HUDUMA YA MAJI SAFI NA SALAMA INAVYOKOSESHA USINGIZI WANANCHI WA KIJIJI CHA MJINI KIUYU

 

                           NA FATMA HAMAD PEMBA,

Ukosefu wa huduma za maji safi na salama,  bado ni kilio kikubwa kwa wananchi wa kijiji cha  Mjini kiuyu wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazi Pemba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko kijijini kwao, mwananchi Bikame Bakar Darusi,  alisema  huu  ni  mwaka wa tano  sasa  wamekua  wakikosa  huduma  hiyo  ya  maji safi  na salama.

Alisema wamekuwa wakipata tabu kwani wanashindwa kupata maji ya kutosha ya kufanyia  shughuli zao za nyumbani.

‘’Tunashindwa kupata maji hata ya kuwakoshea watoto wetu’’alieleza mwanachi Bikamae.

Aliendelea kusema kuwa watoto wao wanakwenda skuli na uchafu  kutokana na kadhya hiyo.

Kwa upande wake Bakar Hamad alisema suala la maji limekua ni tatizo sugu, ambalo linawatesa wanawake wa kijijini  hicho.

Alisema  siku yanayotoka maji kwa baadhi ya mabomba  hutoka kuanzia  sa tano  hadi tisa za usiku,  hali ambayo inapelekea wamama kukesha kwenye foleni ya maji.

‘’Hakuna hata mwanamme  mmoja anaelala na mke wake wakati wa usiku, kwani wanawake hulala kwenye  foleni za maji’’ alieleza mwananchi bakar.

Mapema Fatma Khalfan Suleiman alisema kuwa ukosefu wa maji unaweza ukapelekea wananchi wa kijiji hicho kupata maradhi hatarishi yatokanayo na uchafu.

‘’hatupati maji tukaweza kusafishia  vyoo  pamoja na nyumba zetu’’

Nae Ali Masoud alisema  wananchi wa kijiji  hicho  wameanguka kiuchumi  kwani, hawapati maji ya kumwagilia mazao yao.

‘’Kazi yetu kubwa sisi ni kilimo cha mboga mboga ila kwa sasa kimetushinda, tunateseka na watoto,’’ alisema  Ali Masoud.

Hivyo wameitaka wizara husika kukiona kilio chao ili waweze kuondokana na kadhya hiyo.

Fatma Ali na Asha Juma wanafunzi wa darasa la tano walisema wanakosa  kusoma masomo ya vipindi vya mwanzo darasani  kutokana na kuchelewa kwenye kutafuta maji  kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

 Afisa uhusiano wa mamlaka ya maji [Zawa]  Pemba Suleiman Anas  Masoud,  amekiri kuwepo kwa hilo kijiji hapo.

Alisema tatizo hilo linasababishwa  na kukosekana kwa matangi pamoja na uchakavu wa miundombinu ya kusambazia maji.

Hivyo amewataka wanachi hao kuwa na subra, kwani tayari wameshaingizwa kwenye mradi mpya ambao, unamaliziwa kufanyiwa  upembuzi yakinifu, unaofadhiliwa na Benk ya watu wa ujerumani,  ambao utajenga matangi kwenye vijiji vilivyo na shida ya maji. 


 





Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.