BAADA YA BLOG YA PEMBA YA LEO KUIBUA KERO YA MWALIMU WA MADRASA MWENYE ULEMAVU KOKOSA SEHEMU SALAMA YA KUSOMESHEA SASA APATA UFADHILI WA KUJENGEWA.
-Mwalimu
mwenye ulemavu wa viungo ajengewa
mdarassa Shumba vyamboni
-Aibuka
kuushukuru mtandao wa pemba ya leo, mfadhili, wanafunzi wasema
jambo
FATMA
HAMAD, PEMBA
JUNE 24 , mwaka 2022, Blog ya pemba ya leo, lilichapisha
makala, ikielezea changamoto za ukosefu wa madrassa ya kisasa ya mwalimu wa madrasa
mwenye ulemavu wa viungo.
Mwalimu huyo Saada Khamis Hamad wa Shumba
vyamboni wilaya ya Micheweni mkoa wa kaskazini Pemba, akikabiliwa na changamoto
ya ukosefu sehemu rafiki na salama ya kusomeshea wanafunzi wake.
Ndoto zake za kupata madrassa ya kisasa kwa ajili
ya kufundishia wanafunzi wake, hakuwa nayo kabisa kwenye akili yake, hasa kwa
vile alishasomesha miaka zaidi ya minne katika mazingira magumu.
Kwa kweli alikua na kilio cha siku nyingi, cha kupata
ufadhili wa kujengewa madrasa, ndipo mwandishi wa makala kupitia blog ya pemba
ya leo Pemba, alipochapisha makala yake na kisha wafadhili kuchomoza.
Nilikua sina tegemeo kama ipo siku moja nitaondokana na kadhia hii ya kusomesha
kibarazani.
‘’Sikua na tamaa kabisa kama na mimi ipo siku
nitasomesha nikiwa ndani ya madrsa’’alisema mwalimu.
na mimi natasomesha wanafunzi wangu nikiwa ndani ya madras
MJENZI
WA MADRASSA
Msimamizi anaeshughulikia
ujenzi wa madrasa hiyo, Mohamed Suleiman kutoka kijiji cha Konde, anasema
ujenzi huo ni ufadhili kutoka kwa Jumuia ya Firdausi yenye makao makuu yake jijini
Dar-es Salaam.
Baada ya kusikia kwa
waumini, ambao nao walisoma kwenye Blog ya Pemba ya leo, ndipo naye alipochukua juhudi za
kuwasiliana na wafadhili hao.
Anaona, kuandikwa kwa
habari hiyo juu ya changamoto za mwalimu huyo mwenye ulemavu, kusomesha
barazani wanafunzi 75 ni shida.
‘’Kwa hakika, uandishi
ule uliofanywa na mwandishi wa makala ya Blog ya Pemba ya leo ya june 24, mwaka 2022, juu ya shida na dhiki ya
makaazi ya wanafunzi wa madrassa,’’anasema.
Hapo kilichofuata, ni
kulipima eneo ambalo mwalimu husika ameamua kuwa ndio eneo la madarssa, na
baada ya kujua idadi ya wanafunzi wake, ilirahisisha kazi.
‘’Tumejenga madrasa yenye
chumba kimoja chenye upana na urefu wa mita nane kwa saba (8/7), pamoja na vyoo
viwili kwa ajili ya wanafunzi,’’anasema.
‘’Sisi kwa sasa
tunaendelea na ujenzi na umefikia asilimia 95 maana, umeanza kupigwa plasta na
wakati wowote, wanafunzi na mwalimu watahamia,’’anasema.
MWALIMU WA MADRASSA
Mwalimu
huyo Sada Khamis Hamad, anasema wakati anahojiwa na mwandishi wa makala, hakuwa
na fikra ya kuwa inaweza kuwa msaada wa kupatiwa madrassa ya kisasa.
‘’Wengi wameshapita na kunihoji na wakiniahidi
kuwa, ntajengewa madrassa ya kisasa, lakini mwisho wa siku hakuna lolote,
lakini kwa mwandishi wa Blog ya Pemba ya leo, nashukuru kwa sasa,’’anasema.
Walishasema wahenga kuwa, Mungu si asumani, kwa
hakika sasa msemo huu, umejidhihirisha kwa mwalimu Saada mwenye ulemavu
aliyekuwa, akiwapatia elimu ya kur-an wanafunzi 75 barazani kwake.
‘’Leo kwa hakika, siku chache zijazo, ntahamia ndani ya madrassa ya kisasa naushukuru mtandao wa Blog ya pemba ya leo, wafadhili, ofisi ya Mufti na wilaya kwa kusambaaza taarifa zangu,’’anasema.
‘’Kwa kweli nimefurahi sana, kuona kwamba kile
kilio changu cha miaka minne kimepata ufumbuzi,’’ alisema mwalimu Saada.
‘’Tunu yangu ni kuona na
mimi ninasomesha nikiwa katika madrassa kama vile wenzangu na sio juani kama
hivi, haya sio mazingira mazuri, kweli nateseka na wanafunzi wangu,’’anasema.
WANAFUNZI WA MADRASSA
Abdala Kombo Rajabu
ambae ni mmoja wa wanafunzi wa madrassa hiyo, anasema anayo furaha kubwa
kujengewa kwa madrassa ya kisasa, ambayo ilikuwa ndoto yao.
‘’Kwakweli hali hii ya
kusomea kwenye kibaraza ni moja ya changamoto ilioikitufanya tusihudhurie
madrasaa, lakini sasa twashukuru mno, kwa waandishi na wafadhili wetu,’’anasema.
Mwanafunzi Fatma Juma
Hamad, anasema ujenzi wa madrassa yao, ameupokea kwa furaha na bashasha, kwani
wataondokana na changamoto ya kusoma kwenye baraza kama zamani.
‘’Tumefurahi kuona kile
kilio chetu cha muda mrefu cha kupata sehemu salama ya kusomea sasa, kimepata
ufumbuzi,’’anasema mwanaunzi Fatma.
Rehema Haji Seif
amewataka wanafunzi wenzake, kuitunza na kuilinda miundombinu ya madrassa hiyo,
ili kuwanufaisha wao na wengine hapo baadae.
WAZAZI WA WANAFUNZI
Haji Seif ameeleza kuwa,
licha ya msaada huo aliopata mwalimu huyo, watahakikisha nawao wanamuunga mkono,
ili kuona anapata nguvu ya kuendeleza, jambo lake hilo, la kuwapatia watoto
elimu ya kur-an.
‘’Kwa vile mwalimu huyo nguvu zake zote kazielekeza
kutusomeshea watoto wetu, na sisi tutahakikisha tunamsaidia japo kwa michango
midogo midogo,’’anasema.
Asha Khamis Ali
alimshukuru muhisani, ambae alijitolea na kujenga madrassa, baada ya kuona
habari iliyorushwa na mwandishi wa habari June 24, mwaka 2022 juu changamoto ya
kusoma kwenye barazani.
‘’Tunamuombea duwa
muhisani wetu aliewajengea watoto wetu madrassa, Mwenyezi Mungu ampe imani
aendelee kuelekeza nguvu zake kwenye mambo ya kheri,’’ anafafanua.
WANAFAMILIA
Assa Khamis Hamad mwenye
ulemavu wa viungo ambae ni kaka wa mwalimu huyo, amesema msaada wa ujenzi wa
madrassa wameupokea kwa mikono miwili.
Mama mzazi wa mwalimu
huyo Hadia Salim Ameir amewashukuru wahisani waliomsaidia mwanawe huyo, kwani
wamekua wakija watu wengi wakimuahidi na mwisho wa siku hawaoni lolote.
‘’Kipindi cha nyuma huja
watu wakinihoji na kujidai watakuja kunisaidia, ila sioni lolote, sijui ilikua
wakifanya kwa ajili ya maslahi yao tu au vipi,’’anaeleza.
OISI YA MUFTI
Sheikh Said Mohamed
kutoka Ofisi ya Mufti kisiwani Pemba anasema, amefarijika kuona mwalimu huyo
amepata ufadhili wa kujengewa madrassa.
‘’Kama ofisi ya Mufti
tumefurahi kuona wafadhili na wahisani wamejitokeza na kumsaidia mwalimu huyo
wa madrassa, mwenye ulemavu anaefanya kazi ya kuyasambaza maneno ya Mwenyezi Mungu,’’anaeleza.
WANAHARAKATI
Safia Saleh Sultan
kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Pemba, anasema moja ya utekelezaji wa haki za
binadamu moja ni kuweka mazingira rafiki ya kupata elimu.
Asha Mussa Omar, anasema
juhudi za mwalimu huyo, ndio mwelekeo wa TAMWA katika kuthibitisha kuwa
wanawake wanaweza kufanya mambo makubwa.
Mjumbe wa kamati tendaji
wa Jumuia ya wanawake wenye ulemavu Pemba bi Hidaya Mjaka Ali amesema
wanafuraha kuona juhudi za watu wenye ulemavu
zinafanikiwa.
KATIBA YA ZANZIBAR YA
MWAKA 1984
Kifungu cha 10 (g)
kinafafanua ‘kwamba serikali itawekea mazingira rafiki kwa makundi ya wagonjwa,
waliojiajiri, wazee, watoto na watu wenye ulemavu’.
Lakini hata kifungu cha
12 (1) kimefafanua kuwa, ‘watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila
ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria’.’
SHERIA YA WATU WENYE ULEMAVU NO 9/2006
Kifungu cha 9,
kinaelezea haki ya kupata elimu kwa watu wote wenye ulemavu na mafunzi mengine
kama ilivyo kwa raia wengine.
MIKATABA YA KIMATAIFA
Mkataba wa kimataifa wa
haki za watu wenye ulemavu, kwenye ibara 24 (b) inafafanua kuwa, nchi
zilizoridhia mkataba huu, wanatakiwa kuendeleza mtazamao, uwezo na ubunifu
pamoja na uwezo wao wa akili na mwili kwa watu wenye ulemavu.
Comments
Post a Comment