KIJANA ASSA MWENYE ULEMAVU WA VIUNGO AOMBA MSAADA APATIWE MTAJI
NA FATMA HAMAD, PEMBA.
KIJANA
Assaa Khamis Hamad mwenye umri wa miaka 35 mkaazi wa Shumba Vyamboni wilaya ya
Micheweni Pemba ameomba Serikali pamoja na wahisani wamsaidie mtaji ili
aendeleze biashara zake ambazo humpatia kipato cha kuhudumia familia yake.
Kijana huyo mwenye ulemavu wa viungo
anafanya biashara ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na njugu nyasa na Vocha kwa
lengo la kujipatia kipato kitakacho msaidia na familia yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi kwenye machimbo ya mchanga huko Shumba Vyamboni Assaa alisema, hawezi
kufanya kazi ngumu kutokana na hali yake kwani ulemavu alionao ni wa
miguu na mikono.
Alisema kuwa, kwa sasa hafanyi
biashara hizo kutokana na kukosa fedha za kununulia vocha pamoja na njugu,
jambo ambalo anashindwa kuihudumia familia yake.
“Naiomba Serikali, wahisani na
taasisi zinazosaidia, wanipatie mtaji angalau wa shilingi milioni mbili ili
nifanye biashara kubwa itakayonitatia kipato kikubwa kitachonikwamua kimaisha”,
alisema kijana huyo.
Alieleza kuwa, ameamua kuanzisha biashara
ili kujikimu kimaisha inagawa anakwama kutokana na kukosa fedha ya kununulia
bidhaa hizo, jambo ambalo linamuhuzunisha sana.
“Natoka nyumbani kwangu kwa kigari
(wheelchair) hadi kwenye machimbo ya mchanga kuuza njugu na vocha, wateja wangu
ni madereva na wanaochimba mchanga, lakini inafika miezi miwili sina nimekaa tu
sina biashara yeyote, naiomba Serikali inisaidie mtaji”, alisema.
Alieleza kuwa, hana mtu wa kumsaidia
kutokana na kuwa wazazi wake hawana uwezo kwani wamezaliwa wanne wakiwa na
ulemavu kama wake.
“Nina ndungu zangu wawili wenye
ulemavu wa viungo kama mimi na mmoja alikufa kwani tulikuwa wanne, hivyo sina
wakunisaidia na ndio maana napambana mwenyewe lakini nafikia pahala nashindwa”,
alifahamisha Assaa.
Alisema kuwa, ana mke na watoto wawili
ambao wanamtegemea, ingawa anashindwa kuwahudumia kutokana na kukwama katika
biashara zake hizo ambazo ndizo zinazompatia kipato.
Alisema licha ya hali ya ulemavu
anayoishi nayo, lakini hapendi kuishi katika maisha ya utegemezi na ndio maana
alijiajiri mwenyewe, hivyo ni vyema wakahurumiwa na kusaidiwa.
Kwa wao vibarua wanaochimba mchanga
walisema kuwa, licha ya ulemavu alionao kijana huyo lakini amejiajiri mwenyewe
kwa kuuza biashara ya vocha na njugu, ili kujikimu inagawa anakwama kutokana na
kukosa mtaji.
“Kwa kweli hali halisi ya kimaisha
ya kijana Assaa sio nzuri, anaishi katika hali ngumu huku akiwa mikono yake
haina nguvu na wala hawezi kutembea, ambapo hutumia kigari kufika hapa
machimboni, hivyo tunaomba wahisani wamsaidie kwani akili yake iko vizuri na
hapendi kujituliza”, alieleza.
Nao baadhi ya madereva wanaokwenda
kuchukua mchanga katika eneo hilo walisema kuwa, wanamunga mkono kijana huyo
kwa kumpatia pesa ili aweze kujisaidia mahitajio yake, ingawa haikidhi mahitaji
yake kwani ni kiwango kidogo sana wanachompatia.
Mratibu Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi Haji Khamis Haji alifahamisha kuwa, wao wanatoa fedha kwa mkopo katika
vikundi mbali mbali na sio vyenginevyo.
Nae Mratibu
wa Idara ya watu wenye ulemavu Kisiwani Pemba
Mashavu Juma Mabrouk amesema wanao mfuko
maalum ambao wanawawezesha wajasiriamali
wenye ulemavu.
Amefahamisha
kuwa lengo la kuwepo kwa mfuko huo ni kuwasaidia
Mtaji watu wenye ulemavu ambao wanataka kujiajiri wenyewe kwa kuanzisha
biashara zao ambazo zitawapatia kipato.
Aidha amefahamisha
kua mkopo huo hupewa mtu yoyote mwenye
ulemavu anaeuhitaji kwa ajili ya kuanzisha bila ya kuwepo kwenye kikundi
chochote cha ujasiriamali.
Comments
Post a Comment