Mfahamu Joahari, binti mwenye ndoto ya kua kiongozi
NA FATMA HAMAD- PEMBA
Kuwapa nafasi wasichana katika mijadala ya kisiasa, vikundi vya uongozi shuleni na vyuoni, , kunawajengea ujasiri wa kushiriki kwenye michakato ya kisiasa mapema na wakiwa na taarifa sahihi.
Hili linasaidia kuvunja mila na desturi zinazoweza kuzuia wanawake kushiriki nafasi za uongozi kwa kiwango kikubwa.
Kwa kuanzisha ushiriki wao mapema, tunaunda kizazi cha wanawake wenye ujasiri na maarifa, ambao watakuwa tayari kuwania nafasi za uongozi na kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi kwa maslahi ya jamii nzima.
Hii pia inaongeza uwezekano wa kuwa na ushawishi mkubwa zaidi wa kisera kuhusu masuala yanayohusu wanawake na vijana.
Makala hii imezungumza na Johari Ibrahim Mbarouk ambae ni Rais wa Skuli ya Msingi Kiungoni Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambae ana ndoto za kuwa rais wa Zanzibar.
Johari Ibrahim Mbarouk (13) ni miongoni mwa vijana wa kike wenye ndoto ya za kufikia mbalikwenye masuala ya uongozi.
Kwa sasa anasoma darasa la saba Skuli ya msingi Kiungoni Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akiwa Skulini hapo binti huyo anaitumikia nafasi yake ya Urais katika Serikali ya wanafunzi.
‘’Ukiwa na malengo Fulani katika maisha ni lazima kutakua na vitu vingi vizuri ambapo utakua na hamu ya kuvifikia, lakini ikiwa sio kiongozi sio rahisi,’’ anasema Johari.
Skuli ya msingi ya kiungoni ambayo ina jumla ya wanafunzi 1554, wakiwemo wanaume 840 na wanawake ni 714, huku serikali ya wanafunzi ikiwa na viongozi 24, wakiwemo wanawake 15 na wanaume 9, walimu 27, wanawake 16 na wanaume 11.
Kilichomshawishi Johari kugombea uongozi ni kutokana na malengo yake aliyojiwekea katika maisha yake, na kuamini kuwa atakapokua kiongozi ataweza kuyatimiza kwa haraka malengo yake.
‘’Uongozi upo kwenye damu yangu, hivyo nikaona na mimi niombee ili nipate nafasi ya kutatua shida zinazotukabili skulini petu,na pia nitajijengea uthubutu na ujasiri popote nitakapokwenda,’’anasema wakati akiwa skuli.
Anasema atakapomaliza kusoma elimu ya lazima pamoja na Chuo kikuu, anatarajia kujiingiza kwenye harakati za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Lengo lake ni kuhakikisha anaingia kwenye nafazi za maamuzi ili aweze kutetea shida zinazowakwaza wanawake sambamba na kuleta mabadiliko katika jamii.
USHIRIKIANO KUTOKA KWA WAZAZI WAKE
Mama mzazi wa mwanafunzi Johari Zalha Ali Omar anasema walipopata tarifa kwamba mtoto wao anagombea Urais wa skuli, hawakumkatalia bali walimpa mashirikiano ili aweze kutimiza malengo yake.
‘’Kama wazazi wake tulimpa mashirikiano mtoto wetu, kwani uongozi ni kitu ambacho amekipenda na nilipoambia kama amefanikiwa kuwa Rais wa Skuli nilifurahi sana’’ anasema mama wa Johari
Nguvu ya kushinda ya Johari kwenye ngazi ya uongozi kwa Johari inatokana pia kwa baba yake Ibrahim Mbarouk, anasema walimuandaa tokea awali kwa malezi mazuri mtoto wao, kwani walishamuona kuwa anandoto za kufika mbali.
‘’Kwa vile alikua na ndoto za kufika mbali ili aweze kuja kuwa mkombozi kwa familia yake ni lazima apambane licha ya nafasi hiyo aliyochaguliwa hapo Skuli,’’anaelezababa wa Johari.
Baba huyo ameongeza kuwa kuwazarau wanawake na kusema kuwa, hawafai kuwa viongozi sio jambo zuri kwani nawao wakiwezeshwa wanaweza na wanaweza kuleta mabadiliko katika nafasi zao.
MAENDELEO YA ELIMU
Mwalimumkuu skuli ya Kiungoni Msingi Hamad Omar Issa anasema Johari ni mwanafunzi ambae anapenda masomo yake na hufaulu vizuri katika mitihani, kuwa kiongozi si kikwazo kwake kufeli mitihani yake.
‘’serikali ya wanafunzi inawandaa watoto kuwa viongozi wazuri wa badae na kuwajengea uthubutu, kujiamini hususani wanawake kwani kwa kipindi kikubwa wameachwa nyuma katika masuala ya uongozi,’’anaeleza.
Anaeleza Johari ni mwanafunzi hodari mwenye heshima na mwenye bidii hana nidhamu ya woga anaweza kusimama popote akazungumga, amewaunganisha walimu na anafunzi na kuwa kitu kimoja.
Mwalimu wa Serikali ya wanafunzi wa skuli ya msingi kiungoni Ali Said Ali anasema wamekua na kawaida ya kuwanda watoto ambao wanaonekana wanauwezo wa kuwa viongozi, tokea wanapokuepo Chekechea.
‘’Tukimgundua tu mtoto kama ana uwezo wa kuwa kiongozi, na ana ndoto za kufikambali, basi tunamuundaa ili aje awe kiongozi mzuri wa hapo baadae na aweze kuleta mabadiliko chanya katika Tifa lake,’’anafafanua
Anasema uongozi umemsaidia Johari pamoja na wanafunzi wenzake kuongezeka kwa ufaulu katika masomo yao.
Mwanafunzi Time Ali Hemed anasema kuwa tokea zamani Johari alikua ana kipaji cha kuzungumza hakua na woga, hivyo kupata nafasi hiyo kutamsaidia kukuza kipaji chake.
‘’Kila kitu kina mwanzo wake hivyo naamini kwamba kuwepo katika serikali ya wanafunzi kutamfanya ajiamini zaidi na mwisho wa siku atagombea nafasi nyengine za uongozi kama vile majimboni,’’anafahamisha.
WANAOMFAHAMU JOHARI
Kwa upande wake Asha Omari (ambae sio jina lake halisi) ni jirani wa Johari anasema mtoto huyo anawapenda wazazi wake na anawashughulikia wadogo zake, hivyo waliposikia amepata uongozi hawakushangaa.
‘’Johari muonekano wake tu basi unakuambia kwamba anafaa kua kiongozi kwani anaweza kuzungumza na anajiamini,’’anaeleza Asha.
SAFARI NA NDOTO
Waliniambia nisisikilize maneno ya watu, bali ninachostahili kufanya nikufanya kilicho chema, muhimu nifanye wajibu wangu ninavyotakiwa, kwa kufuuata maadili mema,’’anasema Johari.
Wito wake kwa watoto wenzake anawashauri kuwa kuingia katika uongozi sio kujitafutia kufeli masomo, bali ni kuanza kujitengenezea maisha mazuri ya badae, hivyo wasiogope wanapaswa kuamua tu kwani wanaweza.
‘’Nawashauri wajiingize kwenye uongozi kwani ni moja ya njia ambayo itawasaidia katika kazi zao na hata kwenye maisha yao, anamalizia Johari.
VIONGOZI WA SERIKAL
Afisa elimu Sekondari Mkoa wa Kusini Pemba Mohamed Shamte Omar anasema serikali imeweka muongozo maalumu ambao unaruhusu uwepo wa serikali za wanafunzi maskulini.
Anasema takribani skulinyingi ambazo zinaongozwa na viongozi wanawake, ndizo zinazofanya vizuri zaidi, kwani wanawake wanakua karibu na walimu na wanafunzi.
Comments
Post a Comment