UGUMU WA MALEZI KWA WANAFUNZI WALIOJIFUNGUA KUNAVYODIDIMIZA HAKI YAO YA KUPATA ELIMU.


 

                        NA FATMA HAMAD, PEMBA

 KUKOSEA NJIA SIO KUPOTEA NJIA.

Binaadamu akipanga lake na Mungu hupanga lake. Ni usemi maarufu iliozoeleka miongoni mwa jamii ya Watanzania.

Usemi huu unatumika kuonesha kwamba kwa kawaida binaadamu huishi kwa kujipangia mambo ya muda mfupi na mrefu, lakini inapokuja utekelezaji huwa ni majaaliwa. Hata hivyo msisitizo ni kwamba ili tufanikisho mambo yetu tunapaswa kujipangia kwa sababu wataalamu wanasema ukishindwa kupanga basi ujue unapanga kufeli.

Ukweli wa maneno ya hapo juu haushii kwa wakubwa pekee bali Hata watoto nao huwa na mipango yao au labda tuite ndoto zao na hii pia huwa na nguvu Zaidi  kwa wanafunzi.  Huyu analenga kusoma na hatimaye awe mwalimu,  yule anata kuwa daktari, mwengine anapenda kuwa mkulima wa kileo, asakri polisi, mhasibu na kadhalika alimradi ndoto zao zinakuwa hazina mwisho

Lakini kama zinavyoitwa hizo ni ndoto na ndoto zinakuwa na mambo mawili ama kutimia zikawa kweli ama kupotea njia.  Mtu anaweza kujiuliza jee ikitokezea ndoto ya mmoja wetu imekumbwa na vikwazo na haikutimia  jee ndio inapaswa kuwa ndio mwisho wa safari, jee haruhusiwi kuota zaidi, jee hapaswi kushikilia ndoto yake?  Jibu ni Hapana. Kila mtu anapaswa kushikilia ndoto yake. Na jambo hili ni muhimu Zaidi ikiwa mhusika ni mtoto wa kike.

Nadhani Hali kama hii ndio iliopelekea kuwepo msemo maarufu katika jamii ya Waswahili  unaosema Kukosea njia sio kupotea njia. Msemo huu una lengo la kuwapa watu fursa ya kujaribu na kuwaaminisha kwamba bado wananafasi ya kufikia wanakotaka Kwenda hata ikiwa awali wali  kosea, katik kutimiza ndoto yake au kateleza katika kuifuata njia ya ndoto yake ,  au kaanguka  kabisa . Msemo huu unatuhamasisha kwamba mtu aliekumbwa na kadhia hiyo hutakiwa ainuke na kujitahidi kuendelea na safari ili afike huko anakokusudia Kwenda bila kujali kilichomtokea awali

Busara za Usemi huu nadhani ndizo zilizoiongoza  Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  na kupelekea  kutoa fursa kwa wanafunzi waliopata ujauzito kurudi skuli na kuendelea na safari yao ya kusoma baada ya kujifungua. Kwa kweli Wizara ya Elimu ilifanya jambo jema na jambo la Mfano kwa Ukanda huu wa Afrika Mashariki kulifanya jambo hili kuwa ni sehemu ya sera yake ya Elimu ya Mwaka 2006.

 Lakini jee fursa hii inatumiwa kikamilifu. Jibu ni Hapana. licha ya kuwepo fursa hii  wasichana wamekuwa wakikosa kuitumia fursa hii kwa sababu tofauti tofauti na kujikuta wakibakia majumbani kulea watoto wenzao.

Kwa mujibu wa ripoti ya tathmini ya Utekelezaji na Mafanikio ya Sera ya kuwaruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shule Zanzibar iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO mwaka 2021 wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo Pamoja na walimu waliyotaja mambo yafuatayo kuwa ndio kikwazo kikubwa cha wanafunzi kurejea. Mambo hayo ni Pamoja na kuongezeka kwa majukumu kwa wasichana hao, unyanyapaa kutoka kwa wanafunzi wenzao, walimu na jamii, kukatishwa kwa usaidizi wa wazazi au jamaa wakaribu, kutokuifahamu sera na kujisikia aibu.

Kwa mujibu wa teporti hiyo waliokatika hatari ya kuwa wahanga wa mimba wakiwa shuleni ni wasichana wa umri wa kati ya miaka 13 hadi 18. Kwa mfano ripoti ya UNESCO ilifafanua kuwa kati yam waka 2005 na 2020 jumla ya Watoto 646 Unguja na Pemba walipata mimba wakiwa skuli. Na kati yao wanafunzi 190 (29.4%) walikuwa na umri wa kati ya miaka 13 hadi 16.

Na katika kundi hili ndipo anapoangukia  huyu binti wa miaka 16 wa Micheweni niliempatia jina la Nuru (sio jina lake halisi). Nuru alipata ujauzito akiwa darasa la 10 katika Wilaya ya Micheweni . Na yeye ni miongoni mwa wale ambao kadhia ya ujauzito alioupata wakati akiwa skuli  ulimkosesha kuendelea na masomo.

Nuru ambaye alikuja kuitwa mama akiwa na umri mdogo  alinielezea kwa masikitiko namna alivyoshindwa  kuendelea  na masomo kwa sababu majukumu yake yaliongozeka. Hayakuwa tena yale ya kuwahi kuamka asubuhi, kusafisha uwanja, kuchota maji, na kujitayarisha Kwenda Skuli pekee. Sasa lilikuwa limeongezeka jukumu la kumlea mtoto. Kumuosha mtoto, kumsafisha, kumlisha, kumbembeleza kwa ufupi ni malezi. Na katika hili ndio alikosa msaada.   Alikosa mtu wa kumlelea mtoto wake au tuseme wa kumsaidia kulea mtoto wake

‘’Nilitamani kuendelea na masomo hadi nifike chuo kikuu, lakini nilishindwa kwa vile sikupata mtu wa kunilelea mtoto wangu,”anasema.

Alisema mama yake hakuweza kukaa nyumbani kumuangalia  mtoto ili aweze kwenda skuli kwa sababu yeye ndie  anaetafuta huduma zote za nyumbani.

Kilichomuumiza zaidi ni kuona mwanaume aliyempa mimba alimtupa na hakukuwa na mawasiliano yoyote kati yao.

‘’ Aliniacha mkono baada ya kutekeleza takwa lake ”, alisema kwa sauti ya unyonge.

Binti mwengine ambae nae ndoto yake ilikatiswa na ujauzito ni Rehema (sio jina lake halisi)  Rehema yeye aliniambia alikuwa na ndoto ya kuwa daktari wa  binadamu, lakini alishindwa kutimiza ndoto hiyo kutokana na majukumu ya kifamilia.

Binti huyu wa miaka 15 kutoka Wilaya ya Micheweni alielezea jinsi matumaini yake ya kupata elimu yalivyofika nusu njia na kwahivyo kushindwa kufikia kusudio lake la kupata elimu ambayo ingemsaidia kujikwamua kimaisha na kuihudumia familia yake.

Sababu ya safari yake kumalizikia njiani ni kubeba mimba wakati akiwa anasoma na hio kupelekea baada ya kupata ujauzito familia yote kumtenga na kujikuta anaishi  katika maisha ya kutanga tanga.

‘’Nilijikuta naishi katika mazingira magumu kwani familia na majirani pia walinitenga’, alisimulia kwa unyonge.

Licha ya kuwa na mzigo wa malezi ya mtoto bado alikuwa na hamu ya kurudi skuli, lakini haikuwezekana kwa vile  hakupata mtu wa kukaa nyumbani na mtoto wake.

“ Nilitamani nibebe mwanangu mgongoni ili niende nae Skuli ila niliona ni aibu na nikalazimika kubakia nyumbani na kumhangaiki mwanangu”, aliongeza, anaeleza.


 WALIOFANIKIWA KUREJEA SKULI

Mtu anaweza kujiuliza jee hakuna wanafunzi waliorejea skuli baada ya kujifungua . Jibu ni kwamba wapo Licha ya kuwepo vikwazo vya kila aina bado wapo ambao baada ya kujifungua walirudi skuli, wakaendelea na masomo.

Mmoja wa  Wanafunzi hao ni Tumaini (sio jina lake halisi) mwanafunzi aliyerudi skuli kuendelea na masomo baada ya kujifungua aliishukuru serikali kwa kuruhusu wanafunzi waliokata masomo baada ya kupata uja uzio kuweza kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Alichofanya huyu binti ni kukiri kwa wazazi wake kwamba alifanya makosa na mama yake na mwalimu wakamtaka asikate tama na kumtaka arudi skuli baada ya kujifungua na akakubali.

‘’Nilipata ujauzito nikiwa darasa la tisa, na baada ya tu ya kujifungua sikusikiliza maneno ya watu. Nilirudi skuli na mwaka huu naingia darasa la 12,alieleza.

Alieleza kuskitishwa na kuona mwanamme aiyempa ujauzito alimkimbia na kwanza familia yake ilimtenga.

Baba yake alishafariki na anaishi na mama ambaye ndio pekee anayemsaidi kwa huduma zote na ili apate mafanikio hivi sasa anafanya kila bidii ili afuzu mtihani wa taifa wa darasa la 12.

 

‘’Ndoto yangu ni kuwa askari polisi ili nije kuwa mkombozi wa familia yangu na kuchangia maendeleo ya nchi yangu’’ aliongeza.

Msichana mwengine alierudi skuli baada ya kujifungua ni Mariam (sio jina lake halisi) Yeye alisema  alipata ujauzito akiwa darasa la 10 na baada ya kjifungua alirudi skuli na kuendeleza  masomo na wenzake, mariam alisaidiwa na mama yake kulea mtoto wake hadi akafanikiwa kurudi skuli na tayari ameshamaliza  darasa la 12 na anatarajia kujiunga na chuo kwani ndoto zake ni kuwa Mwalimu.

Kwa mujibu wa repoti ya UNESCO nilioitaja hapo awali miongoni mwa sababu zinazowafanya wasichana kurudia skuli baada ya kujifungua ni uungwaji mkono na wazazi na walezi, kujutia mkosa walioyafanya na kujenga matumaini mapya, kupata nasaha kutoka kwa watu wenye ujuzi.


 

KAULI ZA WAZAZI

Nilipomuuliza kwa nini inakuwa vigumu kwa wazazi kuwasaidia Watoto wao waliopata ujauzito jukumu la malezi ili waweze kuendelea na masomo, Bi Asha Omar (50) ambae sio jina lake halisi  alisema  si kwa sababu hampendi mtoto wake  arejee Skuli. La hasha, Sababu kubwa ni kwamba alikuwa  hawezi kukaa kitako kulea mtoto kwani yeye ndie baba na ndie mama wa nyumba na huduma zote anazitafuta yeye.

‘’Huyo mtoto mchanga na huyo mama yake wote wananitegemea. sasa nikishakaa nyumbani  na mtoto hizo huduma watazipata wapi ”,aliuliza.

Kazi anayoitegemea kimaisha ni kilimo cha mwani, hivyo  ni lazima atoke ili akawatafutie chakula pamoja na huduma nyengine muhimu.

Anaeleza sababu kubwa inayompelekea mwanawe kushindwa kurudi Skuli ni kukosa mtu wa kumlelea mtoto.

“ Sijakataa binti yangu kurudi skuli, lakini hali yetu ya maisha nyumbani ni mbaya, siwezi kukaa na kulea mtoto kwani akirudi  atakuwa ananiangalia mimi nimpe huduma zote na mtoto wake”, alisimulia  huku machozi yakimtoka.

‘’Nyumbani nina watoto 7 halafu yeye na mtoto wake  wananitegemea mimi. Hivyo kweli nitaweza kukaa nyumbani kumlelea mtoto ili aende Skuli? Kwa kweli huo ni mtihani” ,alisema.

WANAHARAKATI

Mwanaharakati, Fathiya Mussa Said  kutoka Chama  cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Ofisi ya Pemba ,alieleza kuwa wapo watoto ambao wanashindwa  kurudi skuli kuendelea na masomo wakishajifungu kutokana na wazazi kushindwa kuwasaidia ulezi.

‘’Tunao watoto wetu wengi ambao wanapata ujauzito, wengine kwa kubakwa, ambao wanakosa haki yao ya elimu. Hivyo hulazimika kukaa nyumbani kwa vile wazazi wao hawana muda wa kukaa na watoto wao kwa maelezo kwamba wanatingwa na kazi zao”, alisema. 

Aliwaomba wazazi wawape mashirikiano licha ya kuwa wameshapata mtihani na wanapaswa kufahamu hawa watoto wanastahili kupata elimu licha ya kupata huo mtihani wa uja uzito.

 Bi hidaya Mjaka Ali kutoka Umoja wa Wanawake wa Watu wenye Ulemavu kisiwani Pemba alsema kikwazo kikubwa kinachopelekea watoto wengi wanaopata ujauzito kushindwa kurudi skuli ni kukosa mashirikiano kutoka kwa wazazi wao.

‘’Tumekuwa tukishuhudia mtoto akishapata ujauzito familia yote inamtenga, hapati msaada wowote na  huwa anaishia tu kudhalilika zaidi au kujingiza tena kwenye udhalilishaji ili apate matumizi na huduma kwake na mtoto”, alisema.

 
Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Muhammed  Nassor  Salim, alisema licha ya Wizara kuwapa fursa ya wanafunzi waliopata ujauzito kurudi skuli mara baada ya kujifungua bado kuna baadhi ya wanafunzi hawafaidiki na fursa hiyo.
Alisema lengo la kutoa fursa hio ni kutaka watoto wote wapate haki yao ya elimu hadi sekondari, jambo ambalo litasaidia kupatikana kwa wataalamu katika sekta mbali mbali.

Alisema  wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwarejesha skuli wanafunzi waliopataa ujauzito na wanaendelea na masomo  na wengine wameshafika hadi kidatu cha sita.

Alisema  kwa mujibu wa sera ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar hakuna sababu kwa mwanafunzi anayepata mimba wakati akiwa  masomo kuacha skuli na ndio maana anaruhusiwa kuendelea na masomo akishajifungua.

Alisema Sera ya Elimu imejenga mazingira mazuri kwa mtoto wa kike kuhakikisha anapata Elimu ya kiwango chochote kile atakachojaaliwa nacho bila ya kuwepo kwa vikwazo.

TAKWIMU

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Naibu Mrajisi Wizara ya Elimu Pemba, kuanzia Januari 2022 hadi Disemba 2023, kisiwani Pemba, wanafunzi 74 walipata ujauzito na kati ya hao 40 walifanikiwa kurudi Skuli kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.

Ambapo waliopata uja uzito kwa wilaya ya Chake chake ni 22, wete 18, Mkoani 30 na Micheweni ni Wanne [4].

 MWALIMU WA SKULI.

Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Makangale, Salim Mkadam Hamad, alisema bado elimu inahitajika kwa jamii kuona umuhimu wa kuwaunga mkono watoto wanaopata  ujauzito ili kuhakikisha wanarudi skuli kuendelea na masomo.

Aliishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuwapatia fursa mbali mbali za kimaendeleo wale ambao wamejenga uthubutu wa kurudi skuli baada ya kujifungua, kwani kutajenga hamasa kwa wanaona hapana haja ya kurudi skuli.

Jumla ya wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari  Tanzania ni 18,708 waliopata ujauzito wameripotiwa kurejea maskulii kuendelea na masomo baada ya kujifungua katika kipindi cha miaka ya 2022 na 2023.
Hayo yamebainika katika kilele cha siku ya mtoto wa kike Duniani mnamo 11 October 2023 ambapo takwimu zinaonesha Mwaka 2022 wanafunzi 9,379 wa shule ya msingi walirejea shuleni baada ya kujifungua huku wanafunzi wa shule ya sekondari wakiwa ni 8154 na kufanya jumla yao kuwa wanafunzi 17,532.

Chanzo wasafi FM

 SERA

Sera ya wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ni kuhakikisha inadumisha misingi iliyowekwa na marehemu Abeid Amani Karume mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya 1964, ya utoaji wa Elimu kwa wote bila ya ubaguzi wa Rangi, Kabila, Dini na mwengineo wowote.

SHERIA

Sheria ya Elimu Zanzibar ya mwaka 1982 imeweka mkakati wa kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya elimu kuanzia Msingi hadi Sekondari.

KATIBA

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia kifungu cha 6 [2] kinaeleza kila Mzanzibari, kwa misingi ya katiba hii ataweza kufaidi haki na fursa zote anazostahiki Mzanzibar.

MKATABA WA AFRIKA,

Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka [1999] kipengele cha 11 kinasema watoto wote wanayo haki ya kupata Elimu.

MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA,

Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka[1989] kipengele cha 28 kinaeleza Mtoto anahaki ya kupata Elimu. 


 

                                         

 


 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.