JAMII JATAKIWA KURUDISHA MALEZI YA PAMOJA KATIKA KULEA WATOTO WAO

 MKUU wa Wilaya ya Wete Hamad Omar Bakar ameitaka jamii kushirikiana pamoja katika kupinga  vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku.

Alisema kuwa kwa mujibu zilizotolewa na Wizara ya afya na Ustawi wa jamii imebainisha kuwa Shehia ya Kizimbani kwa Wilaya ya Wete imekuwa ikiongoza kwa vitendo vya udhalilishaji.

Mkuu huyo wa Wilaya aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Idrisa Abdulwakil Kizimbani Wete, wakati alipokuwa akizungumza na Kamati mbali mbali zilizomo katika Shehia ya Kizimbani.

Alieleza kuwa Shehia ya Kizimbani ni miongoni mwa Shehia 36 zilizomo katika Wilaya ya Wete ambayo imekuwa ikitajika sana kuongoza katika vitendo vya udhalilishaji ndani ya Wilaya hiyo.

"Tumeitana hapa ili tuweze kujadiliana au kubuni mbinu zipi ambazo tutaweza kuzitumia ili kuondosha tatizo hili la unyanyasi katika Shehia yetu hii ya Kizimbani kwani imekuwa ni Jambo la aibu sana," alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Mapema Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka Wana jamii hao kushirikiana pamoja na kurudisha malezi ya pamoja Kama ilivyokuwa hapo awali.

"Endapo wanajamii hatutorudisha malezi kwa pamoja tatizo Hilo halitaondoka, lakini pia tatizi hili sio la Serikali bali ni jukumu la jamii yote," alieleza Mkuu wa Wilaya.

Nae Ofisa Ustawi kutoka Wilaya ya Wete Salma alieleza kuwa hivi kumekwa na michezo mbali mbali ambayo watoto huwa wanaicheza ambayo ni hatari kwao.

Alieleza kuwa Ofisi yao ilikaa na wanafunzi hao na kufanya nao mazungumzo na kubaini kuwa michezo hiyo ambayo wanaicheza wameotoka nayo majumbani mwao

"Hivi sasa watoto wetu wamekuwa wakicheza michezo ambayo sio salama kwao na michezo hiyo imetokea mitaani kwetu na watoto kuipeleka maskulini," alisema Salma.

Nae Kamanda wa Polisi Wilaya ya Wete Richard Ogutle aliwataka Wana jamii kushirikiana pamoja na jeshi la Polisi ili kuondosha vitendo vya udhalilishaji katika Shehia zao.

Alisema kuwa bado wananchi wamekuwa na muhali mkubwa wa kutoa ushahidi wa vitendo hivyo jambo ambalo linarudisha nyuma mapambano dhidi ya vitendo viovu anbavyo kwa sasa imekuwa ni tishio.

Nae Bakar Haji Omar mkaazi wa Bopwe alisema kuwa ili kuondosha vitendo hivyo katika ni lazima Jambo la kwanza ni kurudishwa kwa ulinzi shirikishi (Polisi jamii).

Alieleza kuwa wakati ilipokuwepo Polisi jamii katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Wete vitendo vingi viovu viliweza kupungua kwa asilimia kubwa sana.

"Kilichoturudisha nyuma ni pale kutopata uungwaji mkono na Serikali kuu na hivyo jamii ikakata tamaa na kusambaratika bila ya mafanikio yeyote yale,"alisema Bakar.

Nae Ali Rashid Ali mkaazi wa Kizimbani alieleza sababu kubwa ambazo zimepelekea kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji ndani ya jamii ni wazazi wenyewe bado wako nyuma juu ya malezi ya watoto wao.

Alisema endapo wazazi wazazi watakubali na kwa pamoja na kulea vijana wao matendo hayo yanaweza kuondoka bila wasiwasi wowote ule.

Nae Mwalimu Mkuu wa Skuli ya msingi Kizimbani Khadija Khamis Amour alieleza kuwa aliliomba jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na Skuli hiyo ili kuondosha vitendo vya udhalilishaji katika Skuli yao.

Alifahamisha kuwa kipindi ambacho jeshi la Polisi lilifanya msako wa kuwakamata na kuwapeleka kituoni baadhi ya wanafunzi ambao ni watukutu hali ilikuwa ni shuari sana katika maeneo yote ya Skuli.

"Tunaliomba jeshi la Polisi kuendeleza ile amsha ambayo ilikuwepo kwani tuliweza kupata afuweni sana maana wale wote ambao walikuwa wanatoroka madarasani wakati wa masomo na kukaa nje walikata kabisa,"alisema Mwalimu Khadija.

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.