Wandishi wa habari watakiwa kuielimisha jamii juu ya mabadiliko ya tabianchi
NA FATMA HAMAD, PEMBA
AFISA ELIMU kutoka Idara ya Mazingira Ofisi ya Pemba Nassor Ali Salim, amesema endapo kama, hakutochukuliwa hatua za makusudi za kukabiliana na athari zinazotokana na Mabadiliko ya Tabianchi, baada ya miaka 100 kisiwa cha Pemba kitabakia historia, kutokana na maji ya bahari kuingia Nchi kavu.
Alisema kufuatia tatizo hilo la Majichumvi kuingia katika Nchikavu, kunauwezekano mkubwa wa kupoteza Kilomita za mraba 286, sawa na asilimia 28 ya eneo lote la Pemba.
Alisema watu wanaongezeka na Ardhi inaendelea kupungua, hivyo endapo kama hakutochukuliwa jitihada za ziada, juu ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kisiwa cha Pemba kitakua kiko hatarini zaid, na watu wanaweza kuja kukosa maeneo ya kuishi.
Alisema yapo maeneo yasiyopungua 123 yakiwemo makaazi ya watu pamoja na mashamba yanayotumika kwa ajili ya kilimo, yameathirika kutokana na uingiaji wa majichumvi.
‘’Tuna maeneo mengi yameathiwa na mabadiliko ya Tabianchi kama vile Kojani, Mjini kiuyu, Mkoani pamoja na Micheweni na hayawezi kutumika kwa sasa,’’alisema.
Afisa huyo aliyasema hayo wakati akizungumza na wandishi wa habari katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuandika habari za utetezi juu ya masuala ya mabadiliko ya Tabianchi, yaliofanyika Ofisi za Chama cha wandishi wa habari wanawake TAMWA Zanzibar, zilizopo Mkanjuni wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema kufuatia tatizo hilo ambalolimeonekana kua ni tishio kwa wakaazi wa kisiwa cha Pemba, ipo haja kwa wandishi wa habari kuielimisha Jamii, kwani kutapelekea kuzifahamu athari za mabadiliko ya tabianchi na kuchukua tahadhari mapema.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kutoka Chama cha wandishi wa habari wanawake TAMWA Zanzibar, Sofia Ngalapi alisema kufuatia tatizo hilo wameamua kuleta mradi wa kuwawezesha wanawake kutunza mazingira, kwa ushirikiano wao na Jumuia ya Uhifadhi wa misitu Pemba CFP na Jumuia ya uhifadhi wa misitu CFI kutoka Canada ili kujiinua kiuchumi na kuepukana na athari hizo.
Alisema wanawake wamekua ndio wathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi kwani, wao ndio wanaotumia muda mkubwa kuingia maporini na kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia.
‘’Bado wanawake wanaachwa nyuma juu ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi, kwani hawana maeneo ya kuhifadhia, waweze kuepukana na athari hizo’’,.alisema.
Alisema ni vyema kwa wandishi wa habari kuielimisha Jamii kuwapa fursa wanawake waweze kufanya shughuli za utunzaji wa mazingira, ili waweze kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Nae Sada Juma Segenya mtetezi wa masuala ya wanawake kutoka Jumuia ya Uhifadhi wa misitu kisiwani Pemba CFP, alisema moja ya changamoto inayowakabili katika mradi huo ni baadhi ya wanawake kukosa rasilimali Ardhi, kwa ajili ya kufanyia shughuli hizo za uhifadhi.
Kwa upande wao wandishi wa habari ambao walipatiwa mafunzo hayo, walisema watahakikisha wanawaelimisha wananjamii kufahamu athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kuwaungamkono wanawake juu ya uhifadhi wa mazingira.
Uchunguzi wa hali mwaka inaonesha kuwa idadi ya watu wanaoenda Mahkamani kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi inaongezeka.
Hadi kufikia Disemba mwaka 2022, kumekuwa na kesi 2,180 zinazohusiana na mazingira, zilizowasilishwa kwa taasisi za Sheria 65 kote duniani.
Ripoti ya Benki ya Dunia inasisitiza umuhimu wa kuunganisha masuala ya tabianchi katika mipango ya maendeleo ya Tanzania kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ambapo moja ya mkakati wa ripoti hiyo ni kusaidia jamii zilizohatarini, kuwa na uwezo wa kuhimili mishituko ya tabianchi.
Pia ripoti hiyo imeeleza kuwa kushindwa kuchukuliwa hatua za mabadiliko ya tabianchi, kunaweza kupunguza ukuaji wa uchumi wa Tanzania, kwa asilimia nne ifikapo mwaka 2050.
Aidha kunaweza kusababisha watu Milioni 20.6 kuingia kwenye umasikini, na wengine Milioni 13 kulazimika kuhama makazi yao Nchini.
Comments
Post a Comment