BINTI WA MIAKA 15 AMBAE NI MWANAFUNZI WA DARASA LA TANO APEWA UJAUZITO KWA MARA YA PILI NA SHEMEJI YAKE PEMBA.


 




NA FATMA HAMAD PEMBA. 12/4/2021.

 Mtoto wa miaka 15  apewa ujauzito  kwa mara ya pili huko Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba

Waswahili husema mchovya asali hachovi mara moja. Ni hakika hii ndio kawaida kwani asali ladha yake ni tamu na kama utaendekeza kuchovya basi huenda ukamaliza kibuyu.

Mimi kwa hapa naulinganisha msemo huu na wale wanopenda kupata mazuri kwa njia ya mkato bila kujali athari zinazoweza kujitokeza, kwani akifanya mara ya kwanza akifanikiwa bila kupata tatizo lolote basi kwake hujenga mazowea na akaendeleza tabia yake bila kujali kwamba atajiharibia au kumuharibia anaemfanyia uovu hule.

Na haya ndo aloyafanya kijana Mosi Othman Mosi mkaazi wa Muambe Wilaya ya Mkoani huko Kisiwani Pemba.

Kijana huyu bila huruma wala kujali athari za anaemfanyia amediriki kwa mara mbili mfululizo kumpa ujauzito mtoto wa miaka 15 mbaye kwa sasa yupo darasa la tano.

Alianza kumfanyia unyama huu akiwa darasa la nne ambapo kwa wakati huo alikuwa ana umri wa miaka kama 13 hivi na msichana huyu mdogo alilazimika kukatisha masomo ili alee ujauzito wake hadi pale alipojifungua.

Kwa Rehma za Alla alijifungua salama usalmin bila shida yoyote na akafanikiwa kupata mtoto wa kiume. Baada ya kujifungua kamati ya elimu katika eneo lake ilimnasihi mtoto huyu ili arudi skuli kujiunga na wenzake aendelee na masomo nayeye akakubali kufanya hivyo.

Masikini mtoto wa watu aliendelea na masomo kwa matumaini lakini kumbe yule adui wa maisha yake kwa vile yupo na anamuona akanza tena kutumia ulaghai wa maneno na kumuahidi vitu tofauti ikiwemo kufunga nae ndoa hivyo nae bila kujijuwa akanasa katika mtego kwa mara nyengine tena.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko nyumbani kwao huku akiwa anabubujika machozi na kulia kwa kwikwi mtoto huyo  amesema yote haya yalijitokeza kwa vile hadi familia yake ilikuwa hampi msaada hata wa kumlea mtoto wake wakati yeye anapo kwenda skuli hali ambayo ilimfanya akatishe masomo miezi sita tuu baada ya kurudi skuli alipokwisha kujifungua.

Mtoto huyo mwenye muonekano mdogo wa umbo na umri huku akiwa analea mtoto mwenziwe ambaye hajuwi hata namna ya kumuhudumia wote wawili wanaonekana kuchoka kwa idhilali ya maisha.

 Na kwa upande wa kiafya wote wawili kimtazamo wa macho afya zao haziko vizuri kwani hicho kichanga kinaonekana kudhofu sana na ngozi yake kujaa vidonda vinavyo ashiria kukosa matunzo stahiki kwa mtoto mchanga. 

Pamoja na muonekano huo kinachosikitisha zaidi ni kuwa kisichana hicho chenye umri wa miaka 15 pamoja na idhilali hiyo tayari anujauzito usiopungua miezi mitano huku mtenda makosa hayo akiwa hajulikani alipo.

Kwa masikitiko ali mueleza mwandishi wa habari hizi kuwa  kabla ya kumpa ujauzito wa mara  hii ambayo ni ya pili alimuambia ananmpenda amkubalie anayoyataka kwani atafunga nae ndowa.

‘’Aliniahidi atanioa ila mwisho wa siku ameshakimbia hajanio’’ Alieleza mtoto huyo.

Aidha amesema anaishi katika mazingira magumu hawezi kumudu kujihudumia yeye mwenyewe pamoja na mtoto wake.

Amesema  amekuwa akipata mateso pamoja na manyanyaso kutoka kwa familya yake kutokana na masahibu hayo ambayo yamemkuta

Hivyo amevitaka vyombo vya sheria kuchukua hatua kali kwa mtuhumiwa huyo ambae amekatisha ndoto za maisha yake.

Mapema mama mzazi wa mtoto huyo aliebakwa na kupewa ujauzito amesema  kesi  hii ya pili ipo kituo cha polisi Kengeja ingawa kwa kesi ya kwanza ilifika mahakamani lakini haikupata ufumbuzi wowote kwani ilidaiwa kuwa haina ushahidi.

Hivyo amelitaka  Jeshi la Polisi  kumsaidia kumtafuta mtuhumiwa huyo ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

‘’Serikali imtafute mtuhumiwa mpaka apatikane’’ Alisema mama mtoto.

Nae baba mzazi wa mtoto huyo amesema yuko tayari kushirikiana na vyombo vya sheria ili kuona mtuhumiwa huyo ametiwa hatiani na mtoto wake kupata haki stahiki.

Sheha wa shehiya hiyo Fatma Khamis Ali amesema nikweli   mtoto huyo wa miaka 15 ambae ni mwanafunzi wa darasa la 5 ana ujauzito wa miezi 5 ambapo  ujauzito  huo ni wa mara ya pili,  na inasemekana alompa ujauzito huo ni yule yule alompa mara ya kwanza na ni mtu wake wa karibu.

‘’saa hizi angekuwa darasa la sita nae kama wenziwe ila yeye ndo kanfikwa ni mitiani kama hiyo.’’alisema sheha huyo.

‘’Tukio la kwanza ambapo ekuwa darasa la nne nililipeleka kituo cha Polisi Kengeja na  kesi ikafika mahakamani lakini haikupatiwa ufumbuzi kwa sababu eti ilikosa ushahidi, na mchovya asali hachovi mara moja tunkaa kashafanya tena vile vile’’alisema sheha huyo huku akieleza kwamba  kesi ya pili  nayo ipo hapo hapo kengeja ambapo wamesema  mtuhumiwa anatafutwa.

Sheha huyo aliendelea kumueleza mwandishi wa habari hizi kwamba hili ni tukio la pili la wanafunzi kupewa ujauzito ikiwa mmoja ni mwanafunzi wa darasa la kumi na moja, kupewa ujauzito kuanzia januari hadi April mwaka huu katika shehia yake.

Kufuatia malalamiko ya kwamba kesi hizi za udhalilishaji kwa baadhi ya shehia imekuwa ngumu kupatiwa hukumu tulimtafuta Kamanda wa Polisi mkoa wa Kusini Pemba Ahmed Khamis Makarani ambapo amesema endapo mtu amefungua kesi yake katika kituo cha Polisi na akiona hapewi mrejesho wowote  asibakie nyumbani bali  afuate  taratibu hadi kufikia makao makuu mpaka ahakishe kesi yake imepatiwa ufumbuzi.




Mratibu wa chama cha wandishi wa habari wanawake Tanzania Zanzibar  [ Tamwa] Ofisi ya Pemba Fathiya Mussa Said amesema wamekua wakitoa Elimu kwa  wanajamii kuhakikisha kesi za aina hii wanazisimamia na kuzitolea ushahidi ili watuhumiwa waweze kutiwa hatiani kitu ambacho kitasaidia kuondoa tatizo la udhalilishaji kwa jamii.

‘’Naiomba jamii wasikubali kusuluhisha kesi za udhalilishaji katika  Serikali za Shehia nahata katika Vituo Vidogo vya Polisi kwani huwa hakuna hukumu na ndio mana ukaona watuhumiwa kila siku warudia makosa hayo hayo’’ alisema Bi Fathiya.




Msaidizi Afisa ustawi wa wanawake na Watoto kutoka wilaya ya Mkoani  Aisha Abdi amesema bado kesi hiyo haijaripotiwa katika ofisi yake na kuwataka waathirika wa tukio hilo kufuata taratibu za kuiripoti ili wasaidiane katiaka kutafuta haki ya muathirika.

Matukio ya udhalilishaji katika shehia ya Mwambe na Kengeja yanaonekana kushamiri kwani katika kipindi cha mwaka jana pia kuna mwanafunzi wa darasa la sita alipewa ujauzito na mtu wake wa karibu kama ilivyo kwa yule wa darasa la tano ambaye mtuhumiwa hajulikani alipo. 

Jumla ya kesi 174 za udhalilishaji zimeripotiwa katika Vituo mbali mbali vya Polisi Mkoa wa Kusini Pemba kuanzia Januari hadi Disemba mwakajana kati ya hizo 88 ziko kwenye upelelezi, 27 zimefungwa, 44 ziko mahakamani, na moja imeondolewa, ambapo za Watoto wanaokinzana na sheria 11 zipo upelelezi, 2 zimefungwa na moja inaendelea mahakamani, Na kuanzia January hadi March mwaka huu ni jumla ya 55 zimefunguliwa katika vituo hivyo vya Polisi.  






Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.