UJASIRIAMALI UNAVYOINUA WANAWAKE KIUCHUMI


 NA ZUHURA JUMA, PEMBA

 WAJASIRIAMALI wa kikundi cha mboga na matunda cha ‘Hufedheheki’ kilichopo Kwale Mpona Finya wamesema, wanafurahia uongozi wa Katibu wao Subira Mkubwa Mohamed namna anavyopigania katika kuhakikisha kikundi hicho kinapata maendeleo.

 Walisema kuwa, amekuwa akiwashirikisha hatua kwa hatua katika masuala yote ya kikundi, jambo ambalo linawapa faraja kwani wanakuwa na uhuru wa kutoa maoni yao na baadae kuyafanyi kazi kadiri anavyoweza.

 Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wanakikundi hao walisema, Katibu wao huyo anapambania kwa hali na mali kuhakikisha kikundi kinazalisha zaidi na kujipatia kipato kitakachowakwamua kimaisha.

 Mwanakikundi Khamis Ali Khamis alisema, mama huyo ni kiongozi mchapa kazi na mchakarikaji kiasi ambacho na wao hupata nguvu ya kuzalisha zaidi bidhaa zao kwa lengo la kujipatia mafanikio.

 Alisema, wamepata manufaa mengi kupitia kiongozi huyo mwanamke kutokana na kuwa anawahamasisha kufanya kazi kwa bidi, ili kuondokana na hali ngumu ya maisha, ambapo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji.

      "Tumejifunza vitu vingi kupitia Katibu wetu huyu kwa sababu anapambana kuhakikisha tunazalisha bidhaa nyingi na zenye ubora ili kukuza soko,” alifafanua.

Nae mwanakikundi Salma Said Salim alieleza kuwa, mama huyo anaweza kugombea nafasi yoyote ya uongozi na akaitumikia vizuri jamii yake, kutokana na utendaji kazi wake ulio bora.

 "Jinsi anavyosimama imara kutatua changamoto zetu za kikundi, naamini atakapoingia jimboni na kushinda, basi ataibua matatizo yaliyomo ndani ya jamii na kuyatafutia njia mbadala ya kuyatatua,” alisema.

 Alisema kuwa, kikundi chao kinajishughulisha na mazao ya mapesheni, mananasi, ndimu, maparachichi, mchicha, pilipili boga, nyanya chungu, ndizi na malimau, ambacho kilianzishwa mwaka 2000.

 Katibu wa kikundi hicho Subira Mkubwa Mohamed alisema, walihama mjini Wete na kwenda kuhamia kijiji cha Kwale Mpona Finya kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo.

 Alisema kuwa, kwa sasa wamepiga hatua nzuri kwani walianza na robo ekari na sasa wana ekari sita na nusu, ambapo ekari nne na nusu zimejaa mazao mbali mbali.

 Alisema malengo yao, ni kuhakikisha wanazalisha zaidi ili kujinufaisha wao na kuongeza ajira kwa vijana katika kijiji na familia zao.

 Akizungumzia soko kiongozi huyo alisema ni zuri, isipokuwa kama ilivyo kawaida bei ya mazao siku za mvua hushuka kwa vile idadi ya wateja wao ambao huwafuata shambani nayo hupungua.

 Alisema kuwa, changamoto inayowakabili ni kukosa mtaji kwani wanataka wazalishe zaidi, lakini wanashindwa kutokana na kukosa fedha za kujiendeleza.

 ‘’Tumeshaomba mkopo lakini bado hatujapewa, ingawa tunatumai kwamba tutapata, huu utatusaidia kutatua changamoto zinazotukabili,’’ alisema mama huyo.

 Aliwaomba viongozi wa Serikali wafike kwenye shamba lao kukagua shughuli zao na kuona jinsi walivyoimarisha, ili wapatiwe mkopo utaowasaidia kujiendeleza.


 Kaimu Mratibu Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Pemba Haji Mohamed Haji alisema, ombi la mkopo la wakulima wa mboga na matunda Kwale Mpona lipo katika utaratibu na baada ya kumaliza watapatiwa.

 "Mkopo watapewa, lakini maombi ni mengi na wao wakati wanapeleka waliwakuta wenzao, hivyo mpaka wapewe aliowakuta ndipo na yeya apewe,’’ alieleza.

 Aliwataka wanakikundi hao kuwa wavumilivu kwani itakapofika zamu yao watapewa, kwa sababu wao ni walipaji wazuri na wala hawana matatizo yeyote katika urejeshaji wa fedha.

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.