UTELEKEZWAJI WA WANAWAKE UNAVYOCHANGIA KUONGEZEKA KWA UDHALILISHAJI

 
 NA FATMA HAMAD,PEMBA

Utelekezwaji wa Wanawake na Watoto imedaiwa ni moja ya sababu inayo changia kutokea kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia  ikiwemo kubakwa, kulawitiwa, kwa watoto.

Hayo yamesemwa na hakimu wa Mahakama maalumu ya kupambana na Udhalilishaji iliyopo Wete, Muumin Ali Juma wakati akizungumza na Wananchi katika mkutano malumu wa kuwaelimisha Wananchi umuhimu wa kuripoti na kutoa ushahidi Mahakamani huko Chamboni wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema wilaya ya Micheweni ni moja  ya wilaya inayongoza kwa utelekezaji wa wanawake, katika mkoa wa Kaskazini Pemba  jambo ambalo  linachangia  watoto kudhalilishwa.

,,Unamuacha mwanamke na watoto humpi huduma yoyote jee umetegemea nini, niwaulize wanaume wenzangu kesho mbele ya Mungu tutakwenda kujibu nini,aliuliza.

Alisema  mara nyingi kesi  zinazofikishwa mahakamani  za waliofanyiwa udhalilishaji ni watoto ambao wamekosa malezi ya pamoja kati ya Baba na Mama, hivyo aliwataka wananchi hao kuwa na ustahamilivu katika ndoa zao ili waweze kuzilea familia zao, ambapo itakuwa ni muwarubaini wa vitendo hivyo.

 Kwa upande wake Asya Soud Mzee kutoka dawati la Polisi Micheweni aliwashauri Wananchi hao kuwapeleka vyombo vya sheria watoto wanapodhalilishwa ili waweze kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa tiba.

‘’Mtoto akishakudhalilishwa musifiche ripotini Vituoni,kwani mkija nao tunawachunguza na tunawapa dawa za kinga ili kama huyo aliemfanyie kitendo kama anamaradhi asije akambukizwa na yeye,alisisitiza.

 Ali Khamis Faki ambae ni miongoni mwa walioshiriki mkutano huo alishauri Serikali kutoa adhabu kwa pande zote mbili baina ya mwanamme na mwanamke yoyote watakapokamatwa na kosa la udhalilishaji na sio kwa mwanamme pekee, jambo ambalo linaweza likapelekea kuondokana na udhalilishaji.

 Mkutano huo uliandaliwa na Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Micheweni [MIDIPAO] wakishirikiana na Idara ya Msaada wa Kisheria pamoja na Mahakama, ikiwa ni shamra shamra ya madhimisho ya siku ya sheria Duniani.


 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.