WANANCHI WAHIMIZWA KUCHUKUA TAHADHARI JUU YA KUJIKINGA NA UGONJWA WA UKO19
NA FATMA HAMAD PEMBA
AFISA
Mdhamini wizara ya Afya, ustawi wa jamii, wazee, jinsia na watoto Pemba Yakoub
Mohamed Shoka, amewataka waandishi wa habari kuelimisha jamii kwa kutilia mkazo
suala la unawaji wa mikono ndani ya jamii zao zilizowazunguka.
Alisema, hivi sasa takwimu za kidunia zinasema kati ya nchi 60 zenye
maambukizi ya Corona katika kiwango kikubwa kila watu wawili kati ya watatu
kwenye watu Bilioni 1 ambao wameshapata maambukizi wamekosa huduma safi ya
mikono majumbani mwao kwa kunawa maji tiririka na sabuni.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Afisa mdhamini huyo Afisa uwezeshaji kinga
na elimu ya afya Pemba Khamis Bilali Ali alisema, matumizi ya maji yamehimizwa
na kutajwa hata katika vitabu vya dini hivyo aliitaka jamii kujenga utamaduni
wa kunawa mikono ili kuepuka maradhi yanayoambukizwa.
Aliyasema hayo katika mkutano uliowashirikisha waandishi wa habari
ikiwa ni katika kuelekea maadhimisho ya siku ya unawaji mikono Zanzibar
uliofanyika ukumbi wa hoteli ya Archipilago Tibirinzi Chake chake.
Alisema, kutokana na taarifa za hivi karibuni watu waliowengi hususani
kwa nchi zilizoendelea ikiwemo Zanzibar ipo katika uwezekano mkubwa wa kupata
maambukizi yanayotokana na kutokunawa mikono.
“Tunaweza kupata maambukizi ya magonjwa ya kipindupindu na Corona sababu
kuu ikiwa ni kutoendeleza tabia na utamaduni wa kunawa mikono na nusu ya
wanaopata madhara ni watoto, katika maeneo ya skuli kukosa nyenzo”, alisema.
Aidha alisema, iwapo jamii inataka kujizuia na maradhi hayo ni lazima
itoe kipaumbele katika suala la usafi wa mikono na huduma zake zipatikane wa
wote.
Hata hivyo alisema, Wizara ya afya hivi sasa inahitajika kuunganisha
nguvu zake kwa wafadhili wa kimataifa, kitaifa, sekta za serikali na binafsi
pamoja na asasi za kiraia ili kuhakikisha kunakuwa na nguvu za pamoja za
upatikanaji wa nyenzo na huduma rahisi watu wanazoweza kuzimudu.
Mapema Mratibu wa kitengo cha elimu ya afya Pemba Abeid Ali Ali
alisema, lengo la kuandaa mkutano huo kwa waandishi wa habari ni kupeleka elimu
kwa jamii.
“Waandishi wa habari ni kiunganishi kizuri kati ya jamii na jamii
nyengine hivyo tumefarajika sana kukutana nanyi katika mkutano huu matumaini
yetu mutafikisha taarifa kwa jamii kama inavyotakiwa”, alisema.
Nae Mtaalamu wa afya ya jamii kitengo cha afya na mazingira Halima Ali
Khamis alisema, mipango ya wizara katika kuelekea siku ya unawaji mikono jambo
la kwanza ni kuelimisha jamii licha ya kuwa jamii ni ngumu kulingana na tabia
zilizojengeka za kutokunawa mikono kwa maji tiririka.
“Wizara ina mipango mingi katika kulifanikisha jambo hili iliwemo
kutoa elimu kwa jamii, kupitia gari za matangazo, vipeperushi, video, lazima
jamii ifahamu kwamba kunawa mikono ni njia ya kujikinga na maradhi mbali mbali”
alisema.
Siku ya kuosha mikono huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 15 ya kila
mwaka lakini kutokana na sababu mbali mbali maadhimisho hayo yalilazimika
kusogezwa mbele na kutarajiwa kufanyika Kitaifa Febuari 8 mwaka huu kauli mbiu
yake ikiwa ni “OSHA MIKONO OKOA MAISHA”.
Comments
Post a Comment