WANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUEPUKA HABARI ZA UDANGANYIFU
WAANDISHI
wa habari wametakiwa kufuata maadili wakati wanapotekeleza majukumu yao
sambamba na kuandika habari zenye ukweli, zenye kulinda haki, heshima na utu wa
binadamu, hasa katika kipinidi hiki cha kuelekea Uchaguzi mkuu wa Octoba
mwakahuu.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu
Zanzibar Khatib Mwinchande wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi
wa habari kuhusu, uzingatiwaji wa haki za Binadamu na Misingi ya Utawala bora
katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi
hiyo Chake Chake Kusini Pemba.
Alisema, ni vyema waandishi wa habari kufuata miiko na
maadili yao wakati wanapotekeleza kazi zao, hasa katika kipindi hiki cha
uchaguzi mkuu wa Octoba 2025.
Alifafanua, waandishi wa habari ni wadau muhimu wanaopaswa kuzingatia
utekelezaji wa Sheria, kwani kufanya hivyo kutawasaidia kufanyakazi za ukweli, zenye
kulinda haki na utu wa binadamu.
Alisema, suala la uchaguzi ni mchakato muhimu katika Nchi,
inayozingatia Misingi ya Demokrasia, uhuru, haki na amani, hivyo ni wajibu kwa
waandishi wa habari kuandika habari zenye ukweli na zenye kulinda haki za
wananchi, ili kuona kwamba wanajitokeza kwa wingi katika haki yao ya kikatiba
bila hofu.
‘’Waandishi wa habari andikeni habari zenye kuzingatia haki
za binadamu na misingi ya utawala bora, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi
mkuu, ili wajitokeze kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka,’’alisema.
Alisema, waandishi wa habari ni wadau muhimu wanaoweza
kulinda haki za binadamu na amani ya Nchi, hivyo ni budi kuepuka kuandika
habari zenye kuleta migongano, jambo
linaloweza kusababisha vurugu na kuondolewa kwa haki, utu na heshima za wanadamu.
Alisema, kwa kuzingatia Ibara ya 130 (1) (a) ya Katiba ya
Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na kifungu cha 6 (1),
(a), (b) vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora sura ya 391.
Na kifungu cha 8 cha Sheria nambari 12 ya mwaka 2003, Sheria
za Zanzibar, Tume ya Haki za Binadamu inajukumu la kuhamasisha hifadhi za haki
ya binadamu, wajibu wa jamii na kutoa elimu kwa umma juu ya haki za binadamu.
Alifahamisha, ili uchaguzi ufanyike kwa uhuru na amani ni
lazima kuzingatiwa haki, misingi na heshima ya haki za binadamu, hivyo ni vyema
waandishi wa habari kupatiwa elimu, ili kuhakikisha kwamba heshima za watu
hazikiukwi kwa kisingizio cha uchaguzi.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi kutoka Tume ya Haki za
Binadamu Ofisi ya Pemba Suleiman Salum Ahmad alisema, lengo la mafunzo hayo ni
kuwakumbusha waandishi wa habari, kuwa waadilifu na wazalendo wa hali ya juu,
ili kuibakisha nchi katika hali ya amani na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
‘’Katika kipindi cha uchaguzi kumekuwa kukijitokeza vitendo
vingi ambavyo haviendani na maadili na misingi ya kibinadamu, hivyo waandishi
tuweni makini, ili habari zetu ziwe ni zenye kulinda na kuheshimu silka na
desturi za nchi yetu ili kuepusha maafa,’’ alifahamisha.
Akiwasilisha mada ya Haki na Wajibu wa Waandishi wa habari
wakati wa uchaguzi, Mchunguzi Msaidizi Mwandamizi kutoka Tume hiyo Makaruru
Nyarancha, alisema Tume ya Haki za Binadamu imekuja na mafunzo hayo ili kuona
wanatoa habari za msingi, ambazo wananchi watapata kufahamu haki na wajibu wao.
Alisema, kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ya haki za kiraia
na haki za kisiasa ya mwaka 1966 kifungu cha 25, kila raia ana haki ya kupiga
kura na kuchaguliwa katika uchaguzi wa kweli, wa haki na wa mara kwa mara,
uliofanywa kwa kura ya siri na kuhakikisha uhuru wa wapiga kura.
Kwa upande wake Mratibu wa Habari Maelezo Pemba Jamila
Abdala Salim aliwataka wandishi wa habari kuyatumia mafunzo hayo, ili waandike
habari zenye migogoro na zenye kuepusha kuvunjwa kwa haki za binadamu.
Nao waandishi waliopatiwa mafunzo hayo wameahidi kuyatumia
vyema na kuhakikisha wanafuata miiko na maadili ya kazi yao, ili kuibakisha nchi
katika hali yake amani kwa wakati wote wa uchaguzi na baada.


Comments
Post a Comment