NA SAID ABRAHMAN PEMBA.
JAMII imeiomba Serikali kujenga viwanda vya kusindikia samaki
ili kwenda sambamba na dhana ya uchumi wa bluu.
Wakijadili mada juu ya uchumi wa bluu katika kikao
kilichoandaliwa na taasisi ya Action aid, huko Kojani Mkoa wa Kaskazini Pemba,
wananchi wa Kisiwa hicho walisema kuwa ni vyema kwa Serikali kuanzisha viwanda
hivyo ili waweze kunufaika na mazao yanayotokana na bahari na kufikia azma ya
uchumi wa bluu.
Walieleza kuwa wananchi wananchi walio wengi hawajawa na uelewa
sahihi juu ya dhana ya uchumi wa bluu, hivyo ni vyema kwa Wizara husika kutoa
taaluma kwa wananchi ili waweze kuelewa maana yake.
Hamad Juma mjumbe wa Kikundi Cha Mduara alisema kuwa ili Serikali
iweze kukuza uchumi wa bluu na kukuza hali za maisha ya wananchi lazima iweze
kujenga viwanda vya kusindikia samaki ili iweze kwenda sambamba na azma yenyewe
ya Uchumi wa bluu.
Alieleza kuwa endapo Serikali itaweza kujenga viwanda hivyo
wananchi wengi wataweza kunufaika ikiwa ni pamoja na kupata ajira ambazo
zitainua hali zao za kiuchumi.
"Serikali ikiweza kufanya jambo hili la kuweka viwanda vya
kusindikia samaki naamini wananchi wengi wataweza kupata nafasi za ajira katika
viwanda hivyo,lakini pia hata wale samaki ambao watavuliwa wataweza kuhifadhika
kiurahisi zaidi," alisema Hamad.
Nae Mohammed Juma Ali mkaazi wa Kojani aliwaomba watendaji wa
Wizara husika kushuka chini kwa wananchi ili kuelimisha mantiki ya uchumi wa
bluu ili wananchi waweze kufahamu dhana hiyo.
Aidha Mohammed aliiomba Wizara hiyo kuandaa mikakati maalum
ambayo itatekelezeka na kutoa ufanisi mzuri kwa watendaji wake ili wananchi
waweze kufaidika na uchumi wa bluu.
Mapema Mohammed alieleza kuwa katika bahari Kuna faida nyingi
ambazo zinapatikana ikiwemo uvuvi, kilimo Cha mwani, ufugaji wa majongoo,
mapambo ya nyumbani,madini pamoja na mafuta ambavyo vyote vina faida kwa jamii
na taifa kwa ujumla.
"Katika bahari Kuna faida nyingi sana ambazo zinapatikana
na zinaleta tija kwetu ikiwemo kilimo,ufugaji, mapambo na madini",
alieleza Mohammed.
Nae Mwenyekiti wa Kikundi Cha Mduara Kombo Hamad Kombo aliiomba
Serikali kutilia maanani suala zima la upatikanaji wa bima kwa wavuvi.
Alisema kuwa imekuwa ni shida kubwa kwa wavuvi wakati wanapopata
matatizo wakiwa katika harakati zao za uvuvi.
"Mara nyingi sisi wavuvi tunaovua maeneo ya mbali huwa
tunapata matatizo mbali mbali ikiwemo kupotelewa na nyavu zetu au hata mashine
zetu, hivyo tunaiomba Serikali kufanya jitihada za makusudi ili kuona wavuvi
wanapatiwa bima ambayo itaweza kuwasaidia pale wanapitokezewa na
matatizo,"alisema Mwenyekiti Kombo.
Comments
Post a Comment