WANAHABARI, WADAU WAOMBA VIFUNGU VINAVYOMINYA UHURU WA HABARI VIREKEBISHWE

 
 

                                          NA FATMA HAMAD,PEMBA

KILA baada ya miaka 10 sheria huwa zinahitaji kubadilishwa ili kuondosha mapungufu ya vifungu ambavyo vitakua haviendani na utekelezaji wa sheria hiyo.

 Ijapo kuwa wakati mwengine sio lazima kusubiriwe hadi itimie miaka 10 ndio  iweze kufanyiwa marekebisho.

Na hii itasaidia kuweka sawa vifungu vyenye mapungufu ili

viweze kuendana na muda na mazingira ya sasa.

Lakini tukiangalia sheria ya Usajili wa Uwakala wa habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanywa marekebisho na Sheria Namba 8 ya mwaka 1997, haiendani na mazingira ya sasa kwani ni  kongwe hivyo inahitajika ifanyiwe marekebisho.

Takriban ni miaka 26 tangu Sheria hiyo kufanyiwa marekebisho ingawa bado baadhi ya vifungu vyake vina mapungufu ambavyo vinaminya uhuru habari.

Miongoni mwa vifungu hivyo ni kifungu cha 30 kinachompa  mamlaka makubwa  Waziri kiasi ambacho kinaminya uhuru wa habari pamoja na kifungu cha 27[1], 27[2].

 Ambapo kifungu cha 27(1), kinasema Afisa Polisi yoyote anaweza kukamata na kupekua majengo ya habari,

Kifungu cha 27 [2]kinaeleza, Hakimu yoyote anaweza kutoa hati na kumuidhinisha afisa yoyote wa cheo cha Inspekta kwa msaada au bila msaada kuingia na kupekua mahala popote pale ambapo inashukiwa kuna gazeti linachapishwa kinyume na sheria

Na Kifungu cha 30 pia kinaeleza kwamba endapo Waziri ataona kuwa ni kwa munafaa Umma au kwa maslahai ya amani na utulivu anaweza kuamuru kufungiwa kwa gazeti.

Na ndo maana wanahabari pamoja na wadau wa habari mbali mbali wamekuwa wakizipigia kelele, ili kuona sheria hizo zinafanyiwa marekebisho, kwa ajili ya kuondosha mapungufu yaliyomo ili iweze kuendana na mazingira ya wakati uliopo.

Wandishi wa habari ndio wadau wa kubwa ambao wanakwazwa na sheria hiyo, walieleza kuwa ni vyema ikaangaliwa tena upya ili iweze kufanyiwa marekebisho.

WANDISHI WA HABARI

Mchanga Haroub Shehe ambae ni Afisa habari Wizara ya Maendeleo ya Jinsia, Wazee na Watoto alisema wakati imefika kufanyiwa maboresho Sheria hiyo ili wanahabari na vyombo vya habari kufanya kazi zao bila kuingiliwa.

"Kwa kweli tunapoiona hii Sheria inatupa wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yetu, kwa sababu ndani yaku kuna vikwazo kwetu," alisema mwandishi huyo.

Mwandishi wa kujitegemea Mohamed Khalfan ili kuwepo kwa uhuru wa habari nchini ipo haja ya kifungu hicho kufanyiwa marekebisho ili kiendane na mazingira ya wakati wa sasa.

"Kwa kweli sheria ya habari ni kongwe kabisa, hivyo Tuna tamani ipitiwe na iangaliwe tena upya kwani haiendani tena na muda," alisema mwandishi huyo.

Time Khamis Mwinyi ambae ni mwandishi wa Redio Jamii Micheweni alisema, sheria ya habari inafaa kufanyiwa marekebisho ili iweze kuendana na mazingira ya Teknolojia.

"Baadhi ya vifungu vya Sheria hii vina mapungufu na sisi ili tufanye kazi zetu vizuri, vinahitaji virekebishwe," alieleza.

WADAU WA HABARI

Shifaa Said Hassan ambae ni Mjumbe wa Bodi kutoka Shirika la Habari Tanzania [MCT]  upande wa Zanzibar alisema miongoni mwa vifungu ambavyo vimekuwa ni kikwazo kwa wandishi wa habari ni kifungu cha 3, na kifungu cha 27(1) vya sheria ya Usajili wa wakala wa habari Magazeti na vitabu No 5 ya mwaka 1988 iliyo rekebishwa na sheria no. 8 ya mwaka 1997.

Alisema ni wakati wandishi wa habari kufanya utetezi wa kina Sheria hizo ziweze kufanyiwa marekebisho ili ziendane na wakati wa sasa.

‘’Kwa kweli sheria yetu imeshapitwa na muda tunaomba ifanyiwe marekebisho ili kuondoa vifungu ambavyo vinakinzana na uhuru wa vyombo vya habari," alisema.

Omar Ali Omar (sio jina lake halisi) kutoka Tasisi ya Moyo Media alisema, uwezo aliopewa Waziri pamoja na mafiasa wengine wakiwemo Polisi na Mahakimu kwenye sheria ya habari ni mkubwa, ni vyema Serikali pamoja na watu wahabari kukaa pamoja ili waweze kuiangalia tena sheria ya habari.

Alisema, ni vyema kwa nafasi ya uwaziri kupewa mtu amba ana fani ya habari ili iwe ni rahisi kuiendesha wizara hiyo kwa ufanisi.

 TAASISI ZINAZOSHUGHULIKIA MASUALA YA HABARI

Mwenyekiti wa Klabu ya Wandishi wa Habari Pemba (PPC) Bakar Mussa Juma alisema, ipo haja kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya habari kwani ilishakua ya zamani, haiendani tena na mazingira ya sasa.

Alisema, Sheria hiyo inathiri uhuru wa habari kwani imempa mamlaka makubwa Waziri ambayo yanapelekea kukosekana kwa uhuru wa habari.

Mratibu wa Chama cha Wandishi wa habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) Ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said alisema, wamekua wakichukua juhudi mbali mbali kuzisemea sheria hizo ili kuona wahusika wanaoshuhulikia, wanachukua hatua kuhusu kilio chao hicho.

"Tunafanya makongamano na wadau mbali mbali pamoja na kuwapa kazi waandishi wa habari nawao waweze kuzisemea katika vyombo vyao ili kuona zinafanyiwa kazi," alisema.

Alisema, endapo sheria hizo zitaendelea kuwa kandamizi hazitowathiri wanahabari tu, bali kutaathiri jamii nzima kwa sababu kutakosekana kupatikana kwa habari.

 
WANASHERIA

Kwa ujumla vifungu vyote ni kandamizi na kwamba kumpa mamlaka Police, kukamata au kupekuwa chombo au mali za mwandishi wa habari ni sababu ya kumtia hofu ya kutojiamini au kutokuwa huru katika kutekeleza majukumu yake ya kazi akijuwa kuwa nyuma yake amenyooshewa mkono wa chuma ambao ni chombo cha Dola, kinataka kumjeruhi, hivyo hapo hakuna uhuru.

Kuhusu kif. 30 nacho ni hivyo hivyo, Waziri kama binadamu ana mapungufu yake, sasa akipewa mamlaka hayo, lazima atakuwa na majivuno na ikitokea kukerwa na jambo au kazi ya mwandishi, ataifungia kwa maslahi yake binafsi na sio kwa taifa. 

"Hii ni kasoro kubwa na haitoi uhuru kwa mwandishi anapoamua kufanya kazi zake, alisema. 

Hivyo vifungu vinahitaji marekebisho au kufutwa kabisa.

 

          

 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.