WADAU WA HAKI ZA BINADAMU WATAKIWA KUONGEZA NGUVU KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA VITENDO VYA UDHALILISHAJI
NA SALIM HAMAD,PEMBA
MKURUGENZI wa Mashtaka
Zanzibar, Mgeni Jailan Jecha amesema bado kuna juhudi ndogo
zinazochukuliwa na wadau katika mapambano ya vitendo vya
udhalilishaji kwani baadhi yao huzisuluhisha kesi hizo
kienyeji jambo ambalo husababisha kesi hizo kupotea bila
ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema bado wapo baadhi ya watendaji hao hupatanisha kesi
hizo Kiuenyeji ili zisiende mahakamani jambo ambalo linakwamisha juhudi za
mapambano ya kesi hizo na kusababisha kuendelea kujitokeza Vitendo hivyo.
Mkurugenzi aliyasema hayo wakati akifungua
mafunzo elekezi juu ya kuchunguza na kuendesha kesi zinazohusiana na
udhalilishaji wa kijinsia kwa wadau wa mapambano juu ya kupinga vitendo
vya ukatili na udhalilishaji ikiwa ni pamoja na waendesha mashtaka, madaktari,Maafisa
na polisi huko katika ukumbi wa Makonyo Chake chake.
Alisema sababu nyengine ni jamii kutotilia maanani katika
mapambano ya vitendo vya udhalilishaji kwa kuona kuwa jukumu la mapambano hayo
ni la Serikali pekee ama Polisi na mahakama.
Alifahamisha kuwa ili vitendo vya udhalilishaji
viweze kuondoka ni vyema Kwa taasisi zinazoshughulikia kesi jinai ziweze
kupambana kwa pamoja huku wakiondoa ukakasi wa aina zote
katika kufuatilia kesi hizo.
'’Mapambano haya ili yaweze kufanikiwa lazima yawepo
mashirikiano ya pamoja kati ya taasisi husika na jamii Kwa kukataa ushawishi
wowote unaorejesha nyuma ikiwemo rushwa muhali"alisema.
Alieleza kuwa madaktari wana haja ya kujuwa ule utaratibu
mzima ikiwemo kutowa ushahidi Mahakamani hivyo ni lazima kupata mafunzo hayo
ili kuoondosha malalamiko yasiyo ya lazima.
Mapema Ofisa Mdhamini wizara ya Nchi Afisi Rais
Katiba ,Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Halima Khamis
Ali alisema ni lazima kuondokana na vikwazo vinavyokwamisha keshi za
udhalilishaji ikiwemo kutowa ushahidi wa kweli mahakamani ili haki uweze
kupatikana .
Alieleza kuwa ili taifa liweze kuwa imara na lenye ubora lazima
vyombo vinavyosimamia haki visiwe ndio kikwazo kinachokwamisha kesi hizo na
badala yake viwe na ushirikiano na kuweka mikakati ili nguvu za mapambano
ziweze kufanikiwa.
‘’Taasisi hizi za Mahkama Madaktari na Polisi Mmekuwa
mkilalamikiwa sana na jamii kwa kutokuwa na uadilifu na kuondosha Imani kwa
wananchi hivyo ni lazima mubadilike haki itendeke na asionewe mtu’’alisema.
Alisema Wadau hao kama watashirikiana ipasavyo Pamoja na
wananchi vitendo hivyo vitawza kupungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini na
kurejesha imani kwa wananchi.
Akitowa mada ya namna ya kumfanyia uchunguzi muhanga wa kesi ya
udhalilishaji Mkurugenzi tiba kutoka wizara ya afya Dk. Msafiri Ladislaus
Marijani alisema jukumu la daktari ni kumpa matibabu muhanga ili aweze kendelea
na Maisha pamoja na ukusanyaji wa ushahidi utakaosaidia mahakamani.
Alielekeza madaktari wanapompokea muhanga wa udhalilishaji
hakuna haja ya kuweka vikwazo na kupelekea kupoteza ushahidi badala yake
wafanye majukumu yao kama sheria inavyoelekeza.
‘’Madaktari na wao wanafasi kubwa katika kupambana na kesi hizo
kwa kutoa Ushahidi halali pale wanapofanya uchunguzi wa kitaalamu kutambua
mtuhumiwa wa vitendo hivyo ‘’alisema.
Comments
Post a Comment