Masheha watakiwa kuwashirikisha wanawake kwenye kamati zao

 

NA FATMA HAMAD, PEMBA

Sheha wa Sizini Suleiman Shaame Hamad, amewataka masheha wenzake kuhakikisha wanazingatia suala la usawa wa kijinsia katika Kamati zao, ili kuona wanawake nawao wanapata fursa kupitia kamati hizo.

Sheha huyo ametoa wito huo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko kijijini kwake Sizini, amesema ni wakati sasa kwa masheha kuhakikisha wanatekeleza dhana ya Jinsia kwa kuwashirikisha wanawake katika Kamati zao, kwani kutawapa fursa ya kujiamini, na kua viongozi wazuri wa badae.

Amesema unapompa nafasi yoyote mwanamke ni rahisi,  kufanikiwa, kwani wao ni wachapakazi na ni washauri wazuri hasa katika nyanja za maendeleo.

‘’Binafsi nimeona nilipowashirikisha wanawake katika kamati yangu, maendeleo yamepatikana, ukilinganisha na hapo nyuma,’’amesema.

Amesema miongoni mwa faida ambazo amezipata baada ya kuwashirikisha wanawake katika Kamati yake, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kwani ameanzisha shughuli za uhifadhi wa Mikoko, na viumbe wa baharini.

‘’Tokea tuanze kuhifadhi Mikoko tumefanikiwa, kwani tumepunguza Maji ya Chumvi kuingia katika vipando vya wakulima, ambapo msimamizi mkuu wa shughuli  hizo ni wanawake,’’ameeleza.

Amefahamisha kuwa,  kamati yake ina wajummbe 10, wanawake na wanaume wakiwa idadi sawa.

Time Juma Hamad mwanakamati hiyo ya Sizini  amesema licha ya kamati yao kuwa na wajumbe wengi wanawake lakini haijawahi kupoteza kitu.

Amesema zamani kamati ilipokua na wajumbe wengi wanaume ilikua na matatizo mengi ikiwemo udhalilishaji ukilinganisha na sasa.

Omar Hamad ambae pia ni mwanakamati wa Shehia hiyo ya Sizini amesema mwanamke sikuzote ndio mchapakazi nzuri kuliko hata mwanamme.

Amina Ahmed Mohamed  kutoka Chama cha wandishi wa habari wanawake Tanzania Zanzibar –TAMWA Ofisi ya Pemba,  amesema licha ya kuwa hawana utafiti rasmi lakini bado Sera ya Maendeleo ya Jamii na Jinsia, haijatekelezeka ipasavyo.

Ameleza kuwa wanatamani Sera yengetekelezwa, kwani siku zote wanawake ni wapenda amani, wapenda maendeleo na waadilifu kwenye uongozi.

  ‘’Hata tukiangalia kwenye ngazi za shehia idadi ya masheha wanawake ni kidogo kwani ni 81 sawa na asilimi 20 kwenye shehia 388 ya masheha wote Zanzibar,’’amesema.

Mwanaisha Ali Masoud Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto Pemba amesema utekelezwaji wa Sera unahitajika kuanzia hata kwenye ngazi ya familia.

‘’Tunataka kwamba kila alipo mwanamme na mwanamke awepo kwani shida za wanawake anazijua mwanamke,’’ameleza.




 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO

‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’