CHANJO INAYOENDELEA KUTOLEWA KISIWANI PEMBA NI KWA AJILI YA KIPINDU PINDU NA SIO KWA AJILI YA KORONA WANANCHI WATOLEWA HOFU

NA FATMA HAMAD FAKI PEMBA.




Mratibu wa huduma ya chanjo  kisiwani Pemba Bakar Hamad Bakar  amewatoa hofu Wananchi kuwa  chanjo inayoendelea kutolewa kisiwani hapa   ni kwa ajili ya kinga dhidi ya kipindu pindu na sio ya kinga dhidi ya  Corona, kama wananchi wanavosema.

 Bakar ameyasema hayo wakati akizungumza   na  waandishi wa habari kufuatia  kuzuka  kwa zana juu ya chanjo ya kipindu pindu inayotolewa.

Alisema, kwa sasa wizara ya Afya inaendelea na awamu ya pili ya chanjo hiyo kwa njia ya matone, kwa wananchi waliopata awamu  ya kwanza.

Alieleza kuwa, sio sahihi kuwa chanjo hiyo ni ya Corona, kama wanavosema  kwani chanzo ya Corona haitolewi kwa njia matone.

“Niwatowe wasi wasi wananchi kuwa, hii inayoendelea kwa sasa sio chanjo kwa ajili ya Corona, bali ni kwa ajili ya kipindupindu, hivyo wajitokeze kumaliza dozi awamu ya pili,’’alieleza.

Aidha Mratibu huyo alisema, bado chanjo ya Corona haijawasili kisiwani Pemba, na hivyo ikiwasili wananchi wote watapewa taarifa .

Alifafanua dozi ya kwanza ilianza baina ya Julai 3 hadi Julai 7 mwaka huu, na hii ya pili inatarajiwa kuanza Agosti 7 hadi 11 mwaka huu.

Alisema  kuwa zoezi hilo linafanyika  wilaya ya Micheweni na Wete mkoa wa kaskazini Pemba, ambapo hiyo ilikuja kutokana na  ripoti yao ya mwisho, ikionesha baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo kuna wagonjwa wa kipindu pindu.

Alizitaja shehia ambazo zinafanya zoezi hilo kwa awamu ya pili ni Micheweni, Maziwang’ombe, Kiuyu Mbuyuni, Shanake, Chamboni kwa wilaya ya Micheweni na shehia za Kiuyu Minungwini na Kojani kwa wilaya ya Wete.

Hata hivyo amewataka  wananchi  ambao walipata dozi ya  mwanzo  ya chanjo kwa njia ya matone wajitokeze kukamilisha dozi hiyo ‘full doze’.

Kuhusu kudumu kwa chanjo hiyo ndani ya mwili wa mtu aliyepata kinga, alieleza inaweza kudumu  zaidi ya miaka mitatu, ingawa baadae huanza kushuka taratibu.

“Ukipata chanjo ya kinga ya kipindu pindu, unaweza kuishi nayo angalau kuanzia miaka mitatu, na kisha na kuanzia miaka minne na mitano huanza kushuka taratibu kinga hiyo,’’alifafanua.



Nae Mratibu wa elimu ya afya Pemba Abeid Ali Ali, alisema zoezi hilo haliwahusishi wajawazito na watoto waliochini ya umri wa mwaka mmoja.

Kuhusu maeneo yenye kujirudia rudia kwa wagonjwa wa kipindi pindu ikiwemo kisiwa cha Kojani wilaya ya Wete, alisema wanaaendelea na mikakati maalum.

“Moja ya mkakati ambao sasa tumeshafanikiwa ni kuondoa chanzo cha maji kilichokuwa kimetuwama na kua zalio kuu la vimelea vya ugonjwa huo,’’alifafanua.

Waandishi wa habari walisema, lazima mkazo uwekwe kwenye maeneo sugu yanayojitokeza kwa wagonjwa wa kipindu pindu.

JUHUDI ZA SMZ
Mwaka 2019 ilizindua mpango wa kutokomeza kipindu pindu unaolenga kuondosha vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo kwa kusimamia sheria na miongozo inayosimamia usafi wa mazingira na chakula.

Mpango huo wa miaka kumi unahusisha Wizara na Sekta mbali mbali katika utekelezaji wake ambapo unalenga kuwepo kwa hatua za haraka mara tu ugonjwa huo utakapojitokeza pamoja na kupanua wigo na ufanisi, huduma za kinga na upatikanaji wa maji safi na salama.


Mpango huu ulizinduliwa mnamo Septemba 10, 2019 na Rais msataafu wa awamu ya saba Dk. Ali Mohamed Shein ambapo katika hotuba yake alieleza kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya afya na nchi kwa jumla.

alisema kuwa maradhi ya kipindupindu ni hatari mno na yanaendelea kutishia ustawi wa watu na uchumi katika nchi na mataifa mbali mbali duniani.

Tangu mwaka 1817 hadi mwaka 1975 jumla ya miripuko saba mikubwa iliyoenea katika mataifa mbali mbali kwa kipinidi kimoja imeshatokezea.

Miripuko hiyo imesababisha athari kubwa za kiuchumi na kijamii pamoja na kuteketeza idadi kubwa ya watu duniani.

Kwa upande wa Zanzibar inasemekana kwamba mripuko wa kwanza ulitokea katika robo ya mwisho ya karne 19, baadhi ya waandishi walieleza kwamba mripuko huo ulitokea katika mwaka 1888.

Katika mripuko huu ilikisiwa kwamba watu wengi (kwa maelfu), walifariki na walizikwa katika maeneo mbali mbali katika sehemu karibu na fukwe za bahari na katika maeneo ya Ng’ambo.

Mripuko mdogo ulitokea katika kisiwa cha Tumbatu mwanzoni mwa mwaka 1978 ambao uliwasibu wavuvi waliokwenda kuweka dago katika maeneo ya pwani ya Dar es Salaam.

Mripuko wa pili mkubwa ulitokea Mjini Unguja hapo Machi, 1978, ambapo watu wengi waliathirika na ugonjwa ulienea hadi katika baadhi ya mashamba yaliyo karibu na Mjini.

Baada ya mripuko huo mkuu wa mwaka 1978, mripuko mwengine mkubwa wa kipindupindu ulitokea mwaka 1998 na baada ya hapo miripuko ikitokezea takriban kila mwaka na ilisababisha vifo na athari mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Jumla ya miripuko 19 tangu kipindi hicho imeshatokezea hapa Zanzibar, ambapo zaidi ya wagonjwa 14,364 wameuguwa kipindupindu na vifo 210 vimeripotiwa kutokana na maradhi hayo.

Miripuko hiyo imekuwa ikitokezea wakati au mara tu baada ya msimu wa mvua kubwa, hasa za masika na vuli za kila mwaka.
Takwimu zinazotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kwamba miripuko mingine midogo midogo ya maradhi haya imekuwa ikitokezea kila mwaka katika nchi au maeneo tafauti.

Inakaridiwa kwamba mirupuko hii imekuwa ikiathiri kati ya watu milioni 1.3 hadi milioni 4 kila mwaka, na husababisha vifo vya watu kati ya 21,000 hadi 143,000 kila mwaka.





Comments

Popular posts from this blog

UTELEKEZAJI WA WANAWAKE UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WATOTO.

Mkuu wa Polisi Jamii Kaskazini Pemba akerwa na wanao wafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Mrajisi wa Mahakama Zanzibar ahidi kula sahani moja na Mahakimu wasio wadilifu.