aliwaasa wanachama wa ACT jimbo la Konde kuingia katika uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika tarehe 9 Oktoba, kwa njia za amani na ustaarabu, sambamba na kuwaonesha umuhimu wa kushinda uchaguzi huo.

 Akitoa salamu za Wanawake wa chama hicho wa kisiwani Pemba mratibu wa wanawake Bi.Mkunga Hamad Sadala alisema, wanawake wa kisiwa cha Pemba wataendelea kumpa ushirikiano Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye pia ni Mjumbe wa kamati kuu ya Chama hicho


.Baada ya kikao hicho Mama zainab alipata fursa ya kukutana na watoto yatima na wenye  Ulemavu  wa Shehia ya Kinyasini na Mtemani za Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.






MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, ametoa wito kwa mamlaka zote pamoja na asasi za kiraia, kuimarisha afya ya mama na mtoto, ili kujenga ustawi bora wa jamii, utakaochangia maendeleo ya nchi.

 

Mama Zainab ameyasema hayo leo katika ziara yake, alipotembelea Hospitali ya Vitongoji, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

 

Amesema afya ya mama na mtoto ni sehemu muhimu ya msingi wa ustawi wa jamii, unaolenga kuzalisha na kuendeleza nguvu kazi ya Taifa, na hatimaye kufanikisha juhudi za kujiletea maendeleo.

 

"Afya zikiwa vizuri hata uzalishaji unaongezeka, hivyo ni vyema kuzitumia rasilimali tulizonazo kwa uangalifu katika kutoa huduma bora za kijamii ambazo ni pamoja na afya ya mama na mtoto," amesema Mama Zainab. 

 

Akitoa nasaha zake mbele ya madaktari na wahudumu wa hospitali hiyo, Mama Zainab ameahidi kupaza sauti kwa wadau wa afya ili kusaidia kuzitatua changamoto, zikiwemo za uhaba wa vifaa, hasa katika wodi ya akinamama wajawazito na sehemu ya kujifungulia.

 

Aidha ametoa wito kwa madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kuendelea kuchukua tahadhari na kuwaelimisha watu juu ya athari za mripuko wa janga la CORONA.

 

Naye Daktari dhamana wa Hospitali ya Vitongoji, Dokta Sharif Khatib ameeleza shukran zake za dhati kwa kufanikiwa kupata kifaa kipya cha kupimia damu na utambuzi wa maradhi mbali mbali cha ‘HAEMATOLOGICAL ANALYZER’, kitakachosaidia ufanisi wa huduma za hospitali hiyo kwa wananchi.

 

Mama Zainab ambaye ameambatana na Bi. Awena Masoud Sanani, Mke wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, katika ziara yake kisiwani Pemba, ametembelea maeneo mbali mbali yakiwemo Jengo la Bohari ya Dawa la Vitongoji, kabla ya kuelekea Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

 

Katika ziara hiyo, Bi Zainab ameongoza zoezi la kuwapatia misaada mbali mbali wagojwa na watu wasiojiweza, ikiwemo sabuni, pempasi, mipira ya kusaidia kujifungua kwa akina mama pamoja na mashuka ya vitanda vya hospitali.

 

Akikabidhi vifaa hivyo Mama Zainab ametoa wito kwa wananchi kujitokeza katika kusaidia, ijapokuwa kwa kiasi kidogo, ili kuwapatia unafuu wanyonge na kuwatatulia changamoto zinazowakabili.

 

Akitoa salamu za wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Bi Mgeni Khatib Yahya amesifia juhudi za utendaji mzuri zinazotekelezwa na wahudumu wa Hospitali ya Micheweni, licha ya changamoto ya kuhudumia idadi kubwa ya wananchi kila siku.

 

Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na wauguzi wa Hospitali hiyo iliyopanda daraja hadi Hospitali ya Wilaya kuanzia Agosti 30 mwaka huu, ili pia kusaidia kufanikisha malengo ya Serikali.

 

Naye Afisa Mdhamini wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Bw. Yakoub Mohd Shoka amesema ujio wa Mama Zainab katika ziara hiyo ni faraja kubwa, huku akitoa wito kwa viongozi wengine kufuata nyayo zake katika kuimarisha na kuendeleza Sekta ya Afya.

 

 

*Kitengo cha Habari* 

*Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar*

04/10/2021

ReplyForward

 

 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.