MKE WA MAKAMO WA KWANZA WA RAIS AKABIDHI VIFAA VYA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO KATIKA HOSPITALI YA VITONGOJI



 

MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, ametoa wito kwa mamlaka zote pamoja na asasi za kiraia, kuimarisha afya ya mama na mtoto, ili kujenga ustawi bora wa jamii, utakaochangia maendeleo ya nchi.

 Mama Zainab aliyasema hayo leo katika ziara yake, alipotembelea Hospitali ya Vitongoji, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

 Alisema afya ya mama na mtoto ni sehemu muhimu ya msingi wa ustawi wa jamii, unaolenga kuzalisha na kuendeleza nguvu kazi ya Taifa, na hatimaye kufanikisha juhudi za kujiletea maendeleo.

 "Afya zikiwa vizuri hata uzalishaji unaongezeka, hivyo ni vyema kuzitumia rasilimali tulizonazo kwa uangalifu katika kutoa huduma bora za kijamii ambazo ni pamoja na afya ya mama na mtoto," amesema Mama Zainab. 

 Akitoa nasaha zake mbele ya madaktari na wahudumu wa hospitali hiyo, Mama Zainab ameahidi kupaza sauti kwa wadau wa afya ili kusaidia kuzitatua changamoto, zikiwemo za uhaba wa vifaa, hasa katika wodi ya akinamama wajawazito na sehemu ya kujifungulia.

 Aidha alitoa wito kwa madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kuendelea kuchukua tahadhari na kuwaelimisha watu juu ya athari za mripuko wa janga la CORONA.



 Naye Daktari dhamana wa Hospitali ya Vitongoji, Dokta Sharif Khatib alieleza shukran zake za dhati kwa kufanikiwa kupata kifaa kipya cha kupimia damu na utambuzi wa maradhi mbali mbali cha ‘HAEMATOLOGICAL ANALYZER’, kitakachosaidia ufanisi wa huduma za hospitali hiyo kwa wananchi.




Mama Zainab ambaye aliambatana na Bi. Awena Masoud Sanani, Mke wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, katika ziara yake kisiwani Pemba, ametembelea maeneo mbali mbali yakiwemo Jengo la Bohari ya Dawa la Vitongoji, kabla ya kuelekea Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

 Katika ziara hiyo, Bi Zainab aliongoza zoezi la kuwapatia misaada mbali mbali wagojwa na watu wasiojiweza, ikiwemo sabuni, pempasi, mipira ya kusaidia kujifungua kwa akina mama pamoja na mashuka ya vitanda vya hospitali.

 Akikabidhi vifaa hivyo Mama Zainab alitoa wito kwa wananchi kujitokeza katika kusaidia, ijapokuwa kwa kiasi kidogo, ili kuwapatia unafuu wanyonge na kuwatatulia changamoto zinazowakabili.



 Akitoa salamu za wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Bi Mgeni Khatib Yahya alisifia juhudi za utendaji mzuri zinazotekelezwa na wahudumu wa Hospitali ya Micheweni, licha ya changamoto ya kuhudumia idadi kubwa ya wananchi kila siku.

 Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na wauguzi wa Hospitali hiyo iliyopanda daraja hadi Hospitali ya Wilaya kuanzia Agosti 30 mwaka huu, ili pia kusaidia kufanikisha malengo ya Serikali.

 Naye Afisa Mdhamini wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto  Yakoub Mohd Shoka alisema ujio wa Mama Zainab katika ziara hiyo ni faraja kubwa, huku akitoa wito kwa viongozi wengine kufuata nyayo zake katika kuimarisha na kuendeleza Sekta ya Afya.









 


 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.