*RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ongezeko la
watu duniani linachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mahitaji mbalimbali
ikiwemo maji.*
Amesema tatizo hilo
pia husababisha uhaba wa huduma na vifaa mijini na vijijini na kuchangia chachu
ya mabadiliko ya matumizi ya ardhi.
Dk. Mwinyi aliyasema
hayo hotel ya Verde Mtoni, mkoa wa Mjini Magharibi, alipofungua kongamano la 24
la maji lililoyashirikisha mataifa kutoka Mashariki na kusini mwa bara la
Afrika.
Alisema, hali hiyo
huibua maswala mengi yakiwemo kuzorota kwa vyanzo vya maji, uchafuzi wa
mazingira, upotevu wa viumbe hai na upotevu wa afya ya mazingira kwa
ujumla.
Alisema, ushahidi wa
hayo unaonyesha mazingira ya nchi nyingi za bara la Afrika yanabadilika
mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayohuhusishwa na
mabadiliko ya hali ya hewa husababisha ongezeko la hatari kutokana na hali
mbaya ya hewa.
Rais Dk. Mwinyi pia
alieleza, changamoto hizo zinahitaji usimamizi endelevu wa rasilimali za maji
ili kukidhi mahitaji ya sasa ya kiikolojia, kijamii na kiuchumi bila kuathiri
uwezo wa kukidhi mahitaji hayo kwa siku zijazo.
“Tunahitaji kuwa na
msimamo thabiti na kuendeleza mikakati ya kupata maji kwa ajili ya watu wetu,
uchumi wetu pamoja na mazingira” alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.
Alisema, kongamano
hilo limekuja wakati mwafaka wakati mataifa ya kusini mwa bara la Afrika
yakiendeleza mchakato wa kuharakisha mabadiliko kupitia mbinu za kibunifu na
utengamano kwa ajili ya usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kwenye mataifa
yao.
“Tunaamini
tunapobadilishana uzoefu na utaalamu baina yetu kupitia mkutano huu kutaleta
mawazo mapya na njia za kutumia vyema na kudhibiti maji au kuongeza maji
yanayopatikana sasa kupitia suluhu mbadala" alieleza Dk. Mwinyi.
Alisema, Zanzibar
ilianzisha mpango wa uwekezaji maji wa mwaka 2022 hadi 2027 uliolenga kukusanya
rasilimali kwa ajili ya uwekezaji wa usalama wa maji kwa ajili ya utekelezaji
na uendelevu wa muda mrefu wa usambazaji maji kwa mahitaji ya msingi na miradi
ya maji kwa mahitaji ya kiuchumi.
Rais Dk. Mwinyi
alisema pia mpango huo umezingatia maeneo matano yakiwemo uwekezaji wa maji na
fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira, Kujenga
uwezo wa kuhimili hali ya hewa, Usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa kijamii,
Kuimarisha utaratibu wa kitaasisi, pamoja na Uchumi wa bluu na usimamizi
endelevu wa rasilimali maji.
Halkadhalika, Rais Dk.
Mwinyi aliwakaribisha washirikiri na wageni wa kongamano hilo kutembelea
vivutio mbalimbali vya utalii vilivyomo nchini, akiwaeleza sifa za kisiwa
maarufu duninani kinachotamba na sifa ya marashi ya karafuu Zanzibar, kutokana
na kilimo na usindikaji wa viungo vyenye harufu nzuri za karafuu, manjano,
mdalasini, mchaichai, pilipili manga na hoho. Pia aliwataka wageni hao
kutembelea mashamba ya viungo ili kujifunza kuhusu mchakato na historia
wa mazao hayo.
Sambamba na kuwaeleza
vivutio vyengine vya utalii vinavyopatikana Zanzibar ukiwemo utamaduni,
mila na silka za kipekee kwenye maeneo ya kihistoria ya hifadhi ya mji Mkongwe
wa Zanzibar ambao ni urithi wa dunia, Fukwe zenye mchanga mweupe na maeneo
mengine ya hifadhi ya asili.
Kongamano hilo
limewaweka pamoja wataalamu wa kutunga sera, wasomi, watafiti na wadau wa
tasnia ya maji kwa lengo la kubadilishana ujuzi na uzoefu ili kuchunguza njia
sahihi za kushughulikia changamoto na matarajio ya kimsingi kwa sekta ya maji
kwa mataifa ya Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika.
Akizungumza kwenye
mkutano huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Omar Juma Kipanga, alipongeza juhudi zinazochukuiliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kukuza Sekta ya Maji kupitia uchumi wa
Buluu.
Naye, Naibu Waziri wa
Maji, Nishati na Madini, Zanzibar Shaaban Ali Othman alisema jitihada kubwa
zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaondolea
changamoto ya maji wananchi wake pamoja na kuhakikisha usalama wa maji safi unaendelea
kuatikana maeneo yote ya Zanzibar.
Naye Mwenyekiti wa
taasisi ya SADC “Water Net Trust” na Mtaalamu wa mazingira kutoka Namibia,
Prof. Nnenesi Kgabi, alieleza mkutano huo ni fursa muhimu ya kubadilishana
uzoefu na ushirikiano baina ya washiriki ambao unadumisha uhusiano uliopo baina
ya mataifa ya kusini mwa bara la Afrika.
Kongamano hilo la 24
la maji kwa lililokuwa na lengo la kuvumbua na kushirikiana kwa nia usimamizi
endelevu wa rasilimali maji Afrika, lilitoka kaulimbiu isemayo “Kuharakisha Mabadiliko,
Kukuza Ubunifu na Utengamano wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Maji kwa
mataifa ya Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika
Hii ni mara ya tatu
kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ikiwemo mara mbili ulifanyika Dar es
Salaam na Zanzibar ni mara ya kwanza.
*IDARA YA MAWASILIANO
IKULU, ZANZIBAR*
Comments
Post a Comment