UGONJWA WA KOVID 19 BADO NI TATIZO KWA WATU WENYE ULEMAVU

 


NA FATMA HAMAD FAKI.

Watu wenye ulemavu wamehimizwa kuendelea kuchukua tahadhari juu ya kujikinga na ugonjwa wa Uviko 19 katika Jamii zao.

Wito huo umetolewa na mjumbe wa kamati tendaji wa jumuia ya watu wenye ulemavu [ZAPDD] Mkubwa Ahmed Omar wakati akifungua mafunzo ya siku moja juu ya kujikinga na ugonjwa kovid kwa watu wenye ulemavu huko Gombani Chake chake Pemba Alisema watu wenye ulemavu ni moja ya kundi lililotajwa kuwa hatarini zaid kupata ugonjwa huo.

Alisema ipo haja kwa watu hao kuchukua jitihada ya hali ya juu ikiwemo kuosha mikono mara kwa mara, Kuchoma chanjo  pamoja na kuvaa barakoa wakati wanapokwenda katika mikusanyiko ya watu jambo ambalo litaepusha kuenea kwa ugonjwa huo.

‘’Nawaomba jamani tujitahidi sana kuchukua tahadhari kwani ugonjwa bado upoo’’aliwasihi mjumbe.

Akiwasilisha mada Afisa kutoka jumuia ya watu wenye ulemavu Zanzibar [ZAPDD] Khalid Abdala Omar alifahamisha kuwa kwa mujibu wa tafiti ya mwaka 2018 jumla ya watu wanaoishi na ulemavu wa aina mbali mbali hapa Zanzibar  ni 54,335 ambapo ni sawa na asilimia 5.9,

Kati yao, watu 41,273 sawa na asilimia 7.1 wanaishi Vijijini.

Alisema  tafiti hiyo inaonesha kuwa watu wengi wenye ulemavu wanaishi zaid katika maeneo ya vijijini .

Alisema licha ya kuwepo kwa watu wengi wenye ulemavu katika maeneo hayo lakini bado huduma za kiafya hazirishi, hivyo ipo haja kwa tasisi husika kuboresha huduma hizo ili kuwaondoshea usumbufu wakati wanapofikwa na matatizo.

Aidha aliwataka Viongozi wa jumuia za watu wenye ulemavu kuwa karibu na jumuia zao ili waweze kuziibua changamoto zinazowakabili wanachama wao na kuweza kupatiwa ufumbuzi.

Modathir Sharif Khamis kutoka jumuia ya Maalbino Zanzibar [JMZ] aliwashauri wazazi wenye watoto wenye ulemavu  wasiwaruhusu watoto wao kwenda katika mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima kwani kufanya hivyo kutawakinga na ugonjwa wa kovid 19.

Nae mratibu wa jumuia ya watu wenye ulemavu[ZAPDD] kisiwani Pemba Khalfan Amour Mohd alisema lengo la kutoa mafunzo kwa makundi hayo ni kuona  ile tahadhari ya kujikinga na ugonjwa  huo inachukuliwa kila sehemu na kuepukana na ugonjwa huo.




Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.