NA ZUHURA JUMA, PEMBA
JAMII imetakiwa kuwa na utamaduni wa kupanda miti katika maeneo
yao wanayoishi, ili kuweka mazingira bora pamoja na kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi.
Akizungumza kwa niaba
ya Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu Pemba, mwalimu Harith Bakar Waziri wakati wa
upandaji miti kwa ajili ya kutengeneza msitu mdogo, katika skuli ya sekondari
ya Hemed Pujini alisema, Wizara itachukua juhudi za makusudi kuhakikisha
msitu huo unatunzwa.
Alisema kuwa, ni
manufaa makubwa kupata msitu huo kwani eneo hilo ni ukanda wa mashariki ambao
umeathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo utawasaidia sana wanafunzi,
walimu na wanajamii kuwa na mazingira bora na mazuri.
"Muone kuwa
kuwepo kwa msitu mdogo hapa ni jambo jema na ni fursa kwenu, hivyo kuna haja
kwa jamii kuiga mfano huu na wapande miti maeneo mbali mbali katika mitaa
yao," alieleza.
Aidha aliwataka
kuulinda na kuuhifadhi msitu huo ili kuleta manufaa kwao na jamii nzima, jambo
ambalo litaigwa na skuli nyengine kutokana na umuhimu wake.
Kwa upande wake
Mratibu wa mradi wa upandaji miti kwa ajili ya msitu mdogo kutoka taasisi ya
Aga Khan Foundation (AKF), Japhet Elly Wangwe alisema, lengo kubwa la mradi huo
ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kuwa,
wanapanda misitu midogo maeneo mbali mbali, ambapo kwa Dar-es-salaam na Lindi
wameshapanda maeneo 70 na Zanzibar ni mawili likiwemo la skuli ya sekondari
Hemed Pujini Pemba.
"Kwa Zanzibar
skuli ya kwanza ni hii ya Hemed na kesho tunaenda kupanda kule Unguja,
tunafanya hivi kwenye maskuli ili kupambana na hali hii, kwani wanafunzi
watajifunza na wataendeleza wakiwa majumbani kwao," alifahamisha.
Aliishukuru Serikali
kwa kuwapa mashirikiano makubwa, ambayo yanawapa msukumo na hamasa ya kuweka
mazingira bora ambayo hayataathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Nae Afisa kutoka Idara
ya Misitu Pemba Massoud Bakar Massoud alisema, aliishukuru AKF kwa kuwaletea
mradi huo kwani utawasaidia kurudisha asili ya kisiwa cha Pemba kwa kupandaji
miti kwenye maeneo mbali mbali.
"Kwa upande wetu
tunao mradi wa kurudisha asili ya kisiwa hiki, hivyo na mradi wa upandaji miti
kwa ajili ya misitu midogo itaongeza kasi ya kukabiliana na athari zinazotokana
na mabadiliko ya tabianchi," alieleza.
"Mabadiliko ya
tabianchi ni janga kubwa sana, hivyo ili kudhibiti hali hiyo tutashiriki
kikamilifu katika kusimamia, kuutunza na kudhibiti kusitokee uharibifu katika
eneo hilo," alifafanua.
Mapema Afisa Maendeleo
ya jamii kutoka taasisi ya Malezi na Makuzi Bora ya watoto wadogo (MECP-Z) Haji
Ali Hamad, aliwataka wananchi kuona kuwa suala la upandaji wa miti katika skuli
hiyo ni jema kwani wanatengeneza fursa kwao na wengine.
Mwalimu Mkuu skuli
hiyo Jamila Ali Saleh alieleza kuwa, watashirikiana na wanafunzi kuona kwamba
miti hiyo inakuwa na kunawiri vizuri, ili iweze kuwanufaisha.
Mwanafunzi Samira
Mohamed Nassor na Zahor Said Massoud walisema kuwa, wamejifunza kupanda miti na
hivyo wataishughulikia ili kuboreka, kwani wanaamini itawasaidia kupata
mazingira bora yenye upepo wa asili na hewa safi.
Katika utengenezaji wa
msitu huo mdogo, zaidi ya miti 200 ya aina mbali mbali imepandwa.
Comments
Post a Comment