NA SAID ABRAHMAN PEMBA.
SHIRIKA la Umeme
(ZECO) tawi la Pemba limesema kuwa litaendelea kushirikiana na wananchi wa
Kisiwa hicho ili kuhakikisha nishati hiyo inaenea vijiji vyote vilivyoko huko.
Hayo yalibainishwa na
Ofisa mipango na utafiti wa Shirika hilo Ali Faki Ali wakati alipokuwa
akizungumza na Masheha wa Wilaya ya Wete huko katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya ya Wete.
Alieleza kuwa Kwa Sasa
Shirika limefanikiwa kupeleka nishati ya umeme katika vijiji vipatavyo 417 kati
ya 424 huku Shirika hilo likipeleka nishati hiyo katika Visiwa vyote 8
vilivyomo ndani ya Pemba ikiwa ni pamoja na Njao, Fundo, Kokota, Uvinje,Kojani,
Shamiani,Kisiwa panza na Makoongwe.
"Kwa Sasa tuna
asilimia 98.3 ya vijiji vyote ambavyo tayari vimeshapata huduma ya umeme huku
asilimia 1.7 tu ndivyo ambavyo vimebaki havina umeme, Shirika limo mbioni
kuhakikisha navyo vinapata umeme mwaka huu," alieleza Ofisa Ali
Ofisa huyo alivitaja
vijiji ambavyo havijafika na huduma ya umeme Hadi sasa ni pamoja na Kijiji Cha
Kivumoni Mtambwe pamoja na Kijiji cha Mtakao Kilichopo Shehia ya Mlindo Kwa
upande wa Wilaya ya Wete.
"Ama Kwa upande
wa Wilaya ya Micheweni ni Kiuyu mbuyuni ambako Kuna vijiji vitatu navyo ni
Mkwaju panda, Makombani na Mkondoni huku Wilaya ya Mkoani ni Mtadoda iliyopo
katika Shehia ya Minazini pamoja na Kijiji Cha Alikoni Kilichopo Shehia ya
Chumbageni Mkoani," alieleza Ali.
"Jukumu la
Shirika la umeme ni kuwafikishia wananchi wote huduma ya nishati ya umeme,
hivyo katika mikakati yetu tumedhamiria kuona wananchi wananufaika na huduma
hii," alisema Ofisa huyo.
Nae Ofisa Mipango na
utafiti wa Shirika hilo Pemba Hafidh Tahir Silima aliwafahamisha Masheha hao
kuwa Kwa Sasa hakuna gharama yeyote ambayo anatozwa mwananchi Kwa kununua nguzo
ya umeme.
"Serikali ya
awamu ya nane (8) chini ya Dkt, Hussein Ali Hassan Mwinyi umeondoa gharama ya
kuchangia nguzo Kwa wananchi wake,lakini pia hata gharama za kuunga umeme pia
zimepunguzwa Hadi kufikia Tsh, 200,000/- (laki mbili),"alieleza Hafidh.
Hata hivyo Ofisa huyo
aliwatoa wananchi ambao tayari wameshalipa gharama za kuungiwa umeme katika
maeneo yao lakini Hadi sasa huduma hiyo haijawafikia wasiwe na wasiwasi Shirika
limo mbioni kuona nao wananufaika na huduma ya umeme.
"Tulikuwa na
tatizo la vifaa ila Kwa Sasa muarubaini umepatikana kwani meli ambayo ilibeba
mzigo wa vifaa hivyo tayari imeshafunga nanga katika bandari ya Unguja na mzigo
umeshaanza kupakuliwa, hivyo tutahakikisha wale ambao wameshalipa fedha zao
wanapata huduma," alisema Hafidh.
Nae Mohammed Said
Sound aliwata Masheha kuwashajihisha wananchi wao kufika ofisini wenye wao
wakati wanapotaka kuunga umeme bila ya kumtuma mtu mwengine ili kuepusha
rushwa.
"Tuwatake
wananchi wetu pale ambapo watakuwa wanataka kuunga umeme ni vizuri kuja wenyewe
ofisini kwetu ili kuepusha rushwa," alisema Mohammed.
Mapema akifungua kikao
hicho, Katibu Tawala Wilaya ya Wete Mkufu Faki Ali aliupongeza uongozi wa
Shirika la umeme Pemba Kwa mashirikiano yao kwani wamekuwa karibu sana na
wananchi wake.
Alisema kuwa kikao
hicho ni utaratibu wa Shirika hilo uliojipangia ili kuonana nao na kupata
takwimu sahihi za vijiji ambavyo Hadi sasa havijapata huduma ya umeme.
Aidha Katibu huyo
alifahamisha kuwa Shirika hilo limepewa jukumu na Serikali kuhakikisha wananchi
wote wanapata huduma ya umeme bila ya ubaguzi wowote ule.
"Tunalishukuru
Shirika la umeme Kwa kuwa nasi karibu sana kwani pale ambapo panatokezea tatizo
lolote watendaji wake hufika katika eneo na kuweza kulitatua Kwa muda
muafaka," alisema Mkufu.
Nae Mwenyekiti wa
Masheha Wilaya ya Wete ambae pia ni Sheha wa Shehia ya Mtambwe Kusini Othman
Ali Khamis amelipongeza Shirika la Umeme (ZECO) Kisiwani Pemba Kwa mashirikiano
yao wanayowatoa Kwa wananchi wao.
"Tunaliomba
Shirika kuendelea kushirikiana na sisi ili tuweze kupiga hatua ya maendeleo
katika maeneo yao," alisema Sheha Othman.
Comments
Post a Comment