RUSHWA MUHALI YATAJWA NI CHANZO CHA KUONGEZEKA KWA UDHALILISHAJI

 
 

                                              NA FATMA HAMAD, PEMBA

RUSHWA muhali katika jamii bado ni kilio kikubwa kinachosababisha kesi za udhalilishaji kushindwa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kupata hatia.

Akizungumza katika kikao maalumu, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Dk. Mzuri Ali Issa amesema licha ya elimu inayotolewa kwenye jamii lakini bado suala la muhali halijaondoka, jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la udhalilishaji.

Alisema, bado jamii inaendelea na tabia ya kuzikalia kitako na kuzifanyia suluhu kesi za udhalilishaji, jambo ambalo linapelekea kuongezeka kwa matendo hayo siku hadi siku.

‘’Linapotokea tukio la udhalilishaji turipotini kwenye vyombo vya Sheria na sio  kusizifanyia suluhu, kwani kufanya hivyo tunazidi kupalilia udhalilishaji na kuwaumiza watoto wetu," alieleza.

Aidha Dk. Mzuri alisema, jambo jengine linalokwamisha ushahidi wa kesi mahakamani ni kukosekana kwa utumiaji wa ushahidi kwa njia ya kielektroniki, hali ambayo inaleta usumbufu kwa watoa ushahidi hasa kwa watoto na watu wenye ulemavu.

Sambamba na hilo, alivitaka vyombo vya Sheria kuongeza nguvu zaidi na kuwa makini kwenye suala la upelelezi wa kesi pamoja na kutumia vifaa vya teknolojia, ili kuhakikisha kwamba ushahidi unapatikana kwa haraka na mtuhumiwa kutiwa hatiani.

 

Kwa upande mwengine aliwataka Vijana kujishughukisha na shughuli mbali mbali ambazo zitawaletea maendeleo ikiwemo ujasiriamali, na sio kukaa katika vigenge viovu.

‘Jiepusheni  na vikundi viovu,fanyeni biashara hata kama ni kuza Karanga, alisema

 Kwa mujibu wa ripoti ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar ndani ya mwezi wa Novemba mwaka huu kumeripotiwa jumla ya matukio 172 ya udhalilishaji wa kijinsia, ambapo tukio moja tu ndilo lililofikishwa mahakamani kati ya matukio hayo yaliyoripotiwa.

 

              

 

 







 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.