NA ZUHURA JUMA, PEMBA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein
Ali Mwinyi amezitaka Halmashauri, Mabaraza ya Miji na Manispaa kudumisha usafi
katika miji, ili kuiweka katika mazingira bora na haiba ya kuvutia.
kizungumza wakati akifungua kituo cha wajasiriamali Kifumbikai
Wete pamoja na stendi ya Kinowe Konde Dk. Mwinyi aliziagiza taasisi hizo mambo
matano, ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika miji, kujenga masoko, vituo vya
ujasiriamali, maegesho na viwanja vya kufurahishia watoto ambayo hayo yatasaidia
kuweka mazingira bora na mazuri.
Alisema kuwa, usafi ni muhimu katika maisha ya mwanadamu, hivyo
ni wajibu wao kudumisha katika maeneo ya miji, kwa ajili ya kuweka mandhari
nzuri na ya kuvutia.
"Tumebadilisha ugatuzi ili taasisi hizi ziweze kufanya kazi
zake vizuri ikiwa ni pamoja na suala la kuimarisha usafi katika miji yetu,
hivyo mna wajibu wa kuyatekeleza kwa vitendo ili kuimarisha maisha ya
wananchi," alisema Rais Mwinyi.
Aidha Dk. Mwinyi alieleza kuwa, kituo hicho cha wajasiriamali
pamoja na stendi (maegesho) alizozifungua ni fursa muhimu ya kiuchumi kwa
wananchi ambayo watafanya biashara katika maeneo hayo na kujipatia fedha
zitakazowakwamua na maisha duni.
"Wakati nafanya kampeni wajasiriamali walitaka wapatiwe
mtaji, maeneo mazuri ya kufanya biashara zao na kodi nafuu, ambapo kwa miaka
mitatu ya awamu ya nane tayari imeshatekeleza hayo kwa kiasi kikubwa, kwani
jumla ya shilingi bilioni 31 zimetengwa kwa ajili ya kuwapatia mikopo
wajasiriamali bila ya riba kupitia benki ya CRDB," alifafanua.
Dk. Mwinyi aliagiza Mamlaka husika kutowatoza kodi miezi
mitatu kwa wajasiriamali ambao watakwenda kuuza bidhaa zao kwenye soko hilo,
huku akisisitiza kupewa kipao mbele katika suala la kupatiwa mikopo, ili
wajipatie mtaji utakaowasaidia katika shughuli zao za ujasiriamali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk
Khatib alisema kuwa, Dk. Mwinyi amefanya mambo makubwa ambayo yataimarisha
maisha ya wananchi na kupata maendeleo. "Tutayasimamia majengo haya na kudumisha usafi kwenye
vituo, masoko na maeneo mengine ya miji ili wafaidike wao na vizazi
vijavyo," alieleza Mkuu huyo.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za
Mitaa na Idara Maalumu za SMS Massoud Ali Mohamed alisema kuwa, Dk. Mwinyi
anatimiza ahadi zake kwa vitendo ambapo kwa miaka mitatu ya uongozi wake
ameshajenga vitu 25 kwa wilaya 11 za Zanzibar.
"Lengo la Rais kujenga vituo hivyo ni kuwainua wananchi
kiuchumi ili wawe na kipato kizuri kitakachowakwamua kimaisha na kupata
maendeleo endelevu, hivyo mengi yamefanyika katika sekta mbali mbali na
yanaendelea kufanyika," alifafanua Waziri huyo.
Mapema Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar na Mkuu wa
Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya walisema, wamepata faraja kuzinduliwa
kituo cha wajasiriamali na stendi kwani vitaimarisha maisha ya wananchi
kiuchumi.
Mapema wafanyabiashara wa kituo cha wajasiriamali Kifumbikai
Wete walisema kuwa wamefurahi sana kwani watajikwamua kimaisha na kuiomba
Serikali iwapunguzie kodi ili wanufaike zaidi.
Ujenzi wa kituo cha wajasiriamali kimegharimu zaidi ya shilingi
bilioni 1.5 huku stendi ya Kinowe Konde ikigharimu zaidi ya shilingi bilioni
1.4.
Comments
Post a Comment