WASAIDZI WA SHERIA WAHIMIZWA KUISAIDIA JAMII.
NA FATMA HAMAD PEMBA.
Jumuia za wasaidizi wa sheria zimetakiwa kuendelea kuisaidia jamii kwa kutoa msaada wa kisheria ili kupunguza migogoro pamoja na malalamiko yasiyo ya lazima.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa mdhamini ofisi ya Rais, katiba sheria, Utumishi na utawala bora Halima Khamis Ali wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kisheria ngazi ya jamii huko makonyo Chake chake Pemba.
Alisema wasaidizi wa sheria wanajukumu kubwa katika kuhakikisha wanaielimisha jamii kuhusu masuala ya kisheria ili kuibua matatizo yanayowakumba wanajamii na kuweza kupatiwa ufumbuzi.
''Wasaidizi wa sheria mnajukumu kubwa hivyo ni lazima muwe na uzalendo na moyo wa kujitolea ili kuleta mabadiliko katika jamii zetu'' alieleza mdhamini Halima.
Alisema kutokana na umuhimu wa kuepo kwa wasaidizi wa sheria ngazi ya jamii Serikali imeweka mikakati mbali mbali ili kuona wanaharakati hao wanatambulika kisheria katika utendaji wa majukumu yao.
Aidha mdhamini huyo aliwasihi wasaidizi wa sheria kutekeleza majukumu yao ya utoaji wa msaada wa kisheria kwa kufuata miko na madili ya kazi yao.
''Kila kitu kina utaratibu wake na sisi wasaidizi wa sheria sio vizuri kutoa msaada wa kisheria bila kutambulika kisheria'' alisema mdhamini.
Alifahamisha kuwa kitendo walichokifanya jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake [CHAPO] cha kuanzisha darasa maalumu la sheria ngazi ya jamii ni kitendo cha kupigiwa mfano na kinafaa kuigwa na jumuia zote za wasaidizi wa sheria zilizopo Zanzibar.
Kwa upande wake Afisa habari wa jumuia hiyo Haji Nassor Mohd alisema utoaji wa mafunzo hayo ni moja ya sehemu ya utoaji wa elimu ya kisheria ndani ya jamii.
Mafunzo hayo ya siku 10 ya kisheria ya kuwajengea uwezo wanashehia ambayo yanatarajia kufanyika baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa ramadhani yatawajumuisha Masheha na wajumbe wao yameandaliwa na jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake [CHAPO] ambapo mada mbali mbali zitawasilishwa ikiwemo Sheria ya mtoto sheria namba 6/2011 sheria ya Zanzibar.
Comments
Post a Comment