UKOSEFU WA WALIMU MJUMUISHI BADO NI KIKWAZO KWA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU

 

          NA FATMA HAMAD PEMBA. 17/10/2022

Wazazi  wa watoto wenye ulemavu  mkoa wa kaskazini Pemba wameikumbusha Serikali ya mapinduzi Zanziber  kuboresha miundo mbinu ya wanafunzi wenye ulemavu maskulini ikiwemo kuweka walimu wanaojua lugha za alama ili watoto wao nawao waweze kupata haki yao ya elimu.

 Wakizungumza  na mwandishi wa habari hizi  kwa nyakati tofauti wamesema watoto  wengi wenye ulemavu bado wanaendelea kuikosa haki yao ya elimu kutokana na kukosa wakalimani.

 Mmoja wa wazazi hao bi Asha Omar kutoka micheweni alisema  kuwa Skuli nyingi za mkoa wa kaskazini  Pemba hususan wilaya ya micheweni hazina walimu wenye ujuzi wa elimu mjumuishi hivyo wanashindwa kuwapeleka skuli watoto  wao waliopata mtihani wa ulemavu.

 ‘’Tunakilio kikubwa jamani watoto wetu wenye ulemavu hawasomi wanakaa tu majumbani kwani hata wakienda skuli hawafahamu chochote kinachofundishwa’’alieleza bi Asha.

Kwa upande wake baba mzazi wa Salum  Said Asaa mwenye ulemavu wa macho  kutoka Kwale Gongo alisema  kuwa yeye mtoto wake alishindwa kumpeleka skuli kwani anahisi ni kwenda kupoteza muda tu haoni anachokwenda kukisoma na kukifahamu.

‘’Mimi mtoto wangu  alishafika darasa la pili ila nimeshindwa kumpeleka skuli kwani hakuna mwalimu wa kumfundisha yeye , bali  namuacha ande chekechea tu ili apoteze muda tu mana hata kwenye matokeo yake ni mabaya”, alieleza mama mzazi wa Salum.

Nae bi Time Bakar Alawi kutoka Kiuyyu mbuyuni aliitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufanya jitihada ya kuwasomesha walimu lugha ya alama kwa ajili ya wenye ulemavu ili nawao waweze kusoma kuanzia msingi hadi vyuo Vikuu.

Mapema mjumbe kutoka shujuwaza Aziza Alawi Mussa alisema licha ya changa moto hiyo ya uwepo wa uhaba wa walimu mjumuishi aliwashauri wazazi hao kuwatoa na kuwapeleka skuli waweze kuchanganyika na wenzao ili  wajihisi kama nawao ni binadamu wenye haki.

Mratibu wa baraza la  taifa la watu wenye  ulemavu kisiwani Pemba Mashavu Juma Mabrouk alisema  suala la uhaba wa walimu mjumuishi bado ni tatizo, hivyo ameishauri  wizara ya elimu kuwapa kipaombele walimu ambao wamesomea fani ya ukalimani wakati zitakapotokea ajira ili kuona changamoto hiyo imeondoka.

‘’Niishauri wizara ya elimu wakati itakapotoa nafasi za ajira kuwajiri walimu wengi waliosomea elimu mjumuishi ili kuona wanafunzi wenye ulemavu nawao wamefaidika na elimu’’ alieleza Bi Mashavu.

Kaimu Mratibu Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha ‘EMSM’ Pemba Halima Mohamed Khamis, alisema ujio wa dhana hiyo ndio iliyokomboa watoto

wenye ulemavu na wale wenye mahitaji maalum, sasa kupata haki yao ya elimu.

Anasema, awali watoto wenye ulemavu wa aina mbali mbali, waliachwa bila ya kupatiwa elimu, kuanzia ngazi ya jamii na serikali kuu.

Lakini ilipofika mwaka 1991 serikali kupitia wizara ya Elimu ilianzisha madarasa maalum, kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili, ambapo kwa Pemba ni skuli za Michakaini na Pandani msingi.

Kisha mwaka 2006, sasa kukazaliwa dhana ya elimu mjumuisho, ambayo ni ule mpango wa kuwaweka darasa moja katia ya wanafunzi wenye mahitaji na wale wa kawaida.

Anasema, mpango huo ulianza kwa kusua sua, maana ulikuwa mpya kwa wanafunzi wenye mahitaji na wale wengine Ambapo hadi sasa, wapo waalimu watano wenye Master, 10 wenye digrii, wakati wenye diploma 20 na 68 ngazi ya cheti wote wana fani ya Elimu ya Mahitaji Maalum ‘SNE’

‘’Licha ya takwimu hiyo lakini bado tunashida ya walimu mjumuisho, hivyo tunaiomba wizara husika kuliweka somo la lazima  katika vyuo ili kila mwalimu akitoka chuoni aweze kusomesha wanafunzi wenye ulemavu maskulini.

Kaimu Mratibu alisema wanao wanafunzi wenye uoni hafifu 803, wenye usikivu hafifu 690, wenye ulemavu wa matamshi 405, wenye vichwa vikubwa na vidogo 22.

Kundi jengine ambalo wanalo katika skuli mbali mbali ni wenye umbikimo 13, mgongo wazi 7, ulemavu wa akili 111, ulemavu mchanganyiko 113 na ulemavu wa viungo wanafunzi 91.

Kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2006 sheria ya watu wenye ulemavu  miaka zaidi ya 40 iliyopita, ilikuwa ni adimu na ni kichekesho kumkuta mwanafunzi mwenye ulemavu, hasa wa viungo, au wa akili akiwa ni mmoja kati ya wanafunzi.

Kwa kawaida, wenye ulemavu na hasa kabla ya kupitishwa kwa sheria yao, nambari 9 ya mwaka 2006, wazazi na walezi wakiishia kuwakomelea majumbani.

Haki ya elimu, haki ya kucheza, kushiriki na kushirikishwa kwao, ilikuwa ni ndoto ya mchana, na hawakuonekana kama sehemu ya jamii.

 

 

 

 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.