KOSA LA ULAWITI LAMSABABISHIA KWENDA JELA MIAKA 7
MSHITAKIWA Nuhu Kombo Nuhu miaka 19, mkaazi
wa Kijichame wilaya ya Micheweni, amehukumiwa kwenda chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka saba ‘7’ na kulipa fidia ya
shilingi milioni 1, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumlawiti kijana mwenzake
mwenye ulemavu wa akili.
Mwendesha
mashtaka wa Serikali kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka, Juma Mussa Omar alisema
kosa alilolifanya kijana huyo ni kitendo kibaya ndani ya jamii.
Alisema,
kila siku jamii imekuwa ikilalamikia uwepo wa matendo hayo, hivyo kama kila
upande umeshatekeleza wajibu wake ni wakati sasa wa mahakama kutoa adhabu kali.
‘’Jamii
imekua na kilio kikubwa juu ya matukio ya udhalilishaji wa kijinsia, hivyo
tunakuomba utoe adhabu kwa mujibu wa kifungu kinavyoelekeza, ili iwe fundisho
kwake na wengine wenye tabia kama hiyo,’’alishauri.
Baada ya
kupanda kizimbani na kusubiri asomewe hukumu yake mshtakiwa huyo, aliomba
mahakama hiyo impunguzie adhabu kwani bado ni kijana mdogo na anafamilia inayomtegemea.
‘’Mheshimiwa
hakimu naomba mahakama yako inipe adhabu ndogo japo kifungo cha nje tu,
nitakuja kufyagia ofisini kwako au hata Hospitali,’’aliomba mshitakiwa huyo.
Hakimu wa
mahakama ya mkoa inayoshughulikia makosa ya udhalilishaji mkoa wa Kaskazini
Pemba Abdulrahman Ali Abdul rahman alisema kesi hiyo imesikilizwa ikiwa na mashahidi
wa watano, ambao ulitosha kuishawishi mahakama kumtia hatiani.
‘’Mashahidi
walioletwa na upande wa mashtaka, ulikidhi vigezo na haukucha chembe ya shaka,
hivyo kuishawishi mahakama kumtia hatiani mshitakiwa Nuhu,’’alieleza.
Tukio hilo
lilitokea Disemba 13, mwaka 2021, majira ya saa 1:30 asubuhi eneo la Kijichame
wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo mshitakiwa huyo, alimlawiti
kijana mwenye ulemavu wa akili.
Kufanya
hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 116 (1), cha sheria Adhabu nambari 6 ya
mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.
Comments
Post a Comment